Thursday 3 October 2013

Ozil nyota wa Arsenal

Ozil alinunuliwa kutoka klabu ya Madrid
Arsenal imeendelea kunawiri katika michuano ya kombe la klabu bingwa ya Ulaya baada ya ushindi wake dhidi ya Napoli ya Italy katika uwanja wa Emirates.
Nyota wa pambano hilo Mesut Ozil alifunga bao lake la kwanza kwa Arsenal na kisha kuchangia bao la pili liliofungwa na Olivier Giroud na kuamua hatima ya mechi hiyo katika dakika 15 za kwanza.
Arsenal walidhibiti mchezo huo wakionyesha ujasiri uliowawezesha kuongoza Ligi ya Premier. Ozil ambae alisainiwa kutoka Real Madrid ndie aliyekua kichocheo kikubwa cha Arsenal ambayo sasa inaongoza kundi la F.
Katika mechi nyingine ya kundi hilo Borussia Dortmund ya Ujerumani iliilaza Marseille ya Ufaransa kwa mabao 3-0.
Aaron Ramsey nae pia alisifiwa kwa mchezo wake kwa kuchangia katika bao la Ozil na wachezaji hao wawili walionekana kuonana vizuri katika safu ya viungo vya Arsenal.
Katika michuano mingine Barcelona ya Hispania ikimkosa mchawi wao Lionel Messi ilitolewa kijasho na Celtic ya Scotland kabla kuibuka mshindi wa 1-0 bao liliofungwa Cesc Fabregas. Celtic walighadhabishwa na uamuzi wa kumuonyesha kadi nyekundu nahodha wao Scott Brown kwa kumfanyia madhambi Neymar.
Chelsea iliwapa afuweni mashabiki wake kwa kuicharaza Steaua Bucharest ya Rumania kwa mabao 4-0.
Athletico Madrid ya Hispania iliilaza Porto ya Ureno 2-0 na Mario Balotelli aliiokoa AC Milan ya Italy kwa bao la penalti katika kipindi cha majeruhi na kutoka sare 1-1 na Ajax ya Uholanz.

CHANZO: BBC SWAHILI