Wednesday 23 October 2013

Mwanafunzi Edson Kunambi; Ishara ya mafanikio ya elimu jumuishi Tanzania

Edson Kunambi akiwa na mama yake Onoratha Kunambi. Picha na Mpiga Picha wetu 
Na Julieth Ngarabali, Mwananchi

Posted  Jumanne,Oktoba22  2013  saa 12:41 PM
Kwa ufupi
Mazingira ya elimu yakiboreshwa na kuwa rafiki kwa walemavu, katu ulemavu hauwezi kuwa kikwazo kwa watu wenye ulemavu kushindwa kusoma.


Mkakati wa kitaifa wa utekelezaji wa Mpango wa Elimu Jumuishi, utaleta manufaa na mabadiliko chanya ya kielimu kwa watoto wenye ulemavu, ikiwa utatekelezwa kama ulivyopangwa kuanzia uboreshaji wa miundombinu, vifaa, watumishi wa elimu na walimu.
Pia mkakati huo usipochakachuliwa, utaleta uaminifu zaidi kwa familia nyingi zenye watoto wenye ulemavu, hivyo kuwasukuma kuwapeleka watoto wao shuleni, kwani wataamini katika ubora wa malezi ya walimu kwa watoto hao.
Mbali na ubora wa malezi ya walimu, imani ya wazazi katika kuwapeleka watoto walemavu shuleni, itaongezeka kama shuleni kuna vifaa vya kutosha na miundombinu iliyoandaliwa kwa ajili ya kundi hilo la wanafunzi.
Kisa cha Edson Kunambi
Mazingira ya elimu yakiboreshwa na kuwa rafiki kwa walemavu, katu ulemavu hauwezi kuwa kikwazo kwa watu wenye ulemavu kushindwa kusoma. Hili limejidhihirisha kupitia kwa mtoto mwenye ulemavu wa kutokusikia na kusema, Edson Kunambi (13), mkazi wa Kibaha ambaye katika makala haya anaonyesha furaha na mafanikio anayoyapata baada ya kuchanganywa katika darasa moja na watoto wengine wasio na ulemavu
Akizungumza na gazeti hili kwa lugha ya alama, huku akitafsiriwa na mwalimu wake Idd Besha, Kunambi anayesoma darasa la tano, anasema anapenda kusoma katika shule jumuishi kwa sababu watoto wengi wako makini kujisomea, tofauti na ilivyo katika shule maalumu za watu wenye ulemavu.
Tofauti na shule aliyokuwepo awali, anasema katika darasa ya elimu jumuishi kila mtoto anajishughulisha kujifunza iwe kwa kusoma, kuchora au kufanya hesabu.
Akiwa na umri wa miaka minne, anasema alipelekwa kusoma elimu ya awali katika shule ya watoto wenye ulemavu wa uziwi Buguruni Dar es Salaam, ambako alisoma hadi darasa la tatu. Badaye akahamishiwa katika shule jumuishi anayosoma sasa ampapo mwaka huu yuko darasa la tano.
Akishirikiana vyema na wanafunzi wenzake, Kunambi amekuwa moto wa kuotea mbali darasani kwa kuwa na matokeo mazuri kushindwa wanafunzi wengi wasio na ulemavu. Kwa mfano, anasema mwaka 2012 alishika nafasi ya pili darasani.
“Mwaka huu 2013 sikufurahi sana maana nimekuwa wa 17 darasani,’’ anasema.
Mama yake mzazi, Onoratha Kunambi anasema mtoto wake huyo ni mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto watatu, lakini ni yeye tu mwenye ulemavu wa kutokusikia na kuzungumza.
Anaeleza kuwa Edson alizaliwa miaka 13 iliyopita kwa njia ya kawaida. Alipofikisha miezi minane na wiki mbili alianza kusumbuliwa sana na mafua. Baadaye hata alipokuwa akilia hakutoa sauti, huku mdomo ukimjaa mate mengi.

SOURCE: MWANANCHI