Saturday, 5 October 2013

Mapokezi ya kishujaa

Tido Mhando 


Posted  Jumatatu,Septemba30  2013  saa 10:20 AM
Kwa ufupi
Kwenye makala zake hizi za kila Jumapili, anasimulia baadhi tu ya mambo hayo. Wiki jana alianza kuielezea safari yake ya kurejea nyumbani Tanzania kutoka Christchurch, New Zealand, alikokuwa ameenda kutangaza mashindano ya Michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola ya 1974, ambapo mwanariadha Mtanzania, Filbert Bayi, aliweka rekodi mpya ya dunia. SASA ENDELEA…


Kwa miaka mingi sana Tido Mhando alifanya kazi ya utangazaji, hususan wa redio. Kazi iliyokuwa chaguo lake tangu utotoni…Katika kipindi hicho kirefu, alishuhudia mengi mno ya kusisimua.
Kwenye makala zake hizi za kila Jumapili, anasimulia baadhi tu ya mambo hayo.

Wiki jana alianza kuielezea safari yake ya kurejea nyumbani Tanzania kutoka Christchurch, New Zealand, alikokuwa ameenda kutangaza mashindano ya Michezo ya Nchi za Jumuiya ya Madola ya 1974, ambapo mwanariadha Mtanzania, Filbert Bayi, aliweka rekodi mpya ya dunia. SASA ENDELEA…
Safari ya mkondo wa kwanza ya kutoka Christchurch hadi Melbourne, Australia, ilikuwa ya muda wa kama saa tatu hivi. Kikundi chote cha Watanzania, wote tukiwa kwenye sare zetu, kilikuwa cha watu wenye furaha kubwa mno. Nina hakika kila mmoja wetu alikuwa akiwaza kivyake kuhusu itakavyokuwa tutakapowasili kwetu nyumbani.
Tulikuwa tumepangiwa kulala hapo mjini Melbourne kwa muda wa saa chache hadi mapema siku ya pili, kwa hiyo safari ilikuwa bado ndefu. Hata hivyo, kwa upande wangu nilikuwa nikiwaza kuhusu mambo niliyokuwa nimeelezwa na maofisa wa Shirika la Ndege la Qantas juu ya fidia ya sanduku langu lililopotea.
Nikiwa ndani ya ndege hiyo kutokea Chrischurch nilikuwa nikiwaza: “Je, endapo hawa jamaa watanipiga chenga nitafanya nini?” Hii ilikuwa safari yangu ya kwanza ndefu ya kimataifa, kwa hiyo sikuwa na uzoefu wa mambo haya. Lakini nikaamua kupiga moyo konde na kujisemea kuwa ingebidi tu kuwaamini.
Naam, muda mchache baadaye, rubani wetu alitutangazia kujiweka tayari kwa kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Melbourne, mahali ambapo nilikuwa nimepangiwa kukamilisha hizo taratibu za fidia ya sanduku langu ama niseme kwa kweli, kijisanduku changu.
Lazima niwe mkweli maana hadi wakati huo bado mambo ya ujana-ujana ndiyo yaliyokuwa yamenitawala. Ingawaje nilikuwa mpenzi sana wa kuvaa mavazi ya vijana ya siku zile kama walivyokuwa wengine wa rika langu, sikuwa na nguo za kutisha hivyo.
Kwanza, nyingi ya nguo hizo zilikuwa za kushonesha, kuanzia suruali hadi mashati ya kubana. Nilikuwa na fundi cherahani wangu maalumu pale kwenye Mtaa wa Uhindini maeneo ya Mnazi Mmoja ambaye alikuwa ananishonea mavazi yoyote niliyohitaji. Alikuwa fundi maarufu wa vijana wa mjini, lakini alikuwa maalumu sana kwangu na baadhi ya marafiki zangu wa karibu hasa Robert Mwaimu.
Sasa kwa kweli kwenye kisanduku kile nadhani kulikuwa na suruali zisizozidi tano na kama mashati sita hivi, kwisha! Sasa kwa vile hawa jamaa wa shirika la ndege walikuwa tayari wameshanipatia fedha za kujikimu, niliona kama watakuwa wamenilipa zaidi ya kile ninachostahili, lakini ndiyo hivyo - huo ndiyo uliokuwa utaratibu na wajibu wao.
Nilikuwa miongoni mwa wasafiri wa mwisho-mwisho kushuka pale Melbourne na ghafla chini ya ndege hiyo nikamwona mtu aliyekuwa ameshika bango lenye jina langu. Nilimwendea na kujitambulisha ya kwamba mimi ndiye Dunstan Mhando (ambalo ndiyo jina langu rasmi).
Alikuwa jamaa mtanashati na mchangamfu sana ambaye, mbali na kunisalimia na kunitaka nifuatane naye, alikuwa mcheshi wa kutosha, kwani njiani alikuwa akinizungumzisha ingawaje kile Kiingereza chake cha Kiaustralia kilinisumbua kiasi.
Hata hivyo, yote kwa yote, alitaka kufahamu zaidi kuhusu safari yangu na hasa akapenda kufahamu mengi juu ya Filbert Bayi. Ndipo nilipotambua ya kwamba kumbe na yeye alikuwa tayari amezipata habari za ushindi wetu.

Hapana shaka, nilijisemea moyoni, huyu jamaa alikuwa amefuatilia taarifa za michezo ile iliyomalizika hapo jirani tu na kwao, yaani New Zealand na hasa kwa kuwa timu ya Australia ndiyo iliyokuwa imefanya vyema zaidi kwenye michezo mingi. Kwa hiyo, bila shaka raia wake walikuwa wamefurahia michezo hiyo.
Naam, punde kijana huyo alinielezea hayo kwamba raia wa Australia walikuwa kwa siku zote hizo za michezo wakifuatilia kwa karibu sana yale yote yaliyokuwa yakifanyika viwanjani na wamefurahia ushindi mkubwa na mnono walioupata.
Ndipo nikafahamu ya kwamba kwa kweli michezo ni nguzo kubwa ya mshikamano wa kitaifa. Nikawaza wingi wa medali walizozoa hawa jamaa wa Australia, ukilinganisha na medali zetu mbili. Lakini bado na sisi tulikuwa tukienda kifua mbele na hata wakati huo nilipokuwa na ndugu huyu wa Australia nilikuwa bado namtambia.
Mara tukaingia kwenye ofisi moja ndogo kiwanjani hapo. Ilikuwa ofisi nadhifu iliyokuwa na maofisa watatu tu, mmoja wao ambaye alionekana kama ndiye kiongozi humo, alikuwa ni mwanamama, mkubwa kidogo kiumri kuliko wale wengine wawili ikiwa ni pamoja na yule mwenyeji wangu.
Huyu ndiye aliyenikaribisha, pia akanipongeza sana kwa ushindi wa Filbert Bayi na zaidi, akaniambia kuwa kwa muda mrefu yeye na mumewe wamekuwa wakifikiria kwenda Tanzania kupanda Mlima Kilimanjaro.
Nilishtuka sana, kwani sikuwa nimefikiri kwamba kuna watu ambao wapo maili elfu nyingi namna hii ambao walikuwa wanawaza kuja Tanzania kupanda mlima ambao wengi miongoni mwetu wenyewe tulikuwa wala hatuujali kiasi hicho. Nilijisikia vibaya!
Kwa hakika, mama huyu alitaka kufahamu mengi zaidi kuhusu Tanzania na mlima wake wa Kilimanjaro, nami nilijitahidi kwa kiasi changu kumwelewesha na kumwelimisha zaidi na nikamwona kuridhika sana na kufurahia kukutana na mimi.
Hatimaye, akanitaka radhi kutokana na upoteaji wa ‘kasanduku kangu’. Akasema wamejitahidi kila walivyoweza kulitafuta lakini wameshindwa. Kwa hiyo, kwa kuzingatia taratibu na sheria za safari za ndege tulitakiwa ‘kumalizana’. Kwa hali hii wangenipatia kiasi cha Dola 430 kama fidia yao ya mwisho kwangu.
Tayari walikuwa wameandaa nyaraka zote husika kwa kukamilisha utaratibu huo, kwa hiyo kile ambacho mimi nilitakiwa kufanya kikawa ni kutia sahihi tu. Nilifanya hivyo harakaharaka, maana kwa kweli sikuwa nimetegemea hata kidogo kupata kiasi kama hicho cha malipo.
Baada ya kuweka sahihi kwenye karatasi husika, wakanipatia kiasi hicho cha fedha na kunitakia kila la heri huku bado wakiendelea kuniomba msamaha. Kwa kweli niliwaona kuwa watu wastaarabu na waungwana kwelikweli. Baadaye yule kijana alinichukua tena na kunipeleka mahali walikokuwa wenzangu.
Walikuwa tayari wamo kwenye basi la kutupeleka kwenye hoteli ambayo tungelala hadi mapema siku ya pili tutakapoanza safari ya kurejea nyumbani kwa kupitia tena Mauritius. Nilifurahi kwamba hoteli tuliyokuwa tumepangiwa ilikuwa katikati ya mji huo wa Melbourne maana baada ya kukamata kitita kile cha fedha sasa nilikuwa tayari kufanya ‘shopping’ ya nguvu ya nguo na vifaa vingine vya harusi. Nikajua kwamba kweli, Mungu ni mkubwa.
Kwa kuwa katika eneo lile la dunia, ule ulikuwa wakati wa msimu wa kiangazi basi maduka ya pale nayo yalikuwa yamejaa nguo nzuri mno hasa za wanawake zinazoendana na hali ya hewa ya jua la nyumbani Tanzania. Nikaamua kuyavamia kikweli kweli.

 linunua magauni kadhaa ya mvuto ambayo nilijua yangeweza kumpendeza mchumba wangu wakati wa harusi ambayo kwa wakati huo haikuwa mbali. Siku zilibaki chache sana. Zaidi nilihakikisha kwamba zilikuwa nguo za kupendeza za kipekee kabisa maana hata mchumba mwenyewe alikuwa mtu aliyejali sana mitindo.

Pamoja na nguo hizo, mimi pia nilijinunulia nguo kiasi. Halikadhalika nikanunua vitu vingine muhimu hasa kwa harusi ikiwa ni pamoja na viatu na makorokoro mengine ya kutishia tu. Kwa kweli mwisho wa yote nilikuwa nimeridhika mno na ununuzi huo.
Sasa kazi kubwa ikawa ni jinsi ya kuvifungasha. Kwa kuwa masanduku yetu yote yalikuwa yamehifadhiwa kwa pamoja, hatukuruhusiwa kuyachukua wakati tulipoteremka pale Melbourne. Kwa maana hiyo, tulikuwa pia haturuhusiwi kuingia na mizigo mingine mikubwa na mizito. Sasa mimi ikawa kama vile ndiyo naanza safari nikiwa nimefungasha kupindukia.
Nilichokifanya ilikuwa ni kuwakabidhi wachezaji mbalimbali baadhi ya vifurushi na wao wakawa wameridhia kabisa. Tulikuwa tukisafiri kama familia moja kubwa. Hasa kwa kuwa wote walikuwa wanafahamu ya kwamba mara tu nirejeapo nilikuwa nafunga pingu za maisha.
Tuliondoka Melbourne nikiwa mtu mwenye furaha kupindukia. Mambo yote yalikuwa yamekwenda vizuri kupita kiasi. Tulikuwa tunarejea nyumbani tukiwa washindi; nilikuwa nimefanikiwa kununua vitu vizuri na vya thamani kwa ajili ya harusi yangu na nilikuwa nimekamilisha kazi yangu vizuri mno. Ilikuwa ni fahari kubwa kwangu. Tuliwasili Mji Mkuu wa Mauritius, Port Luis, ikiwa nako ni wakati wa mchana kulingana na tofauti ya saa. Baada ya muda si mrefu tuliunganisha moja kwa moja na ndege ya Shirika la Ndege la Afrika Mashariki (EAA) kuelekea Dar es Salaam.
Mkondo huu ulikuwa umejaa shauku kubwa na nina uhakika siyo kwangu tu bali kwa sisi sote. Mimi nilikuwa nawaza na kuwazua jinsi tutavyopokewa tutakapowasili. Kuna nyakati ile hali ya hoihoi tuliyokuwa nayo ndani ya ndege ilikuwa inageuka ya utulivu mkubwa mno.
Naam, baada ya kama saa nne hivi, ikasikika sauti ya rubani ikisema tunakaribia kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Dar es Salaam kwa hiyo tujiandae kwa kufunga mikanda. Kiza kilikuwa kimeanza kuingia.
Niliketi kimya kwa muda hivi, nikifurahi kurejea salama nyumbani lakini nikiwa bado na mawazo mengi. Nilifahamu kwamba nikirejea kazini nitakuwa na kazi kubwa ya kujibu maswali mengi ya wenzangu na wasikilizaji wangu.
Wakati nikiwaza hivyo, nikaamua kuangalia dirishani na kwa mastaajabu makubwa, nikaona nje kulikuwa na halaiki kubwa ya watu waliofika uwanjani pale kutupokea. Nikafahamu kwamba Watanzania walikuwa wamefurahia ushujaa wetu na hasa wa bingwa wetu mpya wa dunia, Filbert Bayi. Machozi yakanilengalenga.
SOURCE: MWANACHI