Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Posted Alhamisi,Novemba7 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Novemba7 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni katika maeneo ya Ubungo Maziwa akiwa ndani ya gari karibu na duka walilopora.
Dar es Salaam.Dereva wa Shirika
la Utangazaji Tanzania(TBC), Ramadhani Gize ameuawa kwa kupigwa risasi
na watu wanaosadikiwa kuwa ni majambazi katika maeneo ya Ubungo jijini
Dar es Salaam akiwa njiani kwenda kuchukua wafanyakazi kuwapeleka
kazini.
Ramadhani alipigwa risasi wakati akienda nyumbani kwa mtangazaji wa kituo hicho,Shaaban Kisu aliyekuwa zamu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni,Camillus
Wambura alisema tukio hilo lilitokea saa 3:45 juzi usiku baada ya
majambazi manne wakiwa na silaha kuvamia duka la Namanga
Shopping lililopo Ubungo na kumlazimisha mmiliki wa duka hilo, Amdan Rajab kutoa fedha.
Alisema majambazi hao walipora fedha kiasi ambacho
hakikufahamika pamoja na vocha za mitandao mbalimbali ya simu zenye
thamani ya Sh400,000.
“Wakati tukio likiendelea,Mwagize alikuwa amepaki
gari karibu na duka hilo na alipokuwa akitaka kuondoka mmoja wa
majambazi alimfyatulia risasi zilizompata kichwani na alipoteza maisha
akiwa njiani kuwahishwa hospitali,” alisema Kamanda Wambura.
Alisema wakati majambazi hayo yakifanya tukio hilo
waliliona gari la TBC likiwa eneo hilo na inawezekana walihofia kupigwa
picha ndipo walichukua uamuzi huo wa kupiga risasi kioo cha mbele cha
gari hilo na kumpata kwenye kichwa dereva huyo,” alisema Wambura.
Alisema risasi hizo pia zilimpata na kumjeruhi mtu
mwingine,Mharami Rajabu (25) aliyekuwa anataka kuegesha gari lake
karibu na eneo la tukio aliyewahishwa katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili anakoendelea na matibabu.
Kamanda Wambura alisema, polisi wanaendesha msako
mkali kuwasaka wahusika na kusisitiza wananchi kushirikiana katika
kuwafichua wahalifu.
Baba mzazi alonga
Akizungumza na Mwananchi jana nyumbani kwa
marehemu,baba mzazi wa dereva huyo, Athumani Mwagize alisema mwili wa
marehemu utasafirishwa leo kwenda kijijini kwao Mgole, wilayani Kilosa
mkoani Morogoro kwa maziko.
Naye Mkurugenzi wa TBC, Clement Mshana aliiambia
Mwananchi: “Nimeshtushwa na tukio hili lakini ninaamini polisi watafanya
kazi yao na wote waliohusika watakamatwa.”
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI