Tuesday, 5 November 2013

Lowassa: Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa hauna meno

Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa akichangia hoja kwenye mjadala wa kupitisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2014/15, mjini Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi 
Na Waandishi Wetu, Mwananchi

Posted  Jumanne,Novemba5  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Lowassa alisema sasa Tanzania imekuwa nchi ya kila mtu kulalamika, kuanzia viongozi hadi wananchi.


Dar es Salaam/Dodoma.Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amesema ana shaka kama Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Result Now), utafanikiwa kutokana na Kitengo cha Utekelezaji, Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo kilicho chini ya Ofisi ya Rais (PDB) kukosa meno.
Akichangia mjadala wa hoja ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2014/2015, Lowassa alisema tatizo kubwa linaloikabili nchi ni viongozi kushindwa kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo.
“Tatizo la nchi hii mnazungumza mambo mengi lakini hakuna utekelezaji,” alisema Lowassa wakati akichangia mjadala huo uliowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, wiki iliyopita.
Mbunge huyo wa Monduli (CCM), Lowassa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Mambo ya Nje alisema itakuwa vigumu kwa PDB kutekeleza wajibu wake wakati hakina meno ya kusimamia utekelezaji wa mipango ya Serikali.
Kitengo cha PDB kinachoongozwa na Omar Issa kiliundwa mwaka huu na kutengewa kiasi cha Sh29 bilioni na kulalamikiwa na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika wakati wa kikao cha Bunge cha Bajeti 2013/14.
Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuinua uchumi kutoka wa chini hadi kufikia wa kati ifikapo mwaka 2025.
“Nataka mjiulize maswali machache. Je, hawa PDB wana meno?” alisema Lowassa na kuongeza:
“Tunazungumza lakini mjue kuwa `discipline’ (nidhamu) ya wenzetu wa Malaysia ni tofauti na hapa kwetu. Hapa kuna uswahili mwingi wa kukaa bila kutekeleza mambo, mnaamua bila kutekeleza.” Huku akishangiliwa na baadhi ya wabunge, Lowassa aliitaka Serikali kuwa na mipango michache ambayo itakayoweza kuifuatilia kwa ukaribu na kuitekeleza. Alipendekeza kuwa ajira, elimu na kuendeleza reli kuwa vipaumbele muhimu.
“Kinatakiwa chombo ambacho kinaweza kufanya uamuzi mgumu unaotekelezeka kwelikweli. Bila kuwavika joho la kufanya uamuzi ili kuwarahisishia utekelezaji wa kazi yao na wakawa na ‘function’ itakuwa ni kazi bure. Ni uamuzi mzuri kuanzisha mpango huu lakini msipoangalia itakuwa kazi bure. Lazima wawe na meno ya kuuma mkishakubaliana mambo yafanyike.”
 Kila mtu analalamika
Lowassa alisema sasa Tanzania imekuwa nchi ya kila mtu kulalamika, kuanzia viongozi hadi wananchi.
“Wananchi na viongozi wote wanalalamika haiwezekani kukawa na jamii ya aina hii, lazima awepo mtu mmoja anayefanya uamuzi na anayechukua hatua. Bila kuchukua hatua tutaendelea kulalamikiana tu” alisema.

Mpango wa Matokeo Makubwa uliingizwa nchini kwa kurudufiwa kutoka Malaysia, ambayo ilipopata uhuru mwaka 1957 ilikuwa katika kiwango sawa na Tanzania katika maendeleo ya kiuchumi lakini sasa ina rekodi ya juu kiuchumi barani Asia. Mpango huu pia unatekelezwa Nigeria na Rwanda na umeonyesha mafanikio makubwa katika nchi hizo.
Katika kutekeleza mpango huo, Serikali imeanza na wizara sita; Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Kilimo, Chakula na Ushirika, Maji, Uchukuzi, Fedha na Nishati na Madini.
Ajira
Akizungumzia suala la elimu, Lowassa alisema: “Huwezi kuzungumza mipango bila kuzungumza ajira, kuna Watanzania wengi waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne na sita wapo mitaani na hawana ajira. Tusipoangalia watakuja kula sahani moja na sisi.”
Alisema katika mkutano wa Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) mwaka huu, walizungumzia mdororo wa uchumi kwa nchi za Ulaya na moja ya nchi hizo ambayo ni Hispania, ilieleza jinsi ilivyoweza kujinasua kwa kuweka kipaumbele cha ajira.
“Hispania walitoa mfano kuwa walikuwa na ukosefu wa ajira kwa asilimia 50, waliamua katika bajeti yao kujikita katika kuzalisha ajira. Kila mwekezaji aliyekwenda katika nchi hiyo alipewa masharti ya kuwekeza katika ajira ya vijana. Kimsingi tunatakiwa kuwa na takwimu za kujua tumezalisha ajira ngapi ndipo tutajua uchumi wetu unakua kwa kiasi gani,” alisema.
Lowassa alisema baada ya miaka mitatu nchi hiyo imetoka kuwa miongoni mwa nchi zisizo na ajira na kusisitiza kuwa mipango mingine ni migumu kutekelezeka kama nchi haitakuwa na ajira.
Alimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu kutokana na kitendo chao cha kuwapa ajira wanafunzi waliohitimu vyuo vikuu baada ya kuwapatia matrekta na mashamba.
Elimu
Lowassa alisema kuna tatizo la msingi katika elimu ya Tanzania. “Nilitegemea wahusika wangepata taarifa ya Tume ya Serikali kuchunguza kushuka kwa kiwango cha elimu ili kujua matatizo yaliyopo katika elimu na nini cha kufanya.”

Mwanzoni mwa mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliunda tume ya watu 15 kuchunguza sababu za idadi kubwa ya wanafunzi wa kidato cha nne kuvurunda katika matokeo ya mtihani huo mwaka 2012.
Tume hiyo tayari imeshakamilisha kazi na kukabidhi ripoti hiyo serikalini, lakini mpaka sasa bado haijawekwa hadharani.
“Haitoshi kumchukua mwanafunzi aliyemaliza chuo kikuu wakati akienda katika soko la ajira wakati shahada yake hamsaidii, mtu ana shahada lakini kazi hakuna.”
“... Kunatakiwa kufanyika mjadala nchi nzima kuzungumza juu ya matatizo na nini kifanyike. Nchi isipokuwa makini katika hili itaachwa katika ushindani uliopo sasa kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).”
Awafagilia Magufuli, Mwakyembe
Akizungumzia uendelezaji wa Reli ya Kati alisema pamoja na juhudi zinazofanywa na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli kujenga barabara, alisema zinaharibika kwa kasi kutokana na kuzidi kwa kiwango cha uzito wa malori.
“Reli ya Kati inatakiwa kuangaliwa kwa haraka maana malori yanayotembea katika barabara yatapungua kwa kuwa mizigo itakuwa inachukuliwa na treni,” alisema. Licha ya kusifu kazi inayofanywa na Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe Lowassa alisema foleni jijini Dar es Salaam zinashusha uzalishaji, kwani watu wengi wanatumia muda mwingi barabarani kuliko kufanya shughuli za maendeleo.
“Serikali haiwezi kukaa hivi hivi, ‘this is a disaster’ (hili ni janga), mtafute njia ya kuangalia mnafanyaje kumaliza foleni ya Dar es Salaam, jambo hili lifanyike sasa,” alisema.
Uamuzi mgumu
Lowassa alisema pia Tanzania haitakiwi kuendelea kulumbana na Uganda, Rwanda na Kenya zinazotaka kuitenga katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), badala yake ichukue uamuzi mgumu wa kushirikiana na nchi nyingine.
“Wao wameamua kuanzisha ushirikiano na Sudan Kusini, Tanzania inaweza kuanzisha ushirikiano na Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) ambako ni kuzuri zaidi na kikubwa kinachotakiwa kufanyika ni kuifufua Reli ya Kati,” alisema.

SOURCE: MWANANCHI