Friday 4 October 2013

Sote tu wazee watarajiwa,tupange maisha ya uzeeni leo

2nd October 2013
Jana dunia iliadhimisha siku ya wazee ambayo ilipambwa kwa kauli mbiu tuondoe vikwazo vyote vinavyowanyima wazee maisha ya utu na kuwashirikisha katika shughuli zote za kijamii.


Wito huu unalenga kuhakikisha maisha bora kwa wazee kwa maana ya kuzifikia huduma za afya, chakula, malazi na mavazi, lakini pia wakipewa fursa ya kutoa mawazo yao katika mfumo mzima wa maisha ya jamii.

Tanzania kama taifa liliungana na mataifa mengine pia kuikumbuka siku hii. Wazee ni sehemu muhimu ya jamii ya Watanzania. Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi iliyofanyika Agosti mwaka jana, wazee kuanzia miaka 60 kuendelea wanaelezwa kuwa ni asilimia 5.6 sawa na watu milioni 2.5 ya Watanzania wote milioni 44.9.

Kundi hili linaelezwa kuwa dogo sana katika baadhi ya mikoa, Kilimanjaro unaelezwa kuwa unaongoza kwa kuwa na wazee zaidi ambao ni asilimia 9.7 ya wakazi wa mkoa huo, ukifuatiwa na Mtwara wenye wazee asilimia 9.5, Lindi asilimia 9.0 na Tanga asilimia 8.5.

Mikoa yenye idadi ndogo zaidi ya wazee ni Dar es Salaam yenye asilimia 3.5 ya wakazi wake wote, Mjini Magharibi asilimia 3.6, Geita asilimia 3.7 na Rukwa asilimia 3.9.

Mchanganuo huo unathibitisha pia kuwa idadi ya vijana ni kubwa kwenye wazee wachache na vijana wachache kwenye wazee wengi. Hali hii inatoa changamoto kubwa ya kijamii.

Takwimu za idadi ya watu nchini zinaonyesha kuwa ingawa kundi la wazee zaidi ya miaka 60 ni ndogo sana likilinganishwa na wengine chini ya umri huo, kuna haueni kwamba wazee wanaweza kuhudumiwa vizuri zaidi kwa sababu ya idadi yao.

Hata hivyo, ni vema wakati siku hii ya wazee duniani ikikumbukwa jamii ikaelewa kwamba kama taifa hifadhi ya jamii ipo hasa mikononi mwa jamii kwa maana ya kila familia kuwatazama na kutunza wazee wake. Pale familia zinapoyumba hata maisha ya wazee hawa nayo yanakuwa shakani kama ambavyo imeshuhudiwa mara nyingi.

Matukio ya kuuawa kwa wazee katika baadhi ya mikoa nchini yakitazamwa kwa undani wake yana uhusiano wa karibu sana na suala zima la changamoto za kiuchumi ndani ya jamii.

Wengi wanaouawa kwa tuhuma kwamba ni wachawi ni wanawake wazee ambao aghalabu hawana waume, ni wajane, lakini wapo wanaoangalia kwa jicho la husuda mali kidogo wanayomiliki.

Kwa maneno mengine, kundi hili la raia ndani ya jamii maisha yao yanakuwa hatarini wakati wote kwa sababu tu ya changamoto za kiuchumi na kukosekana kwa mifumo dhabiti za kuhakikisha usalama wao na mali wanayomiliki. Habari hizi zimeelezwa mara nyingi sana na viongozi, kutangazwa sana na vyombo vya habari lakini bado ni changamoto inayopaswa kutazamwa vilivyo wakati kama huu siku ya wazee inapoadhimishwa ndani ya jamii.

Serikali kwa muda sasa imekuwa na sera ambazo zinajielekeza kutazama kundi la wazee kwa maana ya kuwahakikishia maisha bora na salama. Mikakati hii ni pamoja na ukweli kwamba sheria za hifadhi ya jamii zimebuniwa ili kila anayefanya kazi sasa ajiandae kwa maisha yake ya uzeeni.

Hapa ndipo dhana nzima ya mifuko ya hifadhi ya jamii inapofanya kazi. Lakini kama tujuavyo, bado mifuko hii inachukua idadi ndogo sana ya mahitaji ya wananchi wote katika umri wao wa uzee. Takwimu zinaonyesha kuwa mifuko yote ya hifadhi ya jamii nchini haifikishi wanachama milioni mbili.

Kwa miaka kadhaa sasa serikali imekuwa inahamasisha sera ya huduma za tiba bure kwa wazee wote wenye umri wa miaka 60 na kuendelea. Katika baadhi ya hospitali na vituo vya afya vya umma dirisha kwa ajili ya wazee hawa limefunguliwa nia ikiwa ni kuwawezesha kufikia huduma hizi kirahisi.

Pamoja na nia njema ya serikali, huduma hii kama zilivyo huduma nyingine za kijamii inakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha. Wazee hawa hata wakifanikiwa kufika hospitalini hakuna dawa, baadhi ya vipimo vikubwa kama CT Scan, RMI na hata X-Ray tu hazipatikani katika hospitali nyingi za umma. Vituo vya afya hali ni mbaya zaidi.

Tunafikiri wakati tukiungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha siku ya wazee, ni wakati pia wa kukaa na kutafakari kwamba ni kwa kiwango gani tunaweza kuandaa maisha ya wazee yenye staha, heshima na utu, kwa kuwa kila kijana mwenye nguvu leo anayefanya kazi na kufurahia nguvu hizo ni mzee mtarajiwa. Uzee ni hatima yetu sote tujenge mazingira bora ya maisha bora ya kundi hilo katika jamii.
 
CHANZO: NIPASHE