Sunday, 20 October 2013

‘Mateja’ wapeana ulevi wa dawa za kulevya kwa njia ya damu(2)

Kuhusu uwezekano wa mtu mmoja aliyetumia dawa za kulevya kutolewa damu yake kidogo na kutumiwa na watu wengine wawili na kulewa kwa kiwango kilekile, utatolewa ufafanuzi wa kisayansi toleo lijalo. Picha na Maktaba 
Na Harrieth Makwetta, Mwananchi

Posted  Jumapili,Oktoba20  2013  saa 1:1 AM
Kwa ufupi
Akifafanua kuhusu dawa inayotumika kuondoa sumu ya dawa za kulevya katika mwili wa mwathirika, Dk Masau alisema methadone humwezesha mgonjwa kutosikia hamu ya kutumia dawa hizo, sambamba na kumwondolea maumivu mwilini.


Wiki iliyopita habari hii ilieleza mateja walivyobuni njia ya kupeana ulevi kwa njia hatari ya kubadilishana damu yenye dawa za kulevya. Endelea...
“Kitengo chetu kilianza kutoa huduma hii Februari 2011 na tulianza kupokea wagonjwa wanne kwa siku na ilifikia hatua tulikuwa tukipokea hata 20 waliohitaji huduma kutoka kwetu na mpaka sasa tuna wagonjwa 640. Kati ya hawa 18 tuliwaondoa kutokana na matatizo mbalimbali. Wapo waliokuwa wakifika na silaha mbalimbali na hawa walikuwa tishio kwa kitengo hiki.”
Dk Masao anasema licha ya kuondolewa katika kitengo hicho walio wengi wamekuwa wakirudishwa tena; “Hata kama akifanya vurugu tutamwondoa lakini baadaye lazima tumfuate na kama akikiri kosa na kuahidi kubadilika tunamrudisha na anaendelea na dozi. Kila anayetibiwa hapa sharti la kwanza ni lazima makazi yake halisi yajulikane hivyo inakuwa rahisi kumfuatilia mgonjwa huyu iwapo atakatisha dozi ili kujua sababu ni nini.”
Akifafanua kuhusu dawa inayotumika kuondoa sumu ya dawa za kulevya katika mwili wa mwathirika, Dk Masau alisema methadone humwezesha mgonjwa kutosikia hamu ya kutumia dawa hizo, sambamba na kumwondolea maumivu mwilini.
“Dawa hii wanayopewa inawasaidia mwili kutokuwa na maumivu. Maana mtu anaposikia maumivu hapo ndipo anapoanza kuhangaika kutafuta heroin ili ajidunge. Lakini akipata methadone huwa salama na hawezi kupata tena hamu ila masharti ya dawa hii ukitumia hupaswi kurudi tena na kuanza kujidunga,” alisema Dk Masau na kuongeza; “Dawa hii yenye thamani ya dola 75,000 sawa na Sh124 milioni tumepewa na wafadhili kutoka Canada ambapo walitoa kiasi cha kilogramu 50 ambazo huweza kutumika kwa kipindi cha miaka miwili.”
Anafafanua kuwa dozi hiyo hutolewa kila siku katika hospitali hiyo kwa kiasi cha dozi ya mililita 1.5 kwa kila mwathirika kila siku huku wengine wakitunzwa wodini kutokana na kuathirika kwa kiwango kikubwa, hata hivyo aliweka wazi kuwa idadi kubwa wamekuwa wakishindwa kuhimili gharama za usafiri kila siku.
Alisema Tanzania ni nchi ya kwanza katika nchi za Jangwa la Sahara kuwa na kitengo cha methadone. “Tanzania ni nchi ya kwanza katika nchi za Jangwa la Sahara kuanza kutoa matibabu ya methadone, lakini pia tunafundisha nchi nyingi kutoa huduma hii wakiwemo Nigeria, Msumbiji, Kenya, Uganda, Zambia na nchi nyinginezo ambao hufika hapa Muhimbili kwa ajili ya kupata utaalamu huu,” alisema Dk Masao.
Alisema utaalamu hasa kuhusu matumizi ya dawa hiyo sambamba na ujuzi wa kutoa matibabu hayo waliupata katika nchi ya Vietnam.
“Vietnam ndipo hasa tulipopata ujuzi huu na huko tumekuwa tukiwapeleka wataalamu wengi kujifunza.
Moja kati ya changamoto zilizopo katika kitengo hiki ni ukosefu wa watoa huduma, wengi hawapo radhi kujitolea katika kutoa matibabu kwenye kitengo hiki. Hatuna wanasaikolojia wa kutosha, manesi na madaktari”
Dk Masao anasema kitengo hicho kimekuwa kikipokea pia wanandoa ambao wamekuwa wakifika kwa pamoja kwa nia ya kupata huduma hiyo ili waachane na matumizi ya dawa za kulevya.
Kuhusu uwezekano wa mtu mmoja aliyetumia dawa za kulevya kutolewa damu yake kidogo na kutumiwa na watu wengine wawili na kulewa kwa kiwango kilekile, utatolewa ufafanuzi wa kisayansi toleo lijalo.

Aliitaja mikoa inayoongoza kwa waathirika wa dawa za kulevya kuwa ni Mbeya, Dodoma, Arusha , Tanga na Morogoro.

SOURCE: MWANANCHI