Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Alhamisi,Oktoba17 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Oktoba17 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Baadhi ya wakaguzi hawafanyi kazi yao ipasavyo, wamekuwa wakifika kwenye viwanda na kunyamazishwa na wamiliki.
Dar es Salaam. Afya za baadhi ya Watanzania
ambao ni walaji wa kitoweo aina ya samaki zimeendelea kuwa hatarini
kutokana na kuwapo kwa dalili kwamba Serikali imeshindwa kudhibiti uwepo
wa samaki wabovu katika soko la ndani, wanaoingizwa kutoka nje ya nchi.
Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi pamoja na
taasisi nyingine zinazohusika na udhibiti wa viwango na ubora wa samaki,
kwa nyakati tofauti wametoa taarifa ambazo hazionyeshi hatua
wanazochukua kudhibiti samaki hao, huku kukiwa na uthibitisho wa kuwapo
kwa samaki wabovu katika baadhi ya kampuni zinazofanya biashara hiyo.
Itakumbukwa gazeti hili katika toleo la Jumamosi,
Septemba 28, liliandika kuwapo kwa samaki hao sokoni, wakiuzwa kwa wingi
na kwa bei ya chini katika Soko Kuu la Kimataifa la Feri, Dar es
Salaam, lakini taarifa hiyo ilikanushwa na Katibu Mkuu wa Chama cha
Waingizaji wa Samaki Tanzania, Barnabas Mapunda kupitia baadhi ya
magazeti ya kila siku.
Mapunda huku akitetea vyombo vya Serikali
vinavyohusika na ukaguzi, alisema: “Napenda kuchukua fursa hii kukanusha
taarifa hiyo (Samaki hatari waingizwa nchini) na kuufahamisha umma wa
Watanzania si kweli kuwa samaki wanaoingizwa kutoka nje ya nchi
hawakidhi ubora na usalama kwa matumizi ya binadamu.”
Hata hivyo, siku chache baadaye Mamlaka ya Chakula
na Dawa Tanzania (TFDA), ilikamata kilo 7,500 za samaki aina ya vibua
walioharibika ambao waliingizwa nchini Julai mwaka huu na Kampuni ya
Sais Boutique kutoka China.
Kadhalika maelezo ya Mapunda yanatofautiana na
kile ambacho gazeti hili limekibaini ndani ya Kampuni ya Alpha Krust Ltd
ya Dar es Salaam ambayo taarifa zake za ndani zinathibitisha kuwapo kwa
samaki walioingizwa nchini ambao hawafai kwa matumizi ya binadamu.
Uchunguzi ulibaini kuwa samaki hao (Frozen Pacific
Mackerel W/R (Scomber Japonicus) waliingizwa nchini Agosti 29, 2013
kutoka Korea Kusini na Kampuni ya Wookyung Co. Ltd: 1851 Jangheung –don,
Nam-gu ya jijini Pohang na waliagizwa na Kampuni ya Alphakrust Ltd ya
Dar es Salaam.
Taarifa zaidi zinaonyesha kuwa mzigo huo ulibebwa
na Kampuni ya Mediterranean Shipping (T) Ltd. Taarifa zaidi zinaonyesha
kuwa samaki hao walizalishwa Juni 4, 2013 na tarehe ya mwisho kutumika
ilitakiwa kuwa Juni 3, 2014. Hata hivyo, chanzo cha kuaminika katika
kampuni hiyo kimebainisha kuwa tarehe hizo hazina uhalisia kwani samaki
hao walikuwa wameshaharibika na kuwa hizo ‘sticker’ huwa wanabandika tu,
lakini ukweli ni kwamba samaki wanakuja wakiwa wameshaharibika ndiyo
maana huwa wanauzwa kwa bei ya chini, kilibainisha chanzo hicho na
kuongeza:
“Kuna samaki walioharibika wa aina mbili, kwanza
kuna walioathiriwa na mionzi na kuna wale waliokaa muda mrefu. Hawa
waliopo ni waliokaa muda mrefu na ukitaka kuwajua hao samaki, watoe
katika barafu na kuwaloweka, utaona wanapasuka na ukitia kidole
wanabonyea. Athari yake kubwa ni ugonjwa wa saratani ya matumbo,”
kilieleza chanzo chetu.
Katika taarifa ya ukaguzi wa kitengo cha ubora cha
kampuni hiyo (Organoleptic Assessment) uliofanyika Septemba 12, 2013
(nakala tumeiona), sampuli nne za samaki zilithibitika kutofaa kabisa
kwa matumizi ya binadamu.
Uongozi wa Alphakrust
Mkurugenzi wa Kampuni ya Alphakrust, Veda Gire alisema kabla ya
kuuza samaki wanapitia kwenye taratibu zote za Serikali ikiwemo ukaguzi
wa kina kutoka kwa mamlaka husika.
“Hao ambao wamepata samaki wabovu na wanaamini
wametoka kwangu walete ushahidi, lakini mimi ninachojua mamlaka husika
zimethibitisha kuwa wapo safi na ndiyo maana nauza na watu wanakula,”
alisema Gire.
Alipoelezwa kuhusu taarifa ya ukaguzi wa ndani ya
kampuni yake, Gire alisema: “Taarifa ya ukaguzi ya ndani ni siri ya
kampuni, kwa hiyo huwezi kufahamu aina ya vigezo tunavyotumia kufanya
ukaguzi wetu wa ndani, hiyo ni siri ya kampuni. “Kama unataka kufahamu
tunavyofanya kazi, wewe njoo hapa kwenye kampuni yetu, tutakuonyesha
kila kitu, hata wale wenzako (waandishi wa Mwananchi) walionipigia simu
wiki iliyopita niliwaalika waje hapa waone, hakuna siri,” aliongeza.
Msemaji wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS),
Roida Andusamile amekiri kuwa shirika hilo lilikutana na samaki hao
kabla hawajaletwa nchini.
“Ni kweli tulifanya ukaguzi wa samaki wa Alpha
Krust Agosti 6 mwaka huu kabla ya kuingia nchini na tuliwapa cheti cha
ubora. Sasa labda kama walikuja kuharibikia nchini baada ya kuingizwa,”
alisema na kuongeza:
“Tuna utaratibu ulioanza mwaka jana wa kukagua
mizigo kabla haijaingizwa nchini (Pre-shipment verification of
conformity to standard) na tunashirikiana na kampuni za kimataifa kama
vile SBS la Uswisi, Bureauveritas la Ufaransa na Intertec la Uingereza.
Mwagizaji akishakaguliwa hupewa ‘conformity certificate’, hata akifika
nchini tunaangalia cheti tu”.
Kwa upande wake, Mkaguzi wa Kanda wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa (TFDA), Emmanuel Alfonse amebainisha kuwemo kwa udhaifu
katika ukaguzi hasa bandarini wakati alipokuwa akieleza uingizwaji wa
bidhaa za vyakula nchini.
“Pale bandarini kuna idara tano zinazokagua, wapo
watu wa bandari, tupo TFDA, wapo TBS, wakala wa mionzi na Idara ya
Usalama wa Taifa. Wote tunafanya kazi chini ya baba yetu mmoja,” alisema
huku akisita kumtaja huyo ‘baba’.
“Hata hivyo bado mizigo bado inaweza kupenya bila
kukaguliwa, ndiyo maana tulikamata samaki kule Tabata,” aliongeza.
Akizungumzia kampuni inayotajwa kuingiza samaki hao, Alfonse alisema,
hata kama samaki hao waliharibikia kiwandani hapo, bado kampuni hiyo
ilipaswa kufuata utaratibu.
“Kama hao samaki waliingizwa Agosti 29 na Septemba
12 wakabainika kuharibika, mmiliki alipaswa kuwasiliana na Ofisa Afya
wa Manispaa ili apewe kibali cha kuwateketeza. Tutafuatilia
walikopelekwa, isije ikawa waliepelekwa sokoni,” alisema.
Msemaji wa TFDA, Gaudensia Simwanza alisema kabla ya mzigo kuingizwa nchini, mwingizaji anapaswa kuomba kibali.
Hata hivyo, alisema kuna changamoto kubwa ya wafanyabiashara hao kukwepa ukaguzi hasa wanapoingiza mzigo.
“Hiyo ni changamoto kubwa, kwa sababu mzigo ukishaingia
mwingizaji anatakiwa atujulishe na wakaguzi huchukua samaki na kwenda
nao maabara kuwapima. Kama yule tuliyemkamata wiki iliyopita, Sais
Boutique hakukaguliwa wakati wa kuingiza,” alisema Simwanza.
Kwa upande wake, Ofisa Afya wa Manispaa ya Ilala,
Ali Adinan alikiri kuwa kiwanda hicho kipo eneo la Ilala lakini akasema
hana taarifa ya kuwepo kwa samaki wabovu.
“Hatuna taarifa ya kuwepo samaki hao… tunafanya
ukaguzi kila mara na hata tuliposikia taarifa za kuwepo samaki wabovu
sokoni tulifanya ukaguzi katika kiwanda hicho lakini hatukukuta kitu.
Labda kwa kuwa umetupa taarifa tufuatilie tena,” alisema Adinan.
Kauli ya TPA, Waziri
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
kupitia taarifa yake ya Septemba 22 mwaka huu, imekanusha kuhusika na
uingizwaji wa samaki wabovu nchini na kwamba haina jukumu la kukagua
mizigo bandarini.
Kaimu Meneja Mawasiliano wa TPA, Janeth Ruzangi,
alisema jukumu la mamlaka hiyo ni kupakua na kupakia mizigo melini na
kwamba mizigo inayopakuliwa huhifadhiwa sehemu maalumu kusubiri wahusika
ambao hukabidhiwa baada ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa.
“Kwa mizigo kama hii ya chakula chenye kukaa
kwenye barafu au baridi, kawaida huwa inapakiwa kwenye makontena maalumu
ya baridi (refrigerated containters).
“Mara inapokuwa imeshushwa bandarini huwekwa
kwenye sehemu ya umeme kwa kiwango cha baridi (reefer points) ambacho
mwenye meli ataagiza kiwekwe kulingana na vile ilivyokuwa ndani ya meli
kabla ya kushushwa na Maafisa wa Bandari kukagua kila baada ya saa mbili
ili kuhakikisha hakuna mabadiliko ya kiwango cha baridi na endapo
patatokea hitilafu ya umeme, majenerata yataendelea kutoa umeme,”
alieleza Ruzangi.
Alisema baada ya mwenye mizigo kupata nyaraka zote
husika ndipo TPA itaruhusu mzigo huo kutoka kupitia katika milango yake
iliyopo bandarini na si vinginevyo.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Dk
David Mathayo David, amekuwa akisita kuzungumza na gazeti hili kila
anapotafutwa kwa njia ya simu.
Septemba 13, mwaka huu alipotafutwa alisema: “Niko
njiani naendesha hivyo siwezi kutolea ufafanuzi suala hilo”. Oktoba 10
alipopigiwa tena simu alisema: “Kwa sasa siwezi kuzungumzia suala hili,
ila kesho (Oktoba 11) nitakuwa na press conference (mkutano na waandishi
wa habari), nitaeleza kwa kirefu”.
Alipopigiwa simu, Oktoba 11 na kuulizwa kuhusu wapi mkutano huo utafanyika alijibu kuwa mkutano huo umeahirishwa.
Hata hivyo siku hiyo hiyo alifanya mkutano huo na waandishi
wengine ofisini kwake jijini Dar es Salaam, ambapo pamoja na mambo
mengine alizungumia uingizwaji wa samaki hatarishi kutoka nje ya nchi.
“Baadhi ya wafanyabiashara wa samaki hawazingatii
kanuni za uvuvi hususan katika usafirishaji wa samaki. Kuna wengine
magari wanayotumia hayana majokofu na mengine huwa wazi kwa hiyo samaki
huwa wanaingia vumbi na moja kwa moja hukosa matunzo mazuri.
“Pia uuzaji wa samaki kwa njia ya mnada unachangia
uharibifu kwa kuwa mara nyingi huchomwa na jua kali wakati samaki muda
mwingi wanahitaji baridi kutokana na kuwa na protini nyingi,”alisema Dk
Mathayo.
Aliongeza Serikali haiwezi kuacha kuagiza samaki
kutoka nje ikizingatiwa ni sehemu ya uchangiaji wa pato la taifa lakini
pia huwapa faida kubwa wafanyabiashara wa ndani.
Alisema samaki wanapowasili nchini serikali kwa kushirikiana na TFDA, huwathibitisha kabla ya kuwaruhusu kuingizwa sokoni.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI