Wednesday 16 October 2013

Wazuiwa kumwona Ufoo, mamia wamuaga mama yake


Na  Joseph Zablon na Elizabeth Edward, Mwananchi

Posted  Jumatano,Oktoba16  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Anastazia Saro ambaye ni mama mzazi wa Mwandishi wa ITV, Ufoo Saro aliuawa kwa kupigwa risasi mwishoni mwa wiki.

Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji jana walimiminika Kibamba nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam kwa ajili ya kuaga mwili wa Anastazia Saro ambaye ni mama wa Mwandishi wa ITV, Ufoo Saro, aliyeuawa kwa kupigwa risasi mwishoni mwa wiki.
Wakati hayo yakijiri nyumbani, hali ya Mtangazaji Ufoo Saro aliyepata majeraha baada ya kupigwa risasi na mzazi mwenzake imeendelea kuimarika huku ndugu, jamaa na marafiki wakizuiwa kumwona.
Mwandishi huyo wa habari yuko kwenye uangalizi maalumu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kile kilichoelezwa kuwa anahitaji mapumziko ya saa 72 kabla ya kuanza kuonana na watu.
Akizungumza jana nyumbani kwa marehemu, Msemaji wa familia, Allelio Swai alisema shughuli za kuaga zimechelewa kutokana na taratibu za polisi na pia upasuaji ulikuwa mgumu na marehemu alitolewa risasi tano.
Mwili wa mama yake Ufoo, ulitolewa katika chumba cha kuhifadhia maiti saa 7 mchana na kupelekwa nyumbani kwake Kibamba kwa ajili ya kuagwa.
Naye fundi seremala, Leonard Kiondo alisema siku ya tukio alisikia milio ya risasi na baadaye alimwona Ufoo akiwa na shumizi ya kulalia akikimbia huku akivuja damu kabla ya kumuhifadhi na baadaye kumuwahisha hospitali kwa usafiri wa bodaboda.
Iliwachukua polisi saa moja nzima kabla ya kufika eneo la tukio. Mwili wa Anastazia ulisafirishwa jana jioni kwenda Machame, Wilaya ya Hai, Mkoa wa Kilimanjaro kwa maziko yatakayofanyika leo.
Swai alisema maziko hayo yatafanyika baada ya ibada itakayofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Uraa.
Katika hatua nyingine, ndugu, jamaa wa mzazi mwenzake Ufoo marehemu walikutana kwa mara nyingine jana kwenye Hoteli ya 92, kupanga taratibu za maziko ya ndugu yao Antery Mushi aliyejiua kwa kujipiga risasi.
Kaka wa marehemu, Andrea Mushi alisema jana kuwa wanakutana kupanga taratibu hizo kabla ya kuusafirisha mwili wa marehemu kwenda Moshi kwa mazishi yatakayofanyika kesho.
Hospitali ya Taifa Muhimbili
Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alibainisha kuwa hali ya Ufoo inaimarika ukilinganisha na mara ya kwanza alipofikishwa hospitalini hapo.

“Nimezungumza na daktari anayemshughulikia anasema maendeleo yake kiafya ni mazuri ingawa haruhusiwi mtu yeyote kwenda kumuangalia kulingana na tiba anazokabiliana nazo”alisema Aligaesha.
Hata hivyo, Aligaesha alikataa kuzungumzia ripoti ya daktari kuhusiana na idadi ya risasi zilizotolewa katika mwili wa Ufoo kwa madai kuwa hiyo ni siri ya mgonjwa.
“Sina chochote cha kusema zaidi ya anaendelea vizuri mambo mengine ni siri ya mgonjwa na daktari atakapoamua mwenyewe atawaambia lakini sina jukumu hilo.”

SOURCE: MWANANCHI