Saturday 2 November 2013

Tusikubali kuivunja Jumuia ya Afrika Mashariki

Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta. PICHA|MAKTABA 
Na Mwananchi

Posted  Ijumaa,Novemba1  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Vilevile, Sitta alisema Tanzania haitahudhuria mikutano ya Jumuiya hiyo yenye ajenda ambazo nchi hizo tatu zimekubaliana na kuwa na msimamo wa pamoja, huku ikiwaagiza watendaji wake kutotoa majibu ambayo yatachukuliwa kama msimamo wa nchi.


Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa sasa inapitia katika kipindi kigumu baada ya nchi za Rwanda, Uganda na Kenya kuanzisha ushirikiano wa peke yao huku zikizitenga Tanzania na Burundi.
Ushirikiano ulioanzishwa na nchi hizo unahusu maeneo ya miundombinu, biasharana viza; ushirikiano ambao umezikera nchi za Tanzania na Burundi.
Tayari Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta imetoa msimamo bungeni kuhusu kuchukizwa na kitendo hicho, ambacho kinaonyesha wazi kuwa yanayofanyika siyo dalili njema kwa jumuiya hiyo.
Sitta aliliambia Bunge juzi kuwa Serikali ya Tanzania imechukua hatua kadhaa mpaka sasa ikiwamo kutaka ufafanuzi kutoka Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba baada ya wiki mbili ikishapata majibu itatoa msimamo wake.
Vilevile, Sitta alisema Tanzania haitahudhuria mikutano ya Jumuiya hiyo yenye ajenda ambazo nchi hizo tatu zimekubaliana na kuwa na msimamo wa pamoja, huku ikiwaagiza watendaji wake kutotoa majibu ambayo yatachukuliwa kama msimamo wa nchi.
Tangu nchi ziitenge Tanzania na Burundi, yapo maoni mengi ambayo yamekuwa yakitolewa na Watanzania ikiwamo kuzishauri nchi zilizobaguliwa kuunda umoja wao ambao utajumuisha nchi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Tunachukua fursa hii kutoa msimamo wetu kuwa chokochoko zinazofanyika kuivunja jumuiya hii hatukubaliani nazo, kwani tunaamini kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki bado ni muhimu kwa wanachi mmoja mmoja, na kwa nchi wanachama.
Zipo faida nyingi ambazo nchi wanachama zimeshaanza kupata hata kabla ya kufikia kwa shirikisho kamili. Moja ya faida hizo ni ushirikiano wa kibiashara na kuondelwa kwa vikwazo vya kibiashara katika nchi hizo na kuanzisha ushuru wa pamoja wa forodha.
Inashangaza kuona wakati nchi nyingi duniani zikikimbilia kuungana ili kuwa na nguvu kiuchumi, sisi Afrika Mashariki tunaaanza kugawanyika kwa sababu zisizokuwa na mashiko. Tunaamini kuwa chokochoko hizi zinazofanyika kwa manufaa ya baadhi ya viongozi waliopo madarakani katika nchi zilizoamua kuanzisha umoja ndani ya jumuiya, hivyo tuzipuuze kwa kujenga hoja badala ya kukimbilia kujitoa.
Hata yale madai ya siku nyingi kuwa Tanzania inakatalia ardhi yake kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa nchi washirika hayana msingi na hayawezi kuwa sababu ya nchi hizo kujitenga wala kufanya mambo ya peke yao.
Kama wahenga walivyosema umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hivyo hakuna nchi inayoweza kupata maendeleo peke yake kama kisiwa bila kuwashirikisha majirani zake wala nchi nyingine kama washirika wa maendeleo. Litakuwa ni jambo la ajabu, kuona nchi ambazo zimekuwa zikikaa pamoja kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali za kuendeleza miundombinu na kupanua biashara baina yao ghafla zinaparaganyika na kila moja kuelekea njia yake.
Tulitarajia kwamba mafunzo yaliyopatikana kutokana na kuvunjika kwa jumuiya ya awali ya Afrika Mashariki mwaka 1977 yalitosha, kumbe bado wapo watu wenye agenda binafsi ambazo zisipokemewa zitaathiri hata jumuiya hii ya sasa.
Tunachukua fursa hii kuwashauri marais wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki kuacha kutanguliza maslahi yao mbele, badala yake wafikirie maslahi ya nchi zao. Umoja huu siyo wa viongozi waliopo madarakani. Marais waliopo sasa katika nchi za Afrika Mashariki wataondoka, lakini Rwanda, Kenya, Uganda, Burundi na Tanzania zitabaki.

SOURCE: MWANANCHI