* Uhamiaji yawagawia vibali kinyemela
* Wizi mifugo ya wazawa wakithiri, mazingira yaharibiwa
Wakati
Serikali kupitia kwa Mkuu wa Operesheni Kimbunga, Simon Sirro,
ikijigamba kufanikiwa katika kazi ya kuwakamata wahamiaji haramu na
kuwarudisha kwao, JAMHURI imebaini kuwa
wahamiaji wengi wanaishi na mifugo yao katika Pori la Akiba la Kimisi,
Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, huku wakikingiwa kifua na baadhi ya
vigogo wa Idara ya Mifugo, na Uhamiaji wilayani hapa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili tangu operesheni hiyo ilipoanza,
umebaini kuwa baadhi ya vigogo wa idara hizo waliigeuza kazi hiyo kuwa
mradi wa kujineemesha kinyume cha lengo lililokusudiwa na Serikali, hali
ambayo imesababisha kuwapo kwa migogoro isiyoisha baina ya wenyeji wa
eneo hilo na wahamiaji haramu.
Migogoro
hiyo ambayo chanzo chake ni baadhi ya vigogo wa Idara ya Uhamiaji
kuwagawia kama njugu wahamiaji haramu vibali vya kuishi nchini kwa muda,
ambao kwa kiburi cha vibali hivyo wameamua kuvamia na kujenga katika
maeneo ya wazi yaliyotengwa na Serikali za Vijiji husika kwa ajili ya
shughuli za maendeleo ya umma.
Hali
hiyo imesababisha viongozi wa vijiji husika kuishi kama wakimbizi, huku
wakihofia kuuawa kwa kinachoelezwa kuwa Serikali wilayani Ngara imeziba
masikio.
Tukio
la hivi karibuni, ambalo linadaiwa kuchochewa na baadhi ya vigogo wa
idara za Uhamiaji, na Mifugo waliowekwa mfukoni na kufanya watakavyo
kinyume cha taratibu za nchi, ni la wafugaji wawili kuuawa kinyama kwa
kukatwa kwa panga na kuchomwa mikuki na wananchi. Pia ng’ombe 12
waliuawa katika tukio hilo kijijini Kasulo.
Chanzo
cha mauaji hayo kimeelezwa kuwa ni uhasama wa muda mrefu kati ya
wananchi na wafugaji hao, wanaodaiwa kuingiza mifugo kijijini hapo bila
ridhaa ya Serikali ya Kijiji, bali kwa mgongo wa vigogo wa idara za
Uhamiaji, na Mifugo.
Waliouawa
kwenye tukio hilo lililotokea Septemba 19, mwaka huu, saa 11:00 jioni
ni Ngabo Godfrey (24) na mwingine ambaye hakutambulika mara moja na
kwamba ng’ombe waliouawa kwa kuchomwa mikuki na kukatwa mapanga, nyama
zao zilichukuliwa na wananchi hao kwa ajili ya kitoweo.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngoma B, kijijini Kasulo, lilipotokea tukio hilo, Simon Nzakaya, aliieleza JAMHURI
kuwa miili ya wafugaji hao ilipatikana siku moja baada ya mauaji na
tayari watu wanane waliokuwa wakishikiliwa na vyombo vya dola kwa
mahojiano zaidi.
Hata
hivyo, baadhi ya watu walizitupia lawama baadhi ya mamlaka za Serikali
zikiwamo Idara ya Uhamiaji, Mifugo na Halmashauri ya Wilaya kupitia
Kitengo cha Sheria, kwa kushindwa kuchukua hatua mapema mara baada ya
kuombwa kuingilia kati mambo ya uvamizi wa wafugaji katika eneo hilo.
“Mgogoro
huu si wa leo… wenzetu Idara ya Uhamiaji, Mifugo na Mwanasheria wetu wa
Halmashauri walishakuwa mawakala wa wafugaji na wahamiaji haramu… na
ndiyo sababu za mauaji kama haya maana wananchi wameshachoka… na
ninakueleza ndugu mwandishi huu ni mwanzo tu, iwapo Serikali
haitazinduka ikasafisha idara hizi na kuleta wazalendo, mauaji
hayatakoma maana wafugaji wanaoingia kinyemela kupitia mlango wa nyuma
ni wengi,” amesema mmoja wa wanakijiji aliyeomba kutotajwa jina
gazetini.
Gazeti
hili, mbali ya kuzungumza na baadhi ya wananchi kwenye vitongoji vya
Njiapanda na Ngoma B ilikofukuta migogoro hiyo na kuelezea kero
wanazokumbana nazo kutoka kwa wafugaji na wahamiaji haramu
inayosababishwa na kukithiri kwa rushwa, pia limefanya mahojiano na
baadhi ya viongozi wa maeneo hayo wakatoa dukuduku zao.
Brighton
Kemikimba, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Njiapanda, amesema tatizo la
uingizaji wa mifugo kutoka ndani na nje ya nchi kuja kijijini hapo na
maeneo mengine ndani ya Wilaya ya Ngara, limechangiwa kwa kiasi na idara
ya Mifugo na ya Uhamiaji ambazo kwa miaka mingi zimekuwa zikiwapa
wafugaji hao vibali kinyume cha sheria.
“Idara
hizi mbili, hususan ya uhamiaji imesababisha maeneo tunayoishi kugeuzwa
kambi za kufugia mifugo ya wahamiaji… maana wamekuwa wakifika kisha
kujimilikisha maeneo ya kufugia na kuishi bila kufuata taratibu za
umilikaji wa ardhi.
“Watu
tukiwa hatuna hili wala lile tunashtukia wapo kijijini… kama viongozi
tumeshafanya vikao vya kijiji, mikutano ya hadhara ya vijijji na kutoa
maazimio hawa watu waondoke katika ardhi yetu na warudi walikotoka,
lakini cha kushangaza wamekuwa wakikimbilia Uhamiaji na kupewa ‘pamiti’
kinyemela, jambo ambalo limezidisha migogoro kila uchao na hatujui la
kufanya,” amesema Kemikimba.
Alifafanua;
“Sheria ya Ardhi Namba 5 ya mwaka 1999 ya Vijiji inatoa mamlaka kwa
Serikali ya Kijiji kuyajadili maombi ya watu wanaoomba kuhamia kijiji
husika, na mkutano wa hadhara wa kijiji ndiyo hutoa mamlaka kwa wahusika
kuishi eneo hilo, lakini hayo yote hayafanyiki, badala yake mamlaka za
kijiji zimeporwa na Uhamiaji.”
Naye
Silvester Katongale, mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Kasulo, amesema
malalamiko yao kuhusiana na Idara ya Uhamiaji kugawa vibali kwa
wahamiaji ambao wamekuwa wakivamia maeneo yao bila kufuata taratibu, ni
ya muda mrefu na kwamba hata Mkuu wa Wilaya aliyekuwapo, Luteni Kanali
Nyakonji, alijaribu kufuatilia bila mafanikio.
“Huyu
DC aliwahi kuagiza iundwe kamati ya kufanya sensa ya mifugo
iliyoingizwa kinyemela ili ijulikane idadi yao, lengo likiwa kuangalia
uwezo wa kijiji, lakini alikwama na hakuna kilichofanyika, badala yake
wahamiaji na mifugo yao wanaendelea kuingia, yaani imekuwa vurugu kubwa
kwani watu wenye asili ya Rwanda wamekuwa mbogo kana kwamba hii ni ardhi
yao.
“Wizi
wa mifugo ya wenyeji umetawala kutokana na wingi wa wafugaji wavamizi
kuingia kila kukicha na pia kumejitokeza uharibifu mkubwa wa mazingira
kwani hali ya mazingira ilivyokuwa awali na sasa ni tofauti na
inavyoonekana, wilaya imeshindwa, hivyo tunamwomba Rais Jakaya Kikwete
aingilie kati,” amesema Katongale.
Mwingine
aliyeathiriwa na wimbi la wahamiaji kuvamia na kuweka makazi kijijini
hapo kinyume cha taratibu, ni Dauda Yunusu, mjumbe wa Serikali ya Kijiji
na Mjumbe wa Kamati ya Wafugaji na Ardhi katika Kijiji cha Kasulo.
Yunusu
amesema; “Niliposikia Rais akitoa tamko la kuhakikisha wahamiaji haramu
wanakamatwa na kurejeshwa kwao nilifarijika nikijua ndiyo mwisho wa
migogoro hiyo, lakini cha ajabu zoezi [kazi] nzima lilihujumiwa na Idara
ya Uhamiaji ambayo kwa makusudi iligeuza operesheni hiyo kuwa
kitegauchumi kwa kuwagawia kinyemela wahamiaji vibali vya kuendelea
kuishi nchini bila ridhaa ya kijiji husika.
“Unavyoniona
ndugu mwandishi mimi, Brighton, na Afisa Tarafa ya Nyamiyaga, pamoja na
Serikali ya Kijiji tumeshitakiwa mahakamani na Evarist David na Medadi
Muhutu, ambaye ni asili ya Rwanda, lakini ana kibali cha kuishi nchini
na kwenye kesi hiyo namba 35/2012 tunadaiwa milioni [shilingi] 17 na
ukichunguza yote ni kwa kuwa tunapigania ardhi yetu, badala ya kuondoka
wanatuburuza mahakamani, hii ndiyo Serikali tunayoitumikia kwani hata
halmashauri imetutelekeza kupitia mwanasheria wake,” ameongeza.
Yunusu
amekwenda mbali zaidi kwa kudai kuwa usimamizi mbovu wa sheria ndiyo
chanzo cha matatizo waliyonayo, kwani pamoja na Rais Kikwete kutoa tamko
la kuwaondoa wahamiaji haramu na mifugo yao, watu wanaolisha mifugo
katika misitu ya hifadhi ukiwamo wa Kimisi hawakuondolewa, badala yake
walipatiwa vibali vya kuendelea kuishi humo.
Amedai
pia kwamba wahamiaji haramu waliokamatwa katika Msitu wa Kimisi na
ardhi ya Kasulo na kuonekana hawana vigezo vya kuishi nchini
walirudishwa nchini kwao, lakini cha kushangaza mifugo yao ilibaki
nchini pamoja na wafanyakazi wao wanaolisha mifugo.
Baadhi
ya wahamiaji haramu waliorudishwa kwao wakiacha mifugo na wafanyakazi
wao kwenye ardhi ya Tanzania katika Kijiji cha Kasulo ni Benoni
Mnyechwi, Kadugala, Katubu na watoto wa ndugu wa mzee Bulalisi
wameondoka huku mifugo yao ikiendelea kubaki yalipo makazi yao katika
Kitongoji cha Kamuri katika Kijiji cha Kasubo, jambo linaloashiria
watarudi nchini.
Ameiomba
Serikali ifanye jitihada za kunusuru hali hiyo, kutokana na ukweli kuwa
operesheni imefanyika ndivyo sivyo kinyume cha matarajio ya Rais Jakaya
Kikwete, hasa ikizingatiwa kuwa bado kuna wahamiaji wanaoishi katika
Msitu wa Hifadhi Kimisi wakiwa na mifugo yao.
“Serikali
iingilie kati hawa watu waondolewe katika Msitu wa Kimisi na waliohodhi
ardhi ya wazawa kinyemela kwa kisingizio cha kuwa na vibali walivyopata
kinyemela waachie ardhi ya watu, vinginevyo yanaweza kutokea machafuko
au mauaji kama yaliyotokea ya wafugaji na mifugo yao kuuawa kinyama.
“Na
hili si la kufanywa tena na Serikali ya Ngara maana imeshindwa
kudhibiti mianya ya rushwa, iundwe tume kuchunguza na kunusuru hali hii
maana Uhamiaji wamekuwa wakitoa vibali vinavyowaruhusu kuishi nchini kwa
muda, jambo ambalo limewafanya wananchi kukosa imani na idara hiyo,”
amesema.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kasulo, Yusuph Katula, akifafanua
utaratibu wa kuomba vibali vya kuishi nchini kwa muda, amesema kwa
kawaida mwombaji wa kibali cha kuishi eneo husika anapaswa ajadiliwe na
kijiji baada ya kupeleka maombi kwenye Halmashauri ya Kijiji na si
vinginevyo.
“Kijiji
kinapomjadili na kumkubali wanampa muhtasari wa kikao kile ili apeleke
Uhamiaji Wilaya, ambao nao hupeleka mkoani ambako hutoa ‘pamiti’ na huo
ndiyo utaratibu tofauti na sasa, kwani Uhamiaji wanatoa vibali hivyo
kama njugu na kuzidisha migogoro isiyo ya lazima kwani wahamiaji wa
kijiji chetu hawakupata vibali walivyonavyo kwa kufuata utaratibu,
wamevipata kwa njia ya panya, rushwa imetawala,” amesema.
Kutokana
na hali hiyo, viongozi waliokuwa wakiongoza zoezi hilo [Operesheni
Kimbunga] hawakuhusishwa kwenye uamuzi ili kujiridhisha na vielelezo vya
wahamiaji haramu kwa aliye halali kuishi na asiye halali, badala yake
wengi wa wahamiaji haramu waliachwa na Polisi wakishirikiana na Uhamiaji
na hata walipohoji walitishiwa maisha na hadi sasa wanaishi kwa kuhofia
usalama wao.
Akinukuu
kumbukumbu za Serkali ya kijiji, alidai kuwa Aprili 24, mwaka jana,
Serkali ya kijiji ilitoa orodha ya wafugaji wanaodaiwa kuvamia kijijini
hapo, wakiingia na maelfu ya mifugo yao wakiwataka kuondoka na kuomba
msaada kutoka mamlaka husika kwa maandishi kuwaondoa, lakini hakuna
hatua yoyote iliyochukuliwa.
Ameongeza
kuwa Desemba 12, mwaka jana, pia uongozi wa wilaya ulijulishwa kwa
taarifa ya kumtaka mfugaji mwingine kuingia kijijini hapo kwa nguvu naye
kuondoka Desemba 28, kulitolewa taarifa kama hiyo, lakini hakuna hatua
yoyote iliyochukuliwa hadi sasa.
Diwani
wa Kata ya Kasulo inayodaiwa kuongoza kwa kuathiriwa zaidi na wimbi la
ufugaji usio na tija na wahamiaji wenye vibali pamoja na wale wanaotoka
wilaya jirani na mikoa, wangeweza kudhibitiwa kama mamlaka za wilaya na
mkoa zingeweza kuingilia katika kukisaidia kijiji mapema kabla ya hali
hiyo kujitokeza.
Ameongeza
kuwa hatua ya Idara ya Uhamiaji kutoa vibali kwa wahamiaji kutoka nchi
jirani na kutumia vibali hivyo kuingiza maelfu ya mifugo katika kata
hiyo na katika hifadhi za Kimisi, Biharamulo na Burigi kumekuwa chanzo
cha mgogoro huo.
Ameongeza
kuwa ukiondoa wafugaji kutoka wilaya na mikoa jirani wanaolalamikiwa
kuingia kinyemela, wengi wanaolalamikiwa ni wahamiaji wanaoingia na
mifugo yao ama baada ya kupata vibali, au uraia na kisha kuingiza mifugo
yao bila ridhaa ya kiijiji.
Amesema
kinachoonekana ni kwa baadhi ya watumishi wa Serikali wasio waadilifu
kutanguliza zaidi maslahi yao binafsi kunakotokana na mgogoro huo badala
ya kuupatia ufumbuzi kwa maslahi ya wananchi, wilaya na Taifa.
Diwani
Kiiiza amedai kuwa suala hilo siyo siri, kila kiongozi na wananchi
wanatambua kuwa Idara ya Uhamiaji kupitia vibali inavyovitoa ndivyo
vimekuwa vinatumiwa na wahamiaji hao kama kigezo cha kuingia na maelfu
ya mifugo yao bila kuomba kuingia kijijini, wakitumia ubabe huku
kukiwapo tetesi za kukingikiwa kifua.
Katika
hatua nyingine, Idara ya Mifugo Wilaya imekuwa haichukui hatua hata
inapojulishwa juu ya kuwapo uingizwaji wa mifugo kutoka nchi jirani au
wilaya na mikoa jirani, badala ya kuchukua hatua yenyewe hubariki na
hivyo wanakijiji kupitia Serikali za kijiji kugeuka yatima.
Mkuu
wa Wilaya ya Ngara, Costantine Kanyasu, ambaye amekiri kuikuta baadhi
ya migogoro hiyo, alipohojiwa kwa njia ya simu kuhusiana na malalamiko
ya zoezi la kukamata na kuwarudisha kwao wahamiaji haramu kutawaliwa na
rushwa, amekana Uhamiaji kugeuza zoezi hilo kuwa kitegauchumi chao huku
akiahidi kufuatilia ili kubaini ukweli halisi.
Aidha,
amekiri kupokea baadhi ya malalamiko, ingawa hata hivyo, amedai
yalikuwa yakielekezwa kwa mamlaka nyingine kwa hatua na ofisi yake
kupewa nakala kutoka kijijini hapo, na sasa atakachokifanya ni kuchukua
hatua za haraka kuhakikisha tukio kama hilo halitokei tena.
Kanyasu
aliyehamia wilayani hapa hivi karibuni, amekiri kuwapo kwa baathi ya
changamoto zinazotolewa na wananchi, lakini zikiwamo za baadhi ya
mamlaka kulalamikiwa kutowajibika juu ya tukio la mauaji. Uchunguzi wake
unaendelelea.
SOURCE: JAMHURI MEDIA
|