Monday 21 October 2013

China kuleta watalii 30,000 nchini

21st October 2013
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
China imeahidi kuleta nchini Tanzania watalii 30,000 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwakani.

Ahadi hiyo ilitolewa jana na Mwenyekiti wa Wakala wa kutoa huduma za usafiri wa China na Hong Kong (CTS), Zhang Xuewu alipofanya mazungumzo na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda jijini Shenzen, China.

Alisema kampuni yake itawandaa mawakala wa usafirishaji watalii ili kuhakikisha kuwa watalii 10,000 wanapatikana kila mwaka ambao kiu yao ni kuja Tanzania.
“Wengi wanapenda kutembelea mbuga, lakini hapa nchini wamezoea kuona walio sakafuni, wakija watawaona wanyama live” (akimaanisha kuwa Wachina wamezoea kuona wanyama wa sanamu kwenye makumbusho yao jijini Shenzen).

Waziri Mkuu ambaye yuko katika siku ya tano ya ziara yake ya kikazi ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya China, alisema haelewi ni kwa nini kampuni hiyo imeweza kupeleka watalii Afrika Kusini na nchi jirani za Afrika Mashariki wakati haina urafiki nazo lakini imeshindwa kuwaleta Tanzania ambayo ina mahusiano mazuri na ya muda mrefu.

Akizungumza na Xuewu pamoja na baadhi ya viongozi kutoka Tanzania alioambatana nao, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema amepewa maelekezo rasmi na Rais Jakaya Kikwete ya kufuatilia suala la watalii wa kutoka China hasa ikizingatiwa kwamba mazungumzo ya jambo hili yalianza wakati wa Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa.

“Katika bara la Afrika hakuna nchi yenye vivutio lukuki kama Tanzania. Na tovuti ya www.safaribooking.com imeitangaza Tanzania kuwa nchi inayofaa kwa safari za mbugani kama mtu anataka kuona vivutio vizuri na vya asili.
Sasa ni kwa nini hatupati watalii wa kutosha na tunafanyaje ili kubadilisha hali hiyo?,” alihoji.

Alisema njia  mojawapo ni kuhakikisha kunakuwa na ndege ya moja moja kutoka miji ya China hadi Dar es Salaam jambo alisema litasadia kupuinguza kero kwa wasafiri ambao hivi sasa inabidi waunge safari mara mbili hadi tatu ili kufika Tanzania.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, (OWM) Uwezeshaji na Uwekezaji, Dk. Mary Nagu; Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda; Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe; Waziri wa Uvuvi na Mifugo wa Zanzibar, Abdallah Jihad Hassan na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mahadhi Juma Maalim.

Pia amefuatana na Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali mstaafu Abdulrahaman Shimbo, Wakuu wa mikoa ya Mtwara, Shinyanga na Simiyu; wabunge wawili, Godfrey Zambi (Mbozi) na Dk. Titus Kamani (Busega), Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji, Julieth Kairuki na viongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF), Salum Shamte na  Godfrey Simbeye.
CHANZO: NIPASHE