Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Posted Alhamisi,Oktoba24 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Oktoba24 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Mwanasheria mwingine, Berious Nyasebwa alivipongeza vyama hivyo na kusisitiza kuwa uamuzi uliochukuliwa umejaa busara na hekima.
Dar es Salaam. Baadhi ya wasomi jijini Dar es
Salaam, wamevipongeza vyama vya siasa kwa kitendo cha kukubaliana kuhusu
maboresho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na kuifanya Serikali
kuandaa hati ya dharura.
Wasomi hao wamesema vyama hivyo vimeonyesha kubadilika kifikra.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti
jana, wasomi hao walisema ili nchi iweze kupata Katiba Mpya yenye
masilahi kwa nchi husika, lazima wananchi na vyama vya siasa wakubaliane
na kuwa kitu kimoja, jambo ambalo limedhihirika juzi.
Mwanasheria maarufu, Profesa Chris Peter Maina
alisema, “Vyama vimetoa hoja nzito kuhusu kasoro zilizomo katika sheria
husika, pamoja na kuamua kuweka kando tofauti zao na kuungana, binafsi
nimependa zaidi hoja zao za msingi zilizolenga masilahi ya taifa kuliko
vyama vyao.”
Profesa huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kituo cha
Huduma za Sheria Zanzibar, alisema hata wabunge wa vyama hivyo
wanapaswa kuwa kitu kimoja katika kupitisha mabadiliko hayo.
Mwanasheria mwingine, Berious Nyasebwa alivipongeza vyama hivyo na kusisitiza kuwa uamuzi uliochukuliwa umejaa busara na hekima.
“Hoja hii ya Serikali sidhani kama itapingwa na
wabunge ikifika bungeni, wanasiasa wameamua kukubaliana na wametambua
wazi kuwa tendo la kuandika Katiba Mpya ni la maridhiano si la mtu
binafsi wala chama fulani” alisema Nyasebwa.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam,
Profesa Gaudence Mpangala alisema, “Binafsi nimepata matumaini mapya juu
ya mchakato huu baada ya vyama kuamua kuweka kando tofauti zao.
Kilichofanyika ni mageuzi ya kifikra.”
Hata hivyo Profesa huyo alisema kulikuwa na
ulazima kwa tume hiyo iliyokuwa imalize kazi yake Novemba 1 kuomba
kuongezewa muda, kwa maelezo kuwa bado ilihitaji kufanya uchambuzi wa
maoni mbalimbali, ili kukamilisha rasimu ya pili ya Katiba.
“Sidhani kama muda ulioongezwa utaathiri mchakato mzima wa Katiba.”
SOURCE; MWANANCHI
SOURCE; MWANANCHI