MBUNGE wa
Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), ametimuliwa katika kikao cha
ndani ya chama hicho Kanda ya Ziwa Mashariki kwa madai ya usaliti.
Uamuzi wa
kutimuliwa kwa mwanasiasa huyo ulifikiwa juzi jioni mkoani Shinyanga
wakati Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alipokutana na viongozi wa
kanda hiyo katika kikao cha ndani kwa ajili ya mikakati ya ujenzi wa
chama.
Akizungumzia
tukio hilo, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Mashariki, Silvester
Kasulumbai, alisema kuwa katika mkutano huo uliowahusisha viongozi wa
mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara, kabla ya Shibuda kutimuliwa, Mbowe
alimpa nafasi ya kutetea tuhuma zilizotolewa dhidi yake ikiwamo sababu
ya kuhudhuria majukwaa ya mikutano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Mmoja wa
wajumbe alisimama na kutoa hoja ya kuwa kikao hicho hakiwezi kuendelea
kujadili masuala ya msingi ya chama ilhali kukiwa na watu wanaotoa
taarifa kwa CCM na ghafla akamtaja mtu huyo kuwa ni Shibuda,” alisema.
Kasulumbai
aliongeza kuwa mtoa hoja alisisitiza kuwa Shibuda alipanda katika jukwaa
moja na viongozi wa CCM na kudai kuwa vyama vya upinzani havina kitu,
kwamba CCM ndicho chama tawala, hali aliyoeleza kuwa hata mikakati
itakayopangwa katika mkutano huo anaweza kuivujisha na hivyo kumtaka
Mbowe amtoe nje ya kikao hicho.
Kwa mujibu
wa Kasulumbai ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki, baada ya hoja
hiyo Mbowe aliwataka wajumbe wasiwe na jazba na wampe nafasi Shibuda ili
aweze kujitetea dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake.
Alisema
baada ya Shibuda kupewa nafasi alieleza kuwa yeye kupanda katika jukwaa
la CCM si jambo la ajabu katika masuala ya kisiasa na kutolea mfano
hatua ya wenyeviti wa vyama vitatu vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF
kukutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu huku wakijua kuwa ni mwenyekiti wa
CCM.
Kasulumbai
alisema katika utetezi wake, Shibuda alisema kwamba mtu mzima anapokuwa
na shida yoyote hukimbilia kwa baba yake na kumaainisha baba huyo ni
chama kinachotawala yaani CCM.
Aliongeza
kuwa kauli ya Shibuda iliwakasirisha wajumbe na kuwaudhi zaidi, hivyo
kuanza kumshambulia kwa maneno hali iliyomfanya Mbowe kuingilia kati na
kuwataka wajumbe kupiga kura kwa ajili ya kufikia hitimisho juu ya uwepo
wake katika kikao hicho.
“Zilipigwa
kura akapata kura 38 zilizotaka aendelee kubaki ndani, tano ziliharibika
na 90 zilitaka aondolewe katika kikao na wajumbe wakamuomba Mbowe
afanye utaratibu wa kumuondoa kwa amani,” alisema Kasulumbai.
Alipotafutwa
kwa simu jana kuzungumzia tuki hilo, Shibuda alisema wanachama na
wafuasi wa CHADEMA walimuelewa vibaya alipopanda jukwaani katika mkutano
wa CCM mjini Geita.
Alisema
wakati alipopanda jukwaani na kuonana na viongozi wa CCM, alikuwa
akiwakilisha kilio cha wakulima wa pamba wa Kanda ya Ziwa.
“Mimi ni
mlezi wa wakulima wa pamba Kanda ya Ziwa na pale nilimfuata Katibu wa
CCM nikamueleza kuwa akamwambie mwenyekiti wake, Rais wa nchi kwamba
tunapata taabu na masilahi kidogo kwa kuwa tunanyonywa na wajanja katika
kilimo cha pamba,” alisema.
Kwa mujibu
wa Shibuda, kitendo hicho angekifanya kwa kiongozi wa chama chochote
kilicho madarakani kwa kile alichoeleza kuwa ilani ya wakati itakayokuwa
inatekelezwa ni ya chama husika.
Aliongeza
kuwa kwa nafasi yake ya mbunge anayetokana na CHADEMA hoja yoyote
atakayoipeleka serikalini na kufanikiwa zitakuwa ni juhudi za chama
badala ya watu kumfikiria kuwa msaliti.
“Kuna
waganga njaa ndio wanaendekeza mifarakano ndani ya chama na hii ipo
katika vyama vyote, wanafanya hivi si kwa sababu ya masilahi ya chama na
nchi bali kuhakikisha matumbo yao yanashiba wakati wote kwa kuendekeza
misigano isiyo na ulazima,” alisema.
Aliongeza
kuwa kama hatua ya kutaka kuwatetea wakulima wa pamba Kanda ya Ziwa ni
usaliti atakuwa tayari kuhukumiwa na kufukuzwa kwa hatua hiyo.