Na Mwandishi wetu,Mwananchi
Posted Jumanne,Novemba5 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumanne,Novemba5 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Unajua mfanyakazi wake mmoja alikuwa ndiyo kwanza
amerudi kutoka matembezi na baada ya kuingia ndani haikuchukua muda
mrefu mlango ulivunjwa,”
Dar es Salaam. Wakati Msemaji wa Taasisi ya Tiba
ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (Moi), Jumaa Almasi akisema
hali ya Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi
imeanza kuimarika, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amedai
kwamba bado hajapata fahamu.
“Hali yake inatia matumaini, ingawa bado hajapata
fahamu lakini madaktari wanaomtibu wameeleza kuwa anaendelea vizuri.
Nami nakubali kwa sababu hali aliyokuwa nayo juzi ilikuwa tofauti, kwa
kuwa najua kusoma mashine za kupumulia, inaonyesha mapigo yake
yanakwenda vizuri,” alisema Mbatia kauli ambayo inapingana na ile ya
Almasi ambaye alisema jana kuwa:
“Hali yake imeanza kuimarika ingawa bado yupo ICU,
ameanza kuzungumza ingawa kwa shida, lakini hamuwezi kumwona kwa kuwa
madaktari wameshauri kwamba anatakiwa kupumzika.”
“Tunajua kwamba Mvungi ni mtaalamu wa masuala ya
sheria, ni kiungo muhimu kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, tunashukuru
masheikh na wanazuoni waliofika kumjulia hali. Mapadri pia wamefika na
kumwombea, lakini bado tunahitaji kuendelea kumwombea zaidi,” alisema
Mbatia.
Alisema pia wanaridhishwa na hatua za kuwasaka
watuhumiwa ambazo zinafanywa na vyombo vya ulinzi, ahadi iliyotolewa na
Inspekta Jenerali wa Polisi, Said Mwema ambaye alikuwa miongoni mwa watu
waliofika kumjulia hali.
Dk Mvungi alijeruhiwa usiku wa kuamkia juzi, baada
ya kukatwa mapanga na watu wasiojulikana waliovamia nyumbani kwake
Kibamba Msakuzi, Dar es Salaam.
Asimulia mkasa
Akisimulia mkasa huo, mjukuu wa Dk Mvungi, Doris
alisema babu yake alikabiliana na watu waliovamia nyumbani kwake na
kumwumiza mmoja wao kabla ya kuzidiwa na watu hao.
Alisema jana kuwa babu yake alimjeruhi mmoja wa
watu hao usoni kwa kitu ambacho hakukitaja na kwamba hali hiyo ndiyo
iliyochochea hasira zao na kumshambulia kwa mapanga mfululizo.
“Tulisikia mlipuko nje ya nyumba kwa mbele,
tukapiga kelele na kuamka wote, ghafla mlango wetu ukavunjwa kwa tofali
tukajaribu kutoka na kumkuta babu akiwa chini sebuleni,” alisema Doris
na kuongeza kuwa watu hao waliwaamuru kulala chini.
Alisema akiwa amelala chini alisikia mmoja wa watu
hao akidai kuwa ameumizwa usoni kauli ambayo ilifuatiwa na mashambulizi
mfululizo kwa Dk Mvungi na kisha wakamvutia jikoni huku wakiendelea
kumshambulia.
Doris alisema majambazi hao walikuwa watatu na
hawakuwa wamejifunika nyuso huku mmoja akiwa amevaa kofia na kwamba
laiti kungekuwa na mwanga chumbani wangewatambua. Alisema watu wengine
wawili walibaki nje na walipiga baruti mbele ya nyumba.
SOURCE: MWANANCHI
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Salome Emmanuel alisema Dk Mvungi
alivamiwa nyumbani kwake na watu ambao anadhani walikuwa wakifuatilia
nyendo za mmoja wa wafanyakazi wake.
“Unajua mfanyakazi wake mmoja alikuwa ndiyo kwanza
amerudi kutoka matembezi na baada ya kuingia ndani haikuchukua muda
mrefu mlango ulivunjwa,” alisema Salome ambaye ni mke wa dereva wa Dk
Mvungi.
Salome ambaye wanaishi na mumewe jirani na Dk
Mvungi, alisema baada ya milipuko inayodhaniwa kuwa ni baruti, alisikia
kelele na kuona mwanga wa tochi kali ndani ya nyumba hiyo na ndipo
alipomwamsha mumewe na kuanza kuhangaika kutafuta namba za simu za
polisi.
Salome alisema wahalifu hao walionekana kuwa na
ufahamu mkubwa wa jiografia ya eneo hilo kwani walipita uani ambako
hakuna mwanga wa umeme na kuingia nyumbani kwa Dk Mvungi na hata
walipoondoka walipita jirani na kwao na muda mfupi baadaye walisikia
mngurumo wa pikipiki.
Polisi wakamata watano wakiwa na gongo
Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imesema
inawashikilia watu sita wakituhumiwa kuhusika na tukio la kumshambulia
kwa mapanga Dk Mvungi.
Kamanda wa Kanda hiyo, Kamishna Suleiman Kova
alisema watuhumiwa, ambao aligoma kutaja majina yao walikamatwa wakiwa
na pombe aina ya gongo lita 17 na kete 15 bangi. Baada ya kuvamiwa, Dk
Mvungi aliporwa bastola na kompyuta.
Kamanda Kova alisema baada ya msako mkali wa
polisi kwa kushirikiana na raia wema waliwakamata watuhumiwa hao wakiwa
karibu na eneo la tukio.
Misa
Kutokana na tukio hilo Mbatia alisema leo saa 10
jioni kutakuwa na misa maalumu ya kumwombea Dk Mvungi, ambaye pia ni
Mkurugenzi wa Katiba, Sheria na Haki za Binadamu wa NCCR-Mageuzi. Misa
hiyo inatarajiwa kufanyika katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Dar es
Salaam.
SOURCE: MWANANCHI