Posted
Alhamisi,Oktoba17
2013
saa
24:0 AM
Kwa ufupi
Kutokana na mvutano huo ni wazi kwamba
usingekuwa na tija kwa Serikali wala Tatoa na Taboa, bali ungeleta
maumivu makubwa kwa wananchi.
Tumeshuhudia mvutano kati ya Waziri wa Ujenzi,
Dk John Magufuli na Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) ambao
wanapinga sheria ya tozo ya asilimia tano kwa wasafirishaji wanaozidisha
mizigo na kusababisha uharibifu wa barabara.
Mbali na Tatoa, Chama cha Wamiliki wa Mabasi
Tanzania (Taboa) pia wanapinga sheria hiyo ya barabara namba 30 ya mwaka
1973 na marekebisho yake ya mwaka 2001.
Waziri Magufuli alisema anasimamia sheria hiyo ili
kuhakikisha barabara haziharibiwi na watu wachache wenye nia ya
kujinufaisha binafsi bila kujali masilahi ya Taifa.
Hata hivyo wamiliki hao kupitia Tatoa walisema
Waziri huyo amerudisha tozo ya asilimia tano kwa maslahi yake na amekuwa
mtu ambaye haambiliki, hashirikiani na wadau pamoja na kujichukulia
sheria mkononi.
Wakizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam
wamiliki hao walieleza kuwa sheria hiyo iliyotangazwa na Magufuli
ilianza kutumika Oktoba Mosi na kupatiwa barua Oktoba 2, mwaka huu ya
kueleza kwamba tozo hiyo imeondolewa jambo ambalo lilisababisha
msongamano. Hata hivyo Waziri Mkuu, Mizengo Pinga aliumaliza mgogoro huo
na kuruhusu wamiliki wa magari hayo kuendelea na safari zao kwa mwezi
mmoja wakati jitihada nyingine zikiendelea.
Pinda alisema kutokana na sakata hilo, amelazimika
kuunda kamati ambayo itakutana na wadau, Tatoa na Taboa ili kupata
ufumbuzi wa mgogoro uliojitokeza. Athari zilizojitokeza ni pamoja na
kusimama kwa upakuaji na upakiaji wa mizigo katika Bandari ya Dar es
Salaam, kukwama kwa usafirishaji wa mizigo ndani na nje ya nchi na
kukwamisha biashara na huduma za jamii kwa wananchi.
Kutokana na mvutano huo ni wazi kwamba usingekuwa
na tija kwa Serikali wala Tatoa na Taboa, bali ungeleta maumivu makubwa
kwa wananchi.
Pamoja na ushupavu wake Dk Magufuli katika
kusimamia sheria, mimi naona wakati mwingine atumie pia busara, kwani
wakati mwingine sheria pekee hazitatui matatizo.
Ni kweli kwamba Dk Magufuli anasimamia sheria
halali, lakini ajue kwamba sheria hizo hutungwa na Bunge
linalowawakilisha wananchi. Dk Magufuli akitoa tamko lake anasema
wasafirishaji wengi nchini ni wanasiasa, kama wanaona kuondolewa kwa ofa
ya uzito uliozidi wa asalimia tano wapeleke hoja bungeni ipitishwe
rasmi.
Dk Magufuli akaendelea kusema kuwa, wanaogomea ni matajiri hivyo waende mahakamani.
Ubabe huu hauna tija yoyote, badala yake anashiriki kwa namna moja au nyingine kuhujumu uchumi wa nchi.
Nchi yetu inapaswa kuondoa vikwazo hivyo ili
kuimarisha biashara za ndani na nje ya mipaka yake. Nchi yetu hii ina
bandari ambayo inategemewa na nchi kama vile Zambia, Zimbabwe, Rwanda,
Burundi, Malawi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC). Anachotakiwa
kufanya Dk Magufuli ni kuimarisha utengenezaji wa barabara kwa kuongeza
kiwango cha ubora ili magari yachukue uzito mkubwa zaidi.
Kwa upande mwingine, Serikali ichukue changamoto hii kama nafasi
ya kufufua Mashirika ya Reli ya TRC na Tazara badala ya kuachia tu
malori yasafirishe mizigo. Wakati sasa umefika mizigo isafirishwe kwa
reli ili kuepuka msongamano wa magari, uharibifu wa barabara na
kuharakisha mizigo inafika kwa wateja kwa wakati.
Kazi ya Waziri Mkuu Pinda isiwe kusubiri migogoro
tu, bali aisimamie Serikali ifufue njia mbadala za usafiri. Ni aibu kwa
nchi yetu yenye zaidi ya miaka 50 ya uhuru, inashindwa kuendesha
mashirika ya usafirishaji kwa mfano shirika la reli na ndege ambayo
yaliyoachwa na wakoloni.
0754 897 287