Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Alhamisi,Oktoba17 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Oktoba17 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Kwa mujibu wa sheria, Vyama vya siasa vinapaswa kuwasilisha hesabu zake kwa CAG kwa ajili ya kufanyiwa ukaguzi.
Dar es Salaam. Maelekezo yaliyotolewa na
Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kutaka
kusitishwa kwa ruzuku kwa vyama vya siasa nchini kutokana na
kutowasilisha taarifa za ukaguzi wa matumizi yake, yamevivuruga baadhi
ya vyama vilivyotajwa.
Vyama vya siasa vinaonekana kutoa matamshi
yanayolenga kujinasua katika hoja hiyo, vikiwemo vilivyomshutumu Zitto,
kuilaumu Serikali na hata vingine vimediriki kutaka ruzuku hiyo ifutwe
kwa maelezo kwamba ni ubadhilifu wa fedha za umma.
Juzi Zitto alisema tangu 2009 Serikali ilitoa
kiasi cha Sh67.7 bilioni kama ruzuku kwa vyama tisa vya siasa, lakini
vyama hivyo havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi hesabu zake
msajili kama sheria inavyoagiza. Kwa sababu hiyo, Zitto aliamuru Ofisi
ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kusimamisha utoaji wa ruzuku hadi
hapo vitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi na makatibu wake wakuu
kuhojiwa.
Kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya 1992 ambayo
ilifanyiwa marekebisho ya Sheria namba 7 ya 2009, Vyama vya Siasa
vinawajibika kuwasilisha hesabu zake kwa CAG na ofisi hiyo inaweza
kuamua kuzifanyia ukaguzi yenyewe au kuteua mkaguzi.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Ludovick Utouh aliwahi kusema kuwa utaratibu ambao umekuwa
ukitumiwa na vyama hivyo kwa kuteua kampuni binafsi siyo sahihi na ni
kinyume cha sheria.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 14 cha Sheria ya Vyama
vya Siasa, vyama vinatakiwa viwasilishe hesabu kwa CAG, ndipo tuzikague
au tuamue kampuni ya kufanya ukaguzi huo, sasa wao walichagua kampuni
binafsi moja kwa moja zikawafanyia ukaguzi,” alisema Utouh wakati
akitangaza kuthibitisha ubora wa hesabu za vyama vitano vilivyoshiriki
kwenye Uchaguzu Mkuu wa 2010.
Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), Mchungaji
Christopher Mtikila alipendekeza kufutwa kwa ruzuku hiyo kwa vyama vya
maelezo kuwa ni inawanyonya wananchi.
“Badala ya kuvipa vyama vya siasa ruzuku,
tuelekeze fedha hizo kwenye miradi mingine ya maendeleo,” alisema
Mtikila huku akiahidi kwamba chama hicho kitawasilisha kwa Msajili wa
Vyama vya Siasa taarifa yake ya fedha iliyokaguliwa katika kipindi cha
wiki mbili kuanzia sasa.
CCM wang’aka
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimemshambulia kiongozi
huyo, huku kikisema kuwa Zitto ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema
anapaswa kushughulikia matatizo yaliyopo katika chama chake kwanza kabla
ya kuzungumzia matatizo katika vyama vingine vya siasa.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
alisema chama hicho hakihusiki na agizo la PAC la kusimaishiwa ruzuku ya
kila mwezi, kwani hesabu zake zimekuwa zikifanyiwa ukaguzi. Alisema CCM
ipo tayari kwenda mbele ya PAC kikiwa na hesabu zilizokaguliwa na
wakaguzi wa nje, Shirika la Ukaguzi la Taifa (Tanzania Audit Corporation
- TAC) kuanzia 1977/1978 hadi 2010/2011.
“Januari 29, mwaka huu niliandika barua yenye
kumbukumbu namba CMM/F. 20/80/89 ili kuwasilisha rasimu ya hesabu za
mwaka wa fedha 2011/2012 lengo likiwa CAG atupangie siku ya TAC
kutukagua,” alisema Nape na kuongeza: “Hesabu zilizokaguliwa na wakaguzi
wa nje TAC ambazo ni za 2009/2010 na 2010/2011 tayari ziliwasilishwa
kwa CAG.”
Nape alifafanua kwamba hesabu za 2011/2012 bado ziko kwa
wakaguzi wa nje, wakishakamilisha nazo zitawasilishwa kwenye vikao vya
chama na hatimaye kwa CAG.
“Hesabu hizi zikikaguliwa kwa mujibu wa utaratibu,
anapelekewa CAG ambaye ndiye anazipeleka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa
na sio vinginevyo,” alisema.
Alidai kuwa Zitto anapaswa kuanza kutoa ‘boriti
kwenye jicho lake ndipo aone kibanzi kwenye jicho la mwenzake’ kwa
sababu chama chake ndicho kimekuwa na matumizi mabaya ya ruzuku. Alisema
Zitto kama Naibu Katibu Mkuu wa Chadema ni vyema akawajibika ndani ya
chama chake ili kuonyesha mfano kwa wengine.
“Wote tunakumbuka kelele zilizopo mtaani kuhusu
matumizi mabaya ya ruzuku zinazoelekezwa na Chadema na viongozi wake
kutoka kwa wanachama wao, hivyo si ajabu wakawa wanakiuka sheria hii na
ndiyo chanzo cha kelele hizo za wanachama wao,”alisema.
Vyama vingine
Kwa upande wake, Chadema kilieleza kwamba
hakijapata barua inayowaarifu kuhusu kutaka kufungiwa ruzuku kutokana na
kutowasilisha taarifa ya ukaguzi.
Ofisa Habari Mwandamizi wa Chadema, Tumaini Makene
ilisema hata barua ya kuitwa kwenye Kamati ya PAC, iliwafikia kwa
kuchelewa. “Tunasubiri barua rasmi ya suala hili ndio mamlaka
zinazohusika na masuala ya fedha ndani ya chama, hususan, Baraza la
Wadhamini wa Chama kuweza kutafakari hatua,” alisema Makene.
Hata hivyo, alisema angependa umma utambue kwamba
“Chadema ndicho kilichokuwa mstari wa mbele tangu kabla na baada ya
mwaka 2009 kutaka ukaguzi na wazi katika mapato na matumizi ya vyama vya
siasa.”
Alifafanua kuwa msimamo wa Chadema kwenye
mkakakati huo ulikuwa ni kuibana CCM kutokana na madai ya baadhi ya
vigogo wake “kukwapua fedha Benki Kuu ( Akaunti ya Madeni ya Nje – EPA)
na kuzitumia kwenye uchaguzi wa mwaka 2005.”
Alijigamba kuwa hesabu za chama chake zimekuwa
zikikaguliwa kila mwaka na kwamba wanasubiri maelezo ya barua kuhusu
kile kinacholalamikiwa.
Kwa upande wa Chama cha Wananchi (CUF) kimesema
hesabu zake ziko safi, ila imeshindikana kukaguliwa kwa vile Serikali
haijatoa fedha za kugharimia ukaguzi huo.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Tanzania Bara, Julius Mtatiro alisema hesabu zao zimekwishakaguliwa na wakaguzi wa ndani.
“Tunachosubiri ni Serikali kutuletea mkaguzi ambaye baada ya
kufanya hivyo hesabu zetu zitakuwa zimekamilika na wananchi wataweza
kuziona,” alisema.
Alisema chama hicho hakina fedha kwa ajili ya kugharimia mkaguzi wa nje na kwamba jukumu hilo ni la Serikali.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Samwel
Ruhuza alisema kuwa chama hicho kipo tayari kuwasilisha hesabu zake,
kwani zipo tayari na kwamba walishindwa kuziwasilisha baada ya kuelezwa
kuwa CAG ndiye anayepaswa kufanya ukaguzi.
Imeandaliwa na Aidan Mhando, Leon Bahati, Fidelis Butahe na Raymond Kaminyoge
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI