Wednesday, 23 October 2013

Makosa wayafanyayo wamiliki wa wavuti na jinsi ya kuyaepuka

Mtumiaji wa Kompyuta akisoma taarifa katika wavuti wa gazeti la Mwananchi ambao ni kati ya wavuti iliyotengenezwa kitaalamu na wamiliki wake.Picha na Fidelis  Felix 


Posted  Jumanne,Oktoba22  2013  saa 12:48 PM
Kwa ufupi
Maendeleo ya Tehama yamefanya gharama za kutengeneza na kumiliki wavuti kushuka, huku watengenezaji wake wakiwa karibu na wateja.


Katika dunia ya leo, watu hususan wafanyabiashara kuwa na wavuti (website) sio jambo la anasa wala la hiari. Kwa walio makini wavuti ni jambo la lazima.
Maendeleo ya Tehama yamefanya gharama za kutengeneza na kumiliki wavuti kushuka, huku watengenezaji wake wakiwa karibu na wateja.
Kila kona katika miji yetu wapo wataalamu wanaoweza kutengeneza wavuti, achilia mbali kampuni za Tehama kama vile Wordpress na Blogspot zinazowawezesha watumiaji wake kuwa na wavuti bila ya kulipia gharama yoyote.
Hata hivyo, kumiliki wavuti sio mwisho wa safari. Wamiliki wengi wana wavuti, lakini hazifanyi kazi kwa kuwa zimelala usingizi mnono. Kwa wenye biashara wavuti ni sehemu ya kujitangaza na pia njia mojawapo ya kuwasiliana na wateja.
Makala haya yanakusudia kuainisha makosa kadhaa yafanywayo na wamiliki wa wavuti na namna ya kuyaepuka kwa minajili ya kuupa mafanikio wavuti wako.
Kukosa mwelekeo
Japo wavuti katika dunia ya sasa, ni sehemu ya biashara, wamiliki wengi hapa nchini hawajui nini kifuate baada ya kuwa na wavuti. Wengi huishia kwenye hatua ya kuwa na wavuti pekee.
Hivi umejiuliza kwa nini uliamua kuwa na wavuti? Haingii akilini kama jibu lako litakuwa ulifanya hivyo ili tu nawe uonekane.
Ili uweze kuona matunda ya wavuti, lazima ujue lengo na mwelekeo wako. Kwa wenye biashara, mwelekeo huo lazima uende sambamba na biashara husika. Kwa mtazamo wangu sioni tija ya kuwa na wavuti kama mtu hatojali maslahi hasa yale ya kibiashara.
Kutokutumia takwimu
Takwimu ni mojawapo ya vitu muhimu kwenye wavuti wowote. Hata hivyo, wengi hawajui umuhimu wake achilia mbali namna ya kuzitumia.
Swali muhimu, kama hujui idadi ya watembeleaji wa wavuti wako, wanafanya nini wakiwa huko au wanapendelea kurasa zipi za wavuti; utawezaje kupima uwezo wa wavuti uliouanzisha?

Kimsingi, takwimu hutoa picha halisi ya matumizi ya watembeleaji wa wavuti wako. Aidha takwimu zitakujulisha tabia za wateja wako, kurasa wanazopendelea, mahala walipo na hata muda wanaopenda kufungua wavuti wako.
Angalia mfano huu. Unamiliki wavuti kuhusu mgahawa uliopo Arusha, lakini kwa kutumia takwimu unabaini asilimia kubwa ya watembeleaji wanapatikana mkoani Dar es Salaam. Kwa mfanyabishara makini hii ni taarifa ya kuifanyia kazi kwa maendeleo ya mgahawa.
Ili kutatua tatizo hili, unashauriwa kutumia programu za takwimu, huku ukitafuta wataalamu wanaoweza kukutafsiria maana ya takwimu hizo kwenye lugha ya kibiashara zaidi.
Katika wavuti nyingi hivi leo,wahusika wameweka takwimu kuhusu watembeleaji pekee. Idadi pekee haitoshi kwani kuna mengi yanayopaswa kujulikana ili hatimaye yaweze kufungamanishwa na bishara na hata uwekezaji kwenye Tehama.
Kukosekana sehemu ya kutafuta taarifa
Kwa wavuti kubwa zilizo na vitu vingi au kufanyiwa mabadiliko ya mara kwa mara, sehemu ya kutafuta taarifa (search button) ni lazima.
Sehemu hii sio tu itasaidia kuokoa muda wa watembeleaji wa wavuti ambao hawana muda wa kuanza kujaribu kurasa moja hadi nyingine, lakini pia utasaidia kuongeza muingiliano kati ya wavuti na watembeleaji.
Cha muhimu hakikisha unakuwa na sehemu ya kutafuta taarifa kwenye wavuti wako. Pia hakikisha unaunganisa kitafuto hiki na mitambo ya takwimu, ili kukupa picha halisi ya vitu gani ambavyo watu wanavitafuta kwa kiasi kikubwa kwenye wavuti.
Zingatia mfano ufuatao; Una wavuti kuhusu saluni ya kinamama, ukiwa na sehemu ya kutafuta taarifa na kisha takwimu zikaonyesha watu wengi wanatafuta bidhaa X, taarifa hiyo itakuwezesha kuboresha mpango wa biashara yako.
Kurasa zisizoweza kutambazika
Kimsingi watu wengi wanapotafuta taarifa kwenye wavuti, hawasomi bali wanatambaza (scan) na huondoka mara wanapokosa taarifa husika. Hapa kuna kosa linalofanywa na wamiliki wa wavuti hasa Tanzania.
Wamiliki wengi wanashindwa kutoa picha ya website yao kwa jicho la kwanza. Wavuti na blogu nyingi za Tanzania zimejaa vitu vingi kiasi msomaji anashindwa aanzie wapi.

Ilivyo hutakiwi kuandika maneno milioni moja ili kumfanya mtu atumie wavuti wako. Watembeleaji hawana muda wa kuanza kudokoa kitu kimoja kimoja. Wengi wanadhani, kuwa na makala nyingi ndio kufanikiwa. Andaa taarifa inayojitosheleza katika njia nyepesi na rafiki zaidi.
Kukipa kisogo Kiswahili
Inasikitisha kuona wamiliki wengi wakitumia lugha ya Kiingereza kwenye wavuti zao ambazo kimsingi wateja wao wakubwa ni watumiaji wa lugha adhimu ya Kiswahili.
Inawezekana matumizi ya Kiingereza yakawa mujarabu zaidi ikiwa biashara husika ni ya kimataifa, lakini kama biashara ama taarifa inahusu zaidi Watanzania ambao wengi wanatumia Kiswahili, hakuna haja ya kutumia lugha ngeni.
Matumizi ya lugha ipi inafaa kwenye wavuti yategemee vitu kama vile lengo na mwelekeo wa wavuti na nani unawalenga. Ukijiuliza haya utakuwa na nafasi nzuri ya kuchagua lugha ya kutumia katika wavuti wako.
Wapo wanaotumia lugha zaidi ya moja kufikisha taarifa kwenye wavuti zao. Ni jambo la kupongeza na la kuigwa.
Mkata Nyoni ni mtaalamu wa Menejimenti ya Teknolojia ya Habari na Mshauri wa Biashara.

Anapatikana kupitia barua pepe: mnyoni@dudumizi.com
 SOURCE: MWANANCHI