Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Posted Jumapili,Oktoba20 2013 saa 1:0 AM
Posted Jumapili,Oktoba20 2013 saa 1:0 AM
Kwa ufupi
Kazi hiyo ya uchunguzi inaanza leo hadi Novemba 5,
mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine watafanya ziara ya uchunguzi
kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya.
Dar es Salaam. Wakati ikisubiriwa ripoti ya
uchunguzi wa Tume Maalumu iliyoundwa kwa Azimio la Bunge kuchunguza
kashfa ya vigogo walioficha Sh323.4 bilioni katika benki nchini Uswisi,
Shirika la Kimataifa la Mtandao wa Ulaya wa Madeni na Maendeleo
(Eurodad), leo linaanza kuwachunguza walioficha mabilioni hayo ya fedha
nchini humo.
Kazi hiyo ya uchunguzi inaanza leo hadi Novemba 5,
mwaka huu, ambapo pamoja na mambo mengine watafanya ziara ya uchunguzi
kuhusu masuala ya uwazi katika kodi katika nchi za Ulaya.
Uchunguzi huo utafanywa na jopo la wataalamu
waliobobea katika masuala ya kodi na maendeleo na wataongozwa na
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe ambaye pia
ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Sakata la kashfa hiyo liliibuliwa bungeni kwa hoja
binafsi ya Zitto, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini, mwishoni
mwa mwaka 2012.
Zitto alisema kwamba kiasi cha fedha kilichofichwa nchini Uswisi ni kikubwa zaidi ya hicho kilichotajwa.
Kufuatia hoja hiyo, Bunge chini ya Spika Anne
Makinda liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja ambacho kinaishia
Oktoba mwaka huu, iwe imekamilisha uchunguzi na kuwasilisha ripoti hiyo
bungeni.
Ripoti ya Tume hiyo iliyoundwa na Serikali kwa
Azimio la Bunge ilitolewa mwishoni mwa mwaka jana, ikiongozwa na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, mpaka sasa
tayari imewahoji vigogo 200 wakiwamo wabunge, wanasiasa na
wafanyabiashara.
Muda wa tume hiyo kufanya uchunguzi unakamilika
mwezi huu na inatarajiwa katika mkutano ujao wa Bunge unaoanza Oktoba 29
mjini Dodoma, itawasilisha ripoti hiyo.
Taarifa zilizolifikia Mwananchi Jumapili na
kuthibitishwa na Zitto jana jioni zilieleza kuwa Eurodad ambao ni
mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali 48 kutoka nchi 19 za Ulaya,
yanayojihusisha na masuala ya kufuatilia madeni ya nchi zinazoendelea,
kwa muda sasa umekuwa ukipambana na watu wanaokwepa kulipa kodi.
“Mashirika haya yamekuwa kwenye kampeni ya kupinga
utoroshwaji wa fedha kupitia ukwepaji kodi unaofanywa na mashirika ya
kimataifa kwa nchi zinazoendelea,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa kesho Zitto atakutana
na Waziri wa Fedha wa Uswisi na maofisa wa benki mbalimbali na asasi za
kiserikali zilizopo katika mji mkuu wa nchi hiyo, Geneva.
“Zitto pia atahudhuria mkutano wa Kamati ya Kodi
ya Umoja wa Mataifa katika kampeni ya kubadili mfumo wa kodi za
kimataifa ili kuzuia unyonywaji wa nchi za Kiafrika unaofanywa na
kampuni kubwa za kimataifa,” inaeleza taarifa hiyo.
Juzi 21 mwaka huu, Werema alizungumza na Mwananchi Jumapili na
kuthibitisha kuhojiwa kwa vigogo hao 200, lakini akasita kuwataja kwa
majina kwa maelezo kuwa asingeweza kuwataja kwa kuwa uchunguzi bado
ulikuwa unaendelea.
“Uchunguzi huo unaendelea,” alisema Werema huku
akisita kueleza kwa undani juu ya kazi hiyo kwa kile alichosema kuwa
hana sababu ya kufanya hivyo kwa sasa.
“Subiri uchunguzi bado unafanywa,” alisema Werema na alipotakiwa kueleza utamalizika lini alisema: “Utamalizika tu.”
Uchunguzi wa walioficha mabilioni ya Uswisi
uliibuka baada ya Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) kutoa taarifa Juni,
2012 kuhusu raia wa kigeni wanaomiliki akaunti za benki nchini humo.
Orodha hiyo iliorodhesha pia baadhi ya Watanzania
wenye akaunti zenye fedha zinazofikia Dola196 milioni ambazo ni sawa na
Sh323.4 bilioni.
Jarida la kimataifa la uchunguzi la ‘The Indian
Ocean Newsletter’ toleo la hivi karibuni, lilimnukuu Werema akisema
uchunguzi huo kwa sasa unatia matumaini.
Mbali na Werema, tume hiyo inaundwa na viongozi
kadhaa wa taasisi nyeti kama vile Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hosea, Mkurugenzi wa Usalama
wa Taifa, Rashid Othman na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno
Ndulu.
Tume hiyo inawahusisha pia Mkuu wa Sheria wa BoT,
Mustapha Ismail na maofisa kutoka idara ya upelelezi na Ofisi ya
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.
Kwa mujibu wa jarida hilo la kimataifa, miongoni
mwa watuhumiwa hao ni wanasiasa na majenerali wastaafu wanaotuhumiwa
kutorosha zaidi ya Dola133 milioni mwaka 2005, kupitia Mfuko wa Ulipaji
Madeni ya Nje (EPA)
Baadhi ya watu wanaodaiwa kuhusika wamehojiwa
kutokana na taaluma zao, familia zao, akaunti zao za benki zilizoko
nchini na nje ya nchi pamoja na nchi walizotembelea mara kwa mara kwa
miaka mitatu iliyopita.
Lengo la kuwahoji inaelezwa ni kutaka kujua iwapo
walifuata njia zinazotakiwa katika kufungua akaunti hizo nje ya nchi na
iwapo fedha zilizohifadhiwa huko zilipatikana kihalali.
Akiwa mkoani Tabora wiki moja iliyopita katika
mikutano ya kuimarisha chama, Zitto alisema tayari amemwandikia barua
Katibu wa Bunge kutaka taarifa ya uchunguzi huo itolewe katika mkutano
ujao.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI