Saturday, 2 November 2013

Wasomi wadai mabadiliko mitihani ya sekondari ni siasa tu


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Juhudi wilayani Ilala jijini Dar es Salaam wakijisomea nje ya viwanja vya shule yao. PICHA | MAKTABA 
Na Fredy Azzah, Mwananchi

Posted  Novemba2  2013  saa 8:34 AM
Kwa ufupi
Baadhi ya wadau hao wakizungumza na gazeti hili jana, walisema Tanzania imeweka rekodi kwa nchi za Afrika kwa kuwa na kiwango kidogo sana cha ufaulu cha alama F kuanzia 0 mpaka 19.

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Serikali kutangaza kupunguza viwango vya ufaulu kwa mtihani ya kidato cha nne na sita, baadhi ya wasomi na wadau wa elimu wameponda uamuzi huo na kusema una malengo ya kisiasa.
Baadhi ya wadau hao wakizungumza na gazeti hili jana, walisema Tanzania imeweka rekodi kwa nchi za Afrika kwa kuwa na kiwango kidogo sana cha ufaulu cha alama F kuanzia 0 mpaka 19.
Walisema, Serikali imechukua uamuzi huo kisiasa ili kuhakikisha kuwa, wanatimiza lengo la Mpango wa Maendeleo Makubwa Sasa (BRN), ambalo ni kuhakikisha matokeo ya ufaulu kwa Mtihani wa Kidato cha Nne mwaka huu yanafikia asilimia 60 kutoka 33 ya mwaka jana.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Herme Mosha alisema kuwa kilichofanywa na Serikali ni kupanua wigo wa watu kufaulu.
“Wanataka watu ambao walikuwa wanapata daraja la nne wapate daraja la tatu, daraja la tatu wapate la pili na la pili wapate la kwanza.
Hata hivyo, kwa muda wote, wadau wa elimu ambao wanataka siyo kuona tu watu wanafaulu, wanataka elimu iliyo bora. Kwa hatua hii waliyoichukua haitasaidia lolote katika kuongeza ubora wa elimu ambao umekuwa kilio cha muda mrefu,” alisema Profesa Mosha.
Alisema kuwa, washikadau wengi wangependa kuona ubora wa elimu umeongezeka na siyo kuongeza wigo wa ufaulu.
“Huku ni kujidanganya, jambo la kwanza wangetakiwa waende katika shule mbalimbali waone ni nini walimu wanataka, tatizo lipo wapi halafu wachukue hatua kwa sababu ukiangalia sasa ni kama kuna mgomo fulani hivi,” alisema.
Kwa upande wake Dk Kitila Mkumbo ambaye ni Mkuu wa Idara ya Saikolojia ya Elimu na Masomo ya Mitalaa ya Shule Kuu ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema tatizo la elimu Tanzania halijawahi kuwa ni viwango vya ufaulu.
“Wanataka tu kuona hiyo asilimia 60 waliyojipangia inafikiwa. Walijiwekea lengo hilo wakijua kabisa kwenye elimu hakuna miujiza, lazima mtu ufanye kazi ndiyo matokeo yaonekane,” alisema.
Alisema kiwango cha kufeli kilichowekwa kinaifanya Tanzania kuwa nchi yenye viwango vidogo sana vya elimu kwenye bara hili.
“Burundi wenyewe mtoto akipata 50 ndiyo anakuwa amefeli, sisi huku tumeweka mpaka 19 ndiyo tunasema amepata hiyo F, lakini bado tunaita amefaulu, huu ni utani,” alisema.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekia Oluoch alisema Matumizi ya Alama za Maendeleo ya Mwanafunzi (CA) ni suala la kupongeza.
Hata hivyo, alisema kuwa kuna matatizo ya msingi kwenye elimu na ni lazima yafanyiwe kazi.
“Lengo lao la kushusha ufaulu ni ili ionekane kuwa BRN imefikia lengo, watoto wamefaulu ndiyo iwe furaha yao,” alisema.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), Mahmoud Mringo alisema wamepokea suala hilo kwa mikono miwili.
“Zamani mtu alikuwa amapata sifuri na mwingine 33 wote tunasema wamepata F, lakini sasa kuna utofauti kwa hiyo unaweza kuona ni namna gani uwatumie hawa watu.
Pia suala hili linatoa mwanya mpana hata kwa Serikali na taasisi nyingine za elimu, ikitokea kwamba watu wa C wamekosekana unaweza kuona sasa tutumie wapi,” alisema.
Alisema kuwa, kwa sasa sera ya elimu inasema watu watakaoingia kidato cha tano wanatakiwa wawe na C tatu, lakini mwaka huu Serikali ilichukua C moja na D mbili wakaenda kidato cha tano.
“Yote hii ni kwa sababu hakukuwa na njia mbadala, lakini kwa sasa kutakuwa na mianya mingi sana.
Hata hivyo, tujue kuwa, tatizo la elimu Tanzania halikuwa madaraja, hii ilikuwa ni sehemu tu, lazima tuhakikishe tunatafuta matatizo ya msingi ya elimu yetu tuyafanyie kazi. Tukibaki kwenye hizi alama, basi nchi yetu itakwenda shimoni,” alisema.


SOURCE: MWANANCHI