Tuesday 5 November 2013

Edward Lowassa: Vijana watatung`oa madarakani


5th November 2013
  Aeleza yaliyotokea kwingineko Afrika hayaepukiki ikiwa�
  Awafagilia Mwakyembe na Magufuli kwa uchapakazi thabiti
Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Lowassa akichangia mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa mwaka wa fedha ujao ndani ya Bunge mjini Dodoma jana.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ametahadharisha kuwa kama tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana halitapatiwa ufumbuzi, itakuwa chanzo cha serikali kupoteza madaraka.

Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli (CCM), alisema hayo jana wakati akichangia mjadala wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2014/2015, uliowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.

Lowassa alisema serikali inapaswa kuangalia kipaumbele muhimu na kinachowezekana kutekelezwa cha kuanzia na kufuatia kingine.

Alisema kama angekuwa yeye (Lowassa), angeanza na kipengele cha ajira. “Huwezi kuzungumza mipango bila kuzungumza habari ya ajira,” alisema Lowassa.

Alisema serikali inapaswa kukiri kwamba, kuna  Watanzania wengi waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne na cha sita, walioko mitaani hawana ajira. Tusipoangalia watakuja kula sahani moja na sisi. Tusipowashughulikia,” alitahadharisha Lowassa.

Alisema iwapo serikali haitokuwa macho juu ya hilo na kulishughulikia, yale yanayotokea katika nchi mbalimbali barani Afrika, yanaweza pia kutokea hapa nchini.

Ingawa Lowassa hakufafanua maana ya kula sahani moja wala kutaja nchi za Afrika ambazo zimesumbuliwa na vijana, Tunisia na Misri ni miongoni mwa nchi zilizokumbwa na vuguvugu la mageuzi kiasi cha kusababisha watawala kuondolewa madarakani.

Vijana kwa maelfu waliingia mitaani katika nchi hizo wakipinga hali mbaya ya uchumi hasa kukosekana kwa ajira na mwishowe serikali zilizokuwa madarakani ziliangushwa. 
Lowassa alisema katika mkutano wa Benki ya Dunia (WB) uliofanyika mwaka huu kulizungumzwa habari kuhusu mdororo wa kiuchumi uliolikumba bara la Ulaya.

Alisema moja ya nchi zilizokumbwa na tatizo hilo ni Hispania, ambayo alisema katika kujinasua, ilimbana kila mwekezaji aliyekuwa akiingia katika nchi hiyo kwa kumpa sharti la kuwekeza ajira ya vijana.
Kwa mujibu wa Lowassa, mkakati huo uliisaidia Hispania, ambayo katika miaka miwili mitatu iliyofuatia ilifanikiwa kujinasua kuondokana na tatizo hilo.
“Lazima tuangalie suala la ajira, ni muhimu sana. Mipango mingine haiwezekani bila kutizama suala la ajira,” alisema Lowassa.

Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwassa, na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, mkoani humo, Elibariki Kingu, ambao alisema wameanza kuhangaikia suala la ajira kwa vijana.  Alisema iwapo kila wizara ikiamua kushughulikia suala la ajira kwa vijana linawezekana.

“Yule mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya wameamua kuchukuwa vijana waliomaliza Chuo Kikuu, wamewatafutia mashamba, wamewatafutia trekta. Wale vijana wamefanya kazi nzuri sana. Kwa hiyo, inawezekana,” alisema Lowassa.

Kadhalika, alisema mipango mingi ya maendeleo nchini imekuwa haifanikiwi kutokana na serikali kutokuwa na msimamo wa kufanya maamuzi magumu.
Badala yake, alisema imekuwa ikiishia kupanga, lakini hakuna utekelezaji na hivyo kuungana na wananchi kulalamikia kukwama kwa mambo.

Alisema anapongeza sana uamuzi wa serikali kuanzisha kitengo maalumu kilicho chini ya Ofisi ya Rais, kijulikanacho kama ‘Presidential Delivery Bureau’ (PDB), kinachosimamia mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na kusema: “Hongereni sana.”

Hata hivyo, akaitaka serikali kujiuliza maswali kama kitengo hicho kina ‘meno’ ya kufanya maamuzi magumu?

 “Tatizo la nchi hii mnazungumza mambo hakuna utekelezaji. Tunazungumza, lakini discipline (nidhamu) ya (nchi ya) Malaysia na hapa (Tanzania) ni tofauti. Hapa kuna uswahili mwingi wa kukaa bila kutekeleza mambo, mnaamua hamtekelezi,” alisema Lowassa.

Alishauri kuwapo na chombo, ambacho kinaweza kufanya maamuzi magumu na yakawa magumu yanayotekelezeka kweli kweli.
Alisema tabia ya kujivika joho la kufanya maamuzi ya utekelezaji, lakini bila kufanya, ni kazi bure.

Kwa hiyo, akasema uamuzi wa kuwa na PDB ni mzuri, lakini akasisitiza kuwa usipoangaliwa itakuwa ni sawa kufanya kazi bure, hivyo akashauri ni lazima kuwapo na meno ya kuuma.
“Tukikubaliana mambo yafanyike. Haiwezekani katika nchi kila mtu akawa analalamika. Kiongozi analalamika, mwananchi analalamika, haiwezi ikawa ni jamii ya kulalamika lalamika. Awepo mtu mmoja anayefanya maamuzi na anayechukua hatua,” alisema Lowassa.

Alisema bila kuchukua hatua, kazi ya serikali na wananchi itabaki kuwa ya kulalamikiana.

Alitoa mfano wa uhasama uliopo baina ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), akisema hakuna haja kwa Tanzania kugombana na marais; Paul Kagame (Rwanda), Uhuru Kenyatta (Kenya) na Yoweri Museveni (Uganda) kwa kuamua kushirikiana kiuchumi na Sudan Kusini na kuitenga Tanzania.

Alisema kwani Tanzania inaweza kushirikiana na Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Goma, ambako alisema ni kuzuri zaidi ya Sudan.
 Lowassa alisema inachohitaji Tanzania kufikia hilo, ni kufufua reli ya kati ili kuzalisha kuliko nchi hizo.

VIPAUMBELE KATIKA MPANGO WA MAENDELEO

Kuhusu vipaumbele vilivyomo katika Mpango huo, alisema ni vingi na kushauri kwamba, vingechaguliwa vichache vikasimamiwa na kutekelezwa.
Alisema kupanga vipaumbele vingi kwa wakati mmoja ni vigumu kutekeleza vyote.

ELIMU

Alisema kipaumbele cha pili ambacho alishauri kipewe kipaumbele ni elimu. Lowassa alisema kinachozungumzwa juu ya elimu hakipaswi kupuuzwa na kusema lipo tatizo la msingi katika elimu ya Tanzania, kwani vitu vinavyochukuliwa havitoshelezi.

Alisema alitegemea kuwa Kamati ya Bajeti ingepata taarifa ya Waziri Mkuu iliyotolewa juu ya elimu kama ingetambua baadhi ya matatizo, serikali ikaangalia cha kufanya.

“Haitoshi kuchukua wanafunzi wengi wanaomaliza Chuo Kikuu wakati akienda sokoni uwezo wake wa kimasomo haupo sokoni” alisema Lowassa.

 Alisema hiyo inatokana na wanafunzi wengi wanaomaliza Chuo Kikuu kutokuwa na hakika ya ajira kwa sababu ya kutokuwa na uwezo wa kushindana katika soko.

Lowassa alisema kelele zinazopigwa na wananchi juu ya elimu nchini, inafaa ukafanyika mjadala kuangalia tatizo lililopo katika elimu na nini cha uhakika cha kufanya.

Alisema vinginevyo serikali isipoangalia, Tanzania itaachwa nyuma na EAC, Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na dunia kwa jumla, badala yake itabaki kuwa mbabaishaji katika soko la elimu.

“Tuwasaidie vijana wetu, tubadilishe mfumo wa elimu, tuangalie tunaweza kufanya nini vizuri zaidi,” alisema Lowassa.

AMSIFU WAZIRI MAGUFULI

Alisema kipaumbele cha tatu kwa maoni ni reli ya kati na kwamba, anamsifu sana Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, kwa kazi nzuri ya ujenzi wa barabara aliyoifanya.

Lakini akasema barabara hizo zimeanza kuharibika kwa kasi ya hali ya juu sana.  “Tumetoka Singida juzi, barabara imeharibika vibaya sana. Ile ya Shinyanga, imeharibika vibaya sana. Kwa sababu malori yanayokwenda yanayopasa kutembea kwenye treni yanatembea kwenye barabara…Naomba reli ya kati muiangalie kwa haraka sana,” alisema Lowassa.

FOLENI DAR, AMSIFU WAZIRI MWAKYEMBE

Akizungumzia tatizo la foleni jijini Dar es Salaam, kwanza alimpongeza Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kwa kazi nzuri anayoifanya ya kupambana na tatizo hilo.

Hata hivyo, alisema jitihada hizo za Waziri Mwakyembe pekee hazitoshi, kwani muda wa saa ambazo wakazi wa Dar es Salaam wanaoupoteza kwenye foleni zikipangwa kwa ajili uzalishaji ni nyingi sana.

Kwa hali hiyo, alisema serikali haiwezi kukaa hivi hivi, kwani hiyo ni hatari kwa uchumi wa nchi.

 “Mtafute njia ya kuangalia tunafanyaje foleni ya Dar es Salaam, sasa si kungoja, it has to be done now (inatakiwa kufanyika sasa),” alisema Lowassa.
MBUNGE AMUUNGA MKONO
Mbunge wa Pangani (CCM), Saleh Pamba, akichangia mjadala huo, alimuunga mkono Lowassa, kwa kusema urasimu uliomo serikalini ni wa kuchukua maamuzi na kusema kwa mwenendo huo kamwe nchi haiwezi kuendelea.  Alisema Malaysia wamefanikiwa na kupiga hatua katika maendeleo kwa sababu kuu moja tu ya kuchukua maamuzi kwa haraka.
 
CHANZO: NIPASHE