25th October 2013
Hayo yalibainishwa jana jijini Dar es Salaam wakati Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), kampuni binafsi na washiriki mbalimbali walipokuwa wakitoa mada na hoja zao kwenye mkutano wa gesi na mafuta.
Mwenyekiti wa TPSF, Dk. Reginald Mengi, alihoji kuwa, serikali itawezaje kutoa vitalu vya gesi na mafuta, bila kuwa na sera.
“Kama serikali haina sera ya kutoa vitalu, je, unauzaje rasilimali za taifa bila ya kuwa na sera? Tusionekane tunauza rasilimali za taifa bila kuwapo kwa sera,” alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi, alisema: “Tanzania ni tajiri, gesi tuliyonayo ndiyo mtaji wenyewe, lakini kusema fedha hazipo, hivyo tuite wageni waje kuwekeza, haiwezekani.
Mtaji si kile tulicho nacho kwenye mifuko yetu, bali kama wenye akili tunajua ulipo. Fedha zipo kwenye masoko ya fedha.”
Mkurugenzi wa kampuni ya Mansoor Industries Ltd, Alkarim Hirani, alisema mkutano huo umetoa nafasi kwa Watanzania kujua kile kilichokuwa kinaendelea na pia umewafungua na kuhoji kwanini serikali ina uharaka wa ugawaji na ununuzi wa vitalu hivyo.
Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini, Eliakimu Maswi, alisema sera ya usimamizi wa mafuta na gesi ilishakamilika na kupitishwa Oktoba mwaka huu isipokuwa rasimu ya sera inayolenga kuwashirikisha Watanzania namna ya kunufaika na rasilimali hizo, inatarajiwa kuwekwa hadharani Desemba mwaka huu.
CHANZO:
NIPASHE