Tuesday 1 October 2013

PPRA yatishia ‘kutilia mchanga’ vitumbua vya vigogo serikalini


Na Leon Bahati

Posted  Jumanne,Oktoba1  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
 “Hilo tumeliona na ndio maaana safari hii tumekuwa makini zaidi. Wale maofisa watakaoshindwa kutoa sababu za msingi tutapendekeza kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua.”

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imetoa matokeo ya ukaguzi ya mwaka 2012/13 huku ikizitaka taasisi 12 za Serikali kujieleza kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma.
 Katika taasisi hizo, zipo ofisi mbili za wakuu wa mikoa pamoja, wizara moja, halmashauri tano, malaka nne za maji na wizara moja.
 Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA, Jaji Thomas Mihayo amesema viongozi wanaosimamia fedha katika taasisi hizo watajadiliana na PPRA kujua hatua mwafaka za kuchukuliwa.
 “Maofisa masuuli, wenyeviti wa bodi za zabuni na wakuu wa vitengo vya ununuzi wataitwa na Bodi ya Wakurugenzi ya PPRA kutoa sababu za kufanya vibaya kwenye ununuzi,” alisema Jaji Muhaoyo.
Aliongeza: “Tutajadiliana  hatua zitakazoweza kuchukuliwa katika kupata ufumbuzi wa mapungufu (upungufu) hayo.”
Taasisi hizo zikishindwa kutoa maelezo, alisema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
 Amezitaja ofisi za wakuu wa mikoa zilizopewa onyo kuwa ni Mtwara na Lindi na kwa upande wa wizara ni Sayansi na Teknolojia.Taasisi nyingine ni Halmashauri za Wilaya ya Korogwe, Wilaya ya Chamwino, Manispaa ya Singida, Wilaya ya Kigoma na Wilaya ya Kilwa
Mamalaka za maji ni Dawasco Dar es Salaam,  Uwasa Bukoba, Uwasa Moshi na Mtwaa. Katika kundi hilo pia lipo Shirika la Masoko Kariakoo.
 Alipoulizwa iwapo haoni kuwa tatizo la matumizi mabaya ya fedha za umma limekuwa ni jambo la kawaida kutokana na PPRA kutokuwa na nguvu za kisheria za kuwachukulia hatua moja kwa moja wahusika, alisema:
 “Hilo tumeliona na ndio maaana safari hii tumekuwa makini zaidi. Wale maofisa watakaoshindwa kutoa sababu za msingi tutapendekeza kwa mamlaka husika kuwachukulia hatua.”
 Katika ukaguzi wao, jaji Mihayo alisema walikagua mikataba 5,867 ya ununuzi yenye thamani ya Sh2 trilioni.
 Miongoni mwa udhaifu uliojitiokeza anassema ni kuwepo kwa viashiria vya rushwa, na myaraka za zabuni kutotayarishwa katika kiwango cha kuridhisha.

 Udhaifu mwingine aliutaja ni michoro kutoambatanishwa kwenye nyaraka za zabuni na mikataba jambo ambalo lilichangia kazi kutotekelezwa kwa ufanisi.
 Kaimu Mkurugenzi wa PPRA, Laurent Shirima alisema mamlaka hiyo ina nguvu kisheria za kukagua manunuzi ya idara na taasisi za Serikali pamoja na kupendekeza kwa serikali hatua zinazopaswa kuchukuliwa.

SOURCE: MWANANCHI