Na Goodluck Eliona na Beatrice Moses, Mwananchi
Posted Oktoba26 2013 saa 10:4 AM
Posted Oktoba26 2013 saa 10:4 AM
Kwa ufupi
Ni kwa kuishawishi kamati ya kudumu ya Bunge kutumia hekima kuepusha mzozo wa kisheria.
Dar es Salaam. Msajili wa Vyama vya Siasa
amevinusuru vyama hivyo, kuendelea kunyimwa ruzuku baada ya kuishawishi
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kutumia hekima
ili kuepusha mzozo wa kisheria kutokana na uamuzi wa awali.
Katika taarifa yake, msajili huyo, Jaji Francis
Mutungi, alisema kwa mujibu wa sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya
mwaka 1992, utaratibu wa ukaguzi wa mahesabu ya vyama ulikuwa kwa vyama
kuweka wakaguzi wake binafsi. Alifafanua kuwa mabadiliko ya sheria hiyo
ya mwaka 2009 yaliweka himizo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kufanya
ukaguzi huo.
“Mabadiliko hayo kutoka kwa wakaguzi binafsi
kuhamishiwa kwa CAG kimsingi yameibua mgogoro na tafsiri ambayo pengine,
kwa hakika ndiyo imechangia kuwepo kwa sintofahamu kwamba nani alipe
gharama hizo za ukaguzi kati ya vyama na CAG.
“Kutokana na hali hii naomba basi hekima ya PAC
kwa maana hiyo, Bunge kutambua kwamba ofisi ya msajili wa vyama vya
siasa ikisitisha ruzuku kwa mujibu wa kifungu 18 (3) , kama
nilivyobahinisha wakati wa mparaganyiko nilioutaja, haukutokana na
utashi au ukaidi wa vyama, tukifanya hivyo tutakuwa tunakiuka
sheria,”alisema Jaji Mutungi.
Awali akizungumza na waandishi wa habari mara
baada ya kukutana na Msajili wa vyama, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Deo
Filikunjombe, alisema kusimamishwa kwa ruzuku kunatokana na matakwa ya
kisheria.
“Tusiporidhika kama kuna chama kinavunja sheria tuna mamlaka hayo ya kusimamisha ruzuku,” alisema Filikunjombe.
Pia alibainisha kuwa Bunge nalo lina deni la
kukuza na kujenga demokrasia na uwezo wa vyama vya siasa hivyo kusitisha
ruzuku kwa wakati huu, kutaigubika nchi katika lawama za ukiukwaji wa
utawala bora na demokrasia.
“Tumemwomba CAG akamilishe ukaguzi wa vyama vyote
tisa ndani ya miezi mitatu, hesabu alizopewa azikague na wale waliosema
zipo tayari ofisini kwao wampelekee azipitie. ” alisema .
Alivitaja vyama ambavyo viliwasilisha mahesabu yao kwa CAG kuwa ni CUF, CCM, TLP na NCCR-Mageuzi.
Alisema vyama vya CUF, NCCR Mageuzi na CCM
viliwasilisha mahesabu ya mwaka 2010/2011 na TLP iliwasilisha mahesabu
ya mwaka 2010/2011 na 2011/2012.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI