Friday, 4 October 2013

FIkRA YA HEKIMA : Tanzania imefilisika wanasiasa wakweli


Imeandikwa na Christopher Gamaina, Dar es Salaam   
Jumanne, Julai 30, 2013 12:37
Tanzania inaweza kuwa ndiyo nchi pekee katika Afrika na pengine duniani, yenye idadi kubwa ya viongozi wa kisiasa waongo na wanafiki kupindukia!
Viongozi wa sampuli hiyo wamefilisika dhana muhimu za ukweli na uzalendo. Wanafarakanisha watu ili kujipatia umaarufu na maslahi binafsi kinyume cha misingi ya umoja wa Watanzania.


Kwa bahati mbaya sana baadhi ya wananchi wanakubali ‘kuingizwa mjini’ na wanasiasa hao. Wanakubali kulishwa uongo na kutumika kuvunja sheria na kuvuruga amani.

Tena viongozi hao ni mahodari wa kuhamasisha uvunjifu wa sheria na amani, ingawa siku zote ndiyo wa kwanza ‘kulamba’ mbio na kuwatelekeza wapambe wao vyombo vya dola vinapowajibika kukabili uhalifu huo.

Kasumba hiyo inawadhihirisha moja kwa moja viongozi wa aina hiyo kwamba dhamira yao ni zaidi ya kutafuta uongozi wa kuwatumikia wananchi.

Kiongozi wa ukombozi wa Afrika Kusini kutoka katika udhalimu wa makaburu, Rais mstaafu Nelson Mandela, alipata kusema: “Kiongozi mzuri ni yule anayesimama nyuma wakati wa sherehe za ushindi, na ambaye anakuwa mstari wa mbele wakati wa matatizo na vita.”

Viongozi wengi wa kisiasa hapa Tanzania wanaamini kimakosa kuwa siasa ni kujengeana uadui, chuki, uhasama, kuzushiana kashfa, kupakana matope na hata kupigana. Wamesahau kuwa siasa ni mchezo wa kupingana kwa nguvu ya hoja na sera.

Wapo viongozi wachache wa kisiasa ambao ni wazalendo na mfano mzuri wa kuigwa katika nchi hii. Wanaheshimu na kutii sheria na taratibu za nchi. Hawa ni tumaini jema kwa mustakabali wa taifa letu na wanastahili kupewa ushirikiano wa dhati waweze kufanikisha malengo yao kwa manufaa ya wengi.

Lakini wengine wanaojipambanua kuwa katika harakati za kutafuta madaraka ya nchi hii, hawana hata chembe ya utii wa sheria bila shuruti. Swali moja linatosha kujiuliza: Hivi siku wakiingia Ikulu watamuduje kusimamia sheria za nchi ilhali wao siku zote wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha raia kuvunja sheria?

Dhana ya ukweli imekuwa ngumu kutawala katika mioyo ya viongozi wengi wa kisiasa Tanzania. Wengine wamefikia hatua ya kulazimisha rangi nyeupe iitwe nyeusi! Hawataki kuukubali ukweli wa mambo unaojidhihirisha wazi. Ni mahodari wa kutamka ahadi tele zisizotekelezeka!

Hatuwezi kusema uongo ndiyo nyenzo muhimu ya ushindani wa kisiasa. Kuendekeza uongo katika siasa ni ‘kubaka’ na kudhalilisha tasnia ya siasa. Hatuwezi kujenga Tanzania yenye wanasiasa na demokrasia ya kweli ikiwa tutaendelea kuwaunga mkono viongozi wa kisiasa, ambao kila kunapokucha kazi yao kubwa ni kupanda mbegu mbaya za chuki, unafiki na uongo katika jamii.

Kwa mfano, wiki iliyopita wengi wetu tumeshuhudia na kusikia jinsi viongozi wa vyama viwili vya siasa walivyogongana kuhusu tukio la mlipuko wa bomu katika mkutano wa kisiasa ulioitishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mjini Arusha.

Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na  Chadema wametuhumiana kusuka tukio hilo lililosababisha watu kadhaa kufariki na wengine kupata majeraha makubwa. Tunashindwa ni upande upi tuuamini, au tuendelee kuamini kwamba kila mwamba ngozi huvutia kwake.

Chadema ilikwenda mbali zaidi kwa kulituhumu Jeshi la Polisi kuhusika kuandaa mkasa huo huku ikisisitiza kuwa na ushahidi wa mkanda unaothibitisha kauli hiyo. Jeshi hilo nalo limekana tuhuma hizo huku likikishuku chama hicho kula njama za tukio hilo.

Kwa upande mwingine, tunaweza kuamini kuwa dhana ya uongo imepenya katika mjadala wa tukio hilo lenye sura ya kigaidi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba hakuna upande uliojitokeza kupeleka uthibitisho (vielelezo) katika vyombo vya ulinzi na usalama.

Inawezekana tuhuma zilizotolewa na viongozi wa vyama vya siasa zinalenga kutafuta umaarufu wa kisiasa tu na kuwahadaa Watanzania kuhusu tukio hilo. Ndiyo maana ninazidi kujiuliza: Wako wapi viongozi wa kisiasa wazalendo katika nchi hii?

Badala ya kuhamasisha amani, upendo na umoja wa Watanzania, baadhi ya viongozi wa kisiasa ndiyo chanzo cha uvunjifu wa amani na kuzorota kwa maendeleo hapa nchini.

Basi, itoshe tu kusema kwamba wanasiasa wengi katika nchi hii ni waongo, wanafiki; ni watu wanaoendekeza chuki binafsi na waliogeuza siasa kuwa chombo cha kujitafutia maslahi binafsi. Nchi imefilisika wanasiasa wakweli, hii ni hatari kubwa kwa maendeleo ya tasnia ya siasa hapa Tanzania.

SOURCE: JAMHURI MEDIA