Tuesday 5 November 2013

Kagasheki aandamwa kwa kuwalinda tembo


5th November 2013
Waziri wa Maliasili na Utalii,Balozi Khamis Kagasheki
Vita dhidi ya ujangili inaelekea kuvaa sura mbalimbali ikiibua hisia kwamba wapo baadhi ya watu ambao hawataki kuona inatokomezwa, ndiyo maana Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amekuwa akilengwa kwa kila njia ili ama kumuondoa kwenye mapambano hayo au kumkatisha tamaa.

Bila kusahau kuwa Tanzania ipo kwenye mstari mwekundu mbele ya jamii ya kimataifa jinsi inavyopambana dhidi ya ujangili kutokana na kuwa chanzo kikuu cha biashara haramu ya pembe za tembo, kwa takribani miaka minane sasa tangu kuingia kwa serikali ya awamu ya nne madarakani mwaka 2005, mawaziri watano waliopita kwenye wizara hiyo isipokuwa Balozi Kagasheki walishindwa kuanzisha operesheni hiyo.

Miaka mitatu iliyopita Shirika la Kimataifa la Kulinda Viumbe ambao wako katika hatari ya kutoweka (CITES), liliikatalia Tanzania kuuza shehena ya pembe za tembo tani 20 baada ya kupingwa na nchi nyingine ikiwamo Kenya na Rwanda, kwa tuhuma za kushindwa kudhibiti ujangili dhidi ya tembo.

Mwelekeo wa kuiandama vita dhidi ya ujangili imekuwa ikijitokeza katika sura mbalimbali kama vile kauli za kutaka kusitishwa kwa operesheni tokomeza na kuwajibishwa kwa wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.

Mawaziri ambao walipata kuongoza Wizara ya Maliasili na Utalii tangu kuanza kwa awamu ya nne, ni pamoja na  Antony Diallo, Profesa Jumanne Maghembe, Shansa Mwangunga na Ezekiel Maige.  

Hali hiyo ikizidi kutanda nchini kauli ya Balozi Kagasheki, aliyoitoa nje ya Bunge kuwashambulia wabunge kwamba, hawajali maslahi ya Taifa, hatishwi na maelezo yao na kwamba hawezi kujiuzulu mpaka Rais Jakaya Kikwete aliyemteua aamue kumuondoa, imeibua mtikisiko mwingine bungeni. 
Jana Mbunge wa Sikonge (CCM), Said Nkumba, ameziita kauli hizo za Waziri Kagasheki kuwa ni za kulikejeli Bunge na kubeza maamuzi yake.

Nkumba alisema hayo wakati akiomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya Bunge ya 68 (7) muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na matangazo bungeni jana, wakati Spika Makinda alitoa kauli hiyo alipokuwa akiutolea uamuzi mwongozo huo.

Nkumba alisema ni juzi (wiki iliyopita) tu wabunge walijadili kwa kina suala la dharura juu ya maonevu, ambayo inadaiwa wamefanyiwa wananchi katika maeneo mbalimbali kupitia ‘Operesheni Tokomeza’ na Bunge kulifanyia maamuzi.  Lakini akasema Jumapili na Jumamosi wiki iliyopita, Waziri Kagasheki alionekana na kunukuliwa kwenye vyombo vya habari akisema kwamba: “Wabunge wanasema sema tu ndani ya Bunge, lakini hawajali rasilimali za Taifa.”

Mbali na hilo, Nkumba alisema pia Waziri Kagasheki alinukuliwa na vyombo hivyo akisema kuwa hatishwi na maelezo ya wabunge ya kumtaka ajiuzulu na kwamba, hawezi kujiuzulu mpaka Rais Kikwete aliyemteua aamue hilo.

 “Sasa kwa kuwa yeye mwenyewe Mheshimiwa Waziri (Kagasheki) ndiye aliyetoa kauli ya kusitisha Operesheni Tokomeza. Na kitendo cha kuwakamata Wachina ni zoezi tu la serikali la kila siku ambalo linaweza likaendelea bila ya operesheni. 

“Je, Mheshimiwa Spika, waziri aliyetoa kauli ndani ya Bunge na anatoka nje anabeza maamuzi ya Bunge, anakejeli Bunge? Naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika kama jambo hili linaruhusiwa,” alisema Nkumba.

Akitolea uamuzi maombi ya mwongozo wa Nkumba, Spika Anne Makinda, alisema kilichosemwa na waziri huyo huyo ni matumizi mabaya ya midomo, ambayo hayapaswi kutumika.  “Kwa sababu tukishakubaliana hapa, tena kwenda kusema vitu vingine, ni kuwasha moto pale ambapo pengine ulikuwa ukiendelea kuwaka vizuri, mimi nadhani ni matamko ambayo siyo makini,” alisema Spika Makinda. 

Jumamosi wiki iliyopita, Waziri Kagasheki akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamatwa raia watatu wa China jijini Dar es Salaam wakiwa na meno zaidi ya 200 ya tembo na fedha taslimu Sh. milioni 30.2, alisema licha ya kushambuliwa bungeni na baadhi ya wabunge kuhusu operesheni hiyo, hawezi kuacha kuwatetea tembo ambao wanazidi kuangamia. Meno hayo ni sawa na mauaji ya tembo 100 kwa kuwa kila mmoja ana meno mawili.

“Serikali pamoja na kusimamisha operesheni hiyo, lakini bado inalichukulia kwa uzito maangamizo ya tembo…wabunge wanaongea tu bila kujali rasilimali za nchi, siwezi kuacha kabisa kutekeleza wajibu wangu,” alisema Waziri Kagasheki.  Alisema pamoja na malalamiko ya wabunge, baadhi ya wananchi na mifugo wamedhurika, lakini hataacha kulinda wanyamapori.
Waziri Kagasheki alisema tukio la kukamatwa kwa Wachina hao, linaonyesha ni jinsi gani tembo wengi wanavyouawa na meno yake kusafirishwa nje ya nchi kwa kuuzwa.

“Tumesimamisha operesheni, nani atawasemea tembo…kweli ipo mifugo imeuawa katika operesheni tokomeza ujangili, lakini hatuwezi kuwaacha watu kama hawa. Tukianza kutajana baadhi ya wabunge hawatapona,” alisema Waziri Kagasheki. Hata hivyo, alisema wabunge wasijidanganye kwamba watamng’oa madarakani, bali mwenye mamlaka ya kumtoa ni Rais Kikwete, ambaye ndiye alimuamini na kumpa wizara hiyo. 

Zoezi la kuwakamata Wachina hao, liliendeshwa na Waziri Kagasheki na kikosi maalumu cha polisi, ambayo liliwanasa Wachina hao waliokuwa wakiishi katika Mtaa wa Faru, Mikocheni jirani na nyumba za mawaziri, jijini Dar es Salaam.

Ijumaa wiki iliyopita, Bunge liliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza na kuchambua sera mbalimbali zinazohusu ardhi, kilimo, mifugo, wanyamapori na uwekezaji. 
Lengo ni kubaini kasoro za ardhi, hatimaye kupeleka mapendekezo bungeni yatakayoondoa migogoro ya ardhi inayoendelea kati ya wakulima, wafugaji, hifadhi, uwekezaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Pamoja na Bunge kuridhika kuwa operesheni za Kimbunga na Tokomeza majangili zilikuwa na kasoro kubwa na kuridhia kuundwa kamati teule ya Bunge kuchunguza, tishio la kutoweka kwa tembo bado ni kubwa kutokana na kasi kubwa ya majangili kuwaua wanyama hao ambao ni urithi wa taifa.

Hatari hiyo inatokana na uamuzi wa kuisitisha operesheni Tokomeza kwa madai kwamba ilikuwa ikiendeshwa kinyume cha haki za binadamu huku kasi kubwa ya kuua wanyama hai ikiendelea kila uchao. Hali hiyo inadhihirishwa na matukio ya kukamatwa kwa kiasi kikubwa cha meno ya tembo katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mfano, mbali ya tukio la Jumamosi iliyopita la kukamatwa kwa meno ya tembo 200 yalikuwa na uzito wa kilo 1,834, katikati ya wiki iliyopita shehena nyingine ya meno ya tembo 90 (sawa na tembo 45) ilikamatwa wilayani Masasi mkoani Mtwara.

Kwa maana hiyo kwa wiki mbili tu tembo ambao wameteketezwa ni 145. Hizi ni takwimu za kutisha sana ikizingatiwa kwamba hivi sasa tembo 30 wanauawa kila siku katika hifadhi za taifa na mapori ya akiba. 

Kutothamini na kupinga hatua anazozichukua Waziri Kagasheki katika kulinda wanyama hao wasitoweke ni sawa na kutojali urithi wa wanyama hao ambao wakitoweka taifa litapata hasara kubwa.
 
CHANZO: NIPASHE