Na Daria Erasto, Mwananchi
Posted Alhamisi,Oktoba17 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Oktoba17 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Alisema alipigiwa simu na mdogo wa marehemu kuwa mkewe ameugua ghafla na hana nguvu na kwamba anapaswa aende haraka akamuone.
Dar es Salaam. Mwanamke mmoja wa Ilala jijini
Dar es Salaam, Mwanahamisi Saidi amefariki dunia wakati
akijiandaa kwenda kwa mumewe baada ya kufunga ndoa.
Tukio hilo la kuhuzunisha lilitokea Jumapili
iliyopita, muda ambao bibi harusi alitakiwa kuchukuliwa na mumewe Amani
Hassan kwenda nyumbani kwake.
Mwanahamisi aliaga dunia akiwa katika Hospitali ya Amana iliyoko Wilaya ya Ilala, baada ya kuugua ghafla.
Akizungumza kwa majonzi, Hassan alisema kuwa
alifunga ndoa kwa taratibu za Dini ya Kiislamu Ijumaa iliyopita katika
msikiti ulioko Vingunguti jijini Dar es Salaam na kupanga kwenda
kumchukua mkewe siku ya Jumapili.
“Baada ya kufunga ndoa niliwaahidi ndugu wa mke
wangu kuwa nitakwenda kumchukua mke wangu Jumapili kwa sababu upande
wangu ulikuwa umeandaa sherehe iliyoanza Jumamosi na Jumapili ndio
tulipanga kumaliza kwa kumchukua mwali wetu,” alieleza kwa masikitiko
Hassan.
Alisema alipigiwa simu na mdogo wa marehemu kuwa mkewe ameugua ghafla na hana nguvu na kwamba anapaswa aende haraka akamuone.
“Nilipofika nikamkuta mwenzangu hali yake ni
mbaya, hawezi kuongea na alikuwa ameshapoteza fahamu, nikafanya
utaratibu wa kumpeleka Hospitali ya Amana,”aliongeza Hassan.
Alisema walipofika Amana, waliambiwa kuwa mgonjwa
wao ameishiwa damu na wakati wakiwa katika harakati za kumhudumia,
Mwanahamisi alizidiwa zaidi. Alisema bibi harusi alishindwa kupata
pumzi, na hivyo kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua lakini ilipofika
saa nane mchana aliaga dunia.
“Mshtuko wa taarifa zile ulinifanya nipoteze
fahamu kwa muda, baada ya kuzinduka sikuwa na jinsi zaidi ya kumpigia
dada yangu, ambaye ndio kama mzazi wangu kwa kuwa tupo wawili tu, wazazi
wetu walishafariki.
Nilimtaarifu habari hizi za huzuni na kumuomba awaambie watu waahirishe sherehe na maandalizi yote ya kwenda Vingunguti.
Alisema wakati anatoa taarifa hizo tayari nyumbani
kwao kulikuwa kumepikwa vyakula na shamshamra za muziki na ngoma
zilikuwa zikiendelea.
“Yaani mpaka sasa siamini kilichotokea, tulikuwa na mipango mingi na mke wangu, hata picha za ndoa yetu bado sijazichukua najisikia uchungu sana ninapokumbuka tukio zima,” alisema Hassan.
SOURCE: MWANANCHI
“Yaani mpaka sasa siamini kilichotokea, tulikuwa na mipango mingi na mke wangu, hata picha za ndoa yetu bado sijazichukua najisikia uchungu sana ninapokumbuka tukio zima,” alisema Hassan.
SOURCE: MWANANCHI