Na Mwinyi Sadallah , Mwananchi
Posted Alhamisi,Oktoba24 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Oktoba24 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni katika matumizi mabaya ya fedha za umma kwa msimu wa Mwaka wa Fedha wa 2011/12.
Zanzibar. Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais
Zanzibar, imekumbwa na kashfa ya kutuhumiwa kuwapo kwa matumizi mabaya
ya fedha za umma kutokana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa
Hesabu za Serikali ya mwaka 2011/12 visiwani hapa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya ukaguzi wa hesabu kwa
wizara, mashirika na taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, jumla
ya Sh295,977,000 zimelipwa kwa matumizi mbalimbali ya huduma kwa Makamu
wa Kwanza wa Rais na mambo mengine bila ya kuwapo na vielelezo vya
matumizi hayo.
Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Fatma Mohamed
Said katika taarifa yake imesema, kukosekana kwa nyaraka za vielelezo
vya matumizi ni kwenda kinyume na kanuni ya 95(4) ya kanuni za Fedha ya
Mwaka 2005.
Alisema wakaguzi wa hesabu wameshindwa kupata
uthibitisho wa malipo na matumizi ya fedha hizo na hivyo kushindwa,
kujiridhisha kutokana na matumizi ya kiasi hicho cha fedha kama
zilivyokuwa zimetoka kupitia hati, hundi na kiasi cha fedha
kilichotumika.
CAG ameeleza kwenye ripoti hiyo kuwa, kati ya
hundi zilizokosa nyaraka za matumizi yake, 12 zilitumika kufanya malipo,
8 zimehusu malipo aliyolipwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif kwa
viwango tofauti hadi Juni mwaka uliopita.
Wakati ufujaji huo ukitokea katika Ofisi ya Makamu
wa Kwanza wa Rais, katika Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar,
Balozi Seif Ali Idd nako kumekosekana kielelezo cha matumizi ya Sh10.5
milioni kupitia malipo yaliyofanyika Januari 24, mwaka jana.
Mbali na Ofisi ya Makamu wa Kwanza kushindwa
kuwasilisha vielelezo vya matumizi ya fedha za walipakodi kiasi cha
Sh19.575 milioni, vielelezo vya matumizi yake vimeshindwa kupatikana kwa
maelezo kuwa fedha hizo zililipwa kampuni mbili ikiwamo ya Sami Trader
na Queen Tour and Traveler kupitia hundi namba 392366 na 392494.
“Kukosekana kwa vielelezo ni kwenda kinyume na
kanuni ya 95(4) ya kanuni ya fedha Zanzibar ya mwaka 2005 , kwa hali
hiyo uhalali wa malipo hayo haukuweza kuthibitishwa,” alieleza CAG Fatma
katika taarifa yake.
Mwananchi,Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza
wa Rais Zanzibar, Fatma Abdulhabib Ferej,alisema matumizi ya viongozi
wakuu wa Serikali yanasimamiwa na Wizara ya Fedha kupitia mfuko maalumu
wa Serikali.
‘Mimi sifahamu kama kuna matumizi yamekosa
maelezo,wanaotoa fedha za huduma za viongozi ni Wizara ya Fedha,wao
wanaweza kufahamu vizuri zaidi kwa sababu ndiyo wahusika wakuu,”alisema
Fatma.
Kuhusu bajeti kupita kiwango kilichoidhinishwa na
BLW alisema suala hilo ni geni kwake na hakumbuki Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais kuzidisha kiwango cha matumizi ya fedha licha ya suala
hilo kuwa limeripotiwa katika ukurasa wa 92 wa ripoti ya mkaguzi mkuu wa
Serikali Zanzibar.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha,Khamis Mussa alisema ni kweli ripoti ya CAG Zanzibar imehoji
baadhi ya vielelezo na nyaraka lakini anaamini fedha zote zilizotoka
zimetumika kama ilivyokuwa imekusudiwa.
SOURCE: MWANANCHI
Mussa alisema tatizo kubwa linalojitokeza ni kutokana na huduma
za usafiri wa ndege za viongozi pale wanapolazimika kukodi na baadhi ya
nyaraka kuchelewa kuwafikia zikiwamo nyaraka za malipo ya
huduma(invoice) kutoka kampuni zinazohusika hivyo kuwapa wakati mgumu
wanapofanyiwa ukaguzi.
Pia alisema watendaji dhamana bado wana nafasi ya
kuwasilisha nyaraka za matumizi kwa CAG ili waweze kufuta taarifa
zilizoripotiwa awali na kuonyesha kuwapo kwa matumizi ya fedha bila ya
vielelzo na matumizi yake.
Hivi karibuni wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
Zanzibar wamekuwa wakilalamika kuhusu vitendo vya ubadhirifu wa fedha za
Serikali na kuundwa Tume mbalimbali za uchunguzi ikiwamo Baraza la
Manispaa,Shirika la Umeme Zanzibar na ripoti kutoa mapendekezo ya
wahusika kuwajibishwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
SOURCE: MWANANCHI