Friday, 4 October 2013

Elimu zaidi kuhusu risiti za mashine itolewe kwa umma kuepusha vurugu


4th October 2013

Jiji la Mbeya juzi lilikumbwa na ghasia kubwa ambazo zilililazimisha Jeshi la Polisi kitumia nguvu kubwa kukabiliana nazo kwa kufyatua mabomu na risasi kwa lengo la kuwatawanya wamachinga waliokuwa wakifanya ghasia hizo.


Mbali ya mabomu, pia gari la kurusha maji ya kuwasha lilitumika katika mitaa ya Kabwe, Makungulu, Mfikemo hadi Ilolo huku wanawake na watoto wakikimbia ovyo mitaani.

Wakazi kadhaa wa Jiji hilo waliathiriwa na vurugu hizo kutokana na usafiri wa daladala kati ya Uyole kwenda mjini na Mbalizi kusimama kwa muda kutokana na vurugu hizo.

Vurugu hizo zilizoanza tangu asubuhi, zilidumu kwa zaidi ya saa sita na kusababisha vijana takribani 20 kutiwa nguvuni.

Polisi walichukua hatua ya kuingilia kati na kutumia nguvu baada ya wamachinga kuingia mitaani na kuhamasisha wafanyabiashara kufunga maduka na shughuli nyingine za biashara huku wakichoma matairi na kufunga barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam kwenda Zambia.

Hatua ya wamachinga inatokana na wafanyabishara wa jiji hilo kukataa kununua mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) kwa bei ya Sh. 800,000 kwa madai kuwa zinauzwa bei  ghali.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mbeya Jumatatu wiki hii, ilitoa muda hadi Novemba 15, mwaka huu kila mfanyabiashara awe amenunua mashine hizo ambazo zinasaidia ukusanyaji wa kodi ya serikali.

Uwezekano wa kutokea vurugu hizo ulianza kuonekana Jumatatu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro, kukutana na baadhi ya wafanyabiashara na viongozi wa TRA ofisini kwake kuzungumzia suala la mashine hizo pamoja na ukusanyaji wa kodi kwa ujumla.

Hatua ya Mkuu wa Mkoa kuzungumza na baadhi ya wafanyabishara hao, ndiyo iliyozua malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wengine ambao walidai kuwa aliokutana nao siyo walengwa, hivyo watakaomuomba azungumze nao  kwenye mkutano wa hadhara.

Sisi tunapinga hatua ya wamachinga ya kufanya vurugu bila sababu za msingi kwa kuwa tayari serikali ilishaonyesha nia ya kukutana na wafanyabiashara kupata mwafaka wa mashine hizo.
Lakini pia haieleweki sababu za wamachinga kufanya vurugu wakati walalamikaji walikuwa ni wafanyabiashara.

Hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kuwa wafanyabiashara huenda wanawatumia wamachinga wafanye vurugu ili serikali isitishe zoezi la kuwabana wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki ikiwa ni njia nzuri ya kusimamia mapato.

Vurugu hizo kama zingefanywa na wafanyabiashara, tungeelewa kuwa walisukumwa na kero wanayodai kuwa ni ghali kwao, lakini kwa kufanywa na wamachinga tunadhani kuna jambo lililojificha.

Tunaambiwa kuwa wafanyabiashara hao waliiomba Serikali kutoa bure mashine hizo kwa kuwa ni ghali ukilinganisha na kipato chao, ingawa tunadhani kuwa hoja zao hazina nguvu kwa kuwa kila mfanyabiashara kipato chake kinajulikana.

Kwa maneno mengine, TRA ina kumbukumbu za wafanyabiashara wote na ndiyo maana wote ambao mauzo yao yanafikia hadi Sh. 40,000 kwa siku, wanatakiwa kununua mashine hizo.

Kama kuna mfanyabiashara ambaye ataona hastahili kuwa na mashine hizo, basi aandike barua ili mamlaka ipitie katika maduka yao kukagua kujiridhisha kama malalamiko yake ni sahihi.

Sisi tunadhani kwamba mashine hizo zinapingwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wakifanya udanganyifu wa kukwepa kodi na siyo vinginevyo.

Tunashauri kwamba kuna haja kwa TRA kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusiana na mashine za kutolea risiti kwamba pamoja na kuwa zinasaidia kuepusha vitendo vya ukwepaji kodi, lakini pia zinawasaidia wafanyabiashara wenyewe kuweka vizuri kumbukumbu za mapato yao.

Itakuwa vizuri wafanyabiashara wote wakabanwa ili waanze kuzitumia mashine hizo na hapo elimu kwa umma kwa maana  wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla, wakaendelea kuelimishwa kuhusiana na umuhimu wa mashine hizo.

Hali hiyo itawapa uelewa wananchi wa kutambua kwamba wanawajibika kudai risiti hizo kwa wafanyabiashara.

Tunaiunga mkono TRA kwa hatua zake za kubuni utaratibu huu ambao unawabana wakwepa kodi. Tunaamini kuwa utasaidia serikali kuongeza ukusanyaji wa mapato yake na kuboresha huduma za jamii.
CHANZO: NIPASHE