Saturday, 5 October 2013

Assad aisuta Uturuki, aiambia 'itajuta' kuunga mkono waasi


Na AFP

Posted  Ijumaa,Oktoba4  2013  saa 17:59 PM
Kwa ufupi

Katika mahojiano na televisheni ya Uturuki, Assad amesema Uturuki imekuwa ikitumiwa kuwafadhili wapinzani hao bila kutambua kwamba hao hao ndiyo watakaoigeuka na kuisambaratisha nchi hiyo jirani na Syria.


Damascus. Rais wa Syria, Bashar al-Assad ameionya Uturuki kwamba itajutia kuwaunga mkono waasi wanaopambana dhidi ya kuondoa utawala wake madarakani.
Katika mahojiano na televisheni ya Uturuki, Assad amesema Uturuki imekuwa ikitumiwa kuwafadhili wapinzani hao bila kutambua kwamba hao hao ndiyo watakaoigeuka na kuisambaratisha nchi hiyo jirani na Syria.
Alisema ni wazi kwamba katika siku za baadaye wapinzani hao wanaotumiwa kuivuruga Syria na kutaka kuifanya iwe nchi isiyotawalika wataiathiri pia Uturuki na nchi hiyo itapata tabu kwa mchango wake wa kuwaunga mkono waasi.
Aidha, Assad alisema ni  jambo lisilowezekana kuwatumia magaidi karata yako na kutembea nayo mfukoni kwa sababu ni sawa na kumtumbukiza nge katika mfuko wa suruali, ambaye bila shaka hatosita kukung'ata wakati wowote.
Uhusiano kati ya Uturuki na Syria, nchi ambazo zilikuwa washirika wa karibu umeharibika  tangu kuanza kwa harakati za kutaka kuuondoa madarakani utawala wa Assad Machi mwaka 2011.
Harakati hizo zimegeuka kuwa vita kamili ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya zaidi ya watu 115,000 na mamilioni kuachwa bila makazi.


SOURCE: MWANANCHI