Saturday, 2 November 2013

Membe: Hatutaathirika kujitoa Afrika Mashariki

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye ametoa kauli kuwa Tanzania haitaathirika kujitoa katika Jumuiya nchi za Afrika Mashariki 
Na Elias Msuya, Mwananchi

Posted  Novemba2  2013  saa 8:50 AM
Kwa ufupi
Mpasuko wa jumuiya hiyo umejidhihirisha siku za karibuni baada ya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kufanya mikutano na kuafikiana kwa mambo kadhaa, huku nchi za Tanzania na Burundi zikitengwa.


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema Tanzania iko tayari kujitoa Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani kuna kila dalili ya kutengwa.
Mpasuko wa jumuiya hiyo umejidhihirisha siku za karibuni baada ya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda kufanya mikutano na kuafikiana kwa mambo kadhaa, huku nchi za Tanzania na Burundi zikitengwa.
Akijibu maswali ya Wabunge hivi karibuni Bungeni mjini Dodoma, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alisema bado Tanzania inatafakari mwenendo huo na inasubiri mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje la Jumuiya hiyo wiki mbili zijazo ili itoe msimamo wake.
Hata hivyo akizungumza na kituo cha Channel Ten juzi jijini Dar es Salaam, Waziri Membe alisema Tanzania iko tayari kujitoa na haitapata hasara yoyote.
“Iko wazi tu kwamba tumeshatengwa na wenzetu...inaweza kuwa sababu pengine tumepeleka majeshi yetu Mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasiamya Congo kuwachakaza, au pengine inawezeka kuna mtu anataka awe kiongozi  (Rais) wa Afrika Mashariki na wengine tukakataa mpango huo.”
“Sisi hatutakubali kuburuzwa,” alisema Membe.

SOURCE: MWANANCHI