Na Aidan Mhando, Mwananchi
Posted Ijumaa,Oktoba18 2013 saa 24:0 AM
Posted Ijumaa,Oktoba18 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Dk Bilal alikuwa mgeni rasmi katika shughuli ya
kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 851, kwenye eneo la Bunju ‘B’
Kinondoni, Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Dk John
Magufuli ametoa mwezi mmoja kwa watumishi wa Serikali ambao wanadaiwa
mikopo ya nyumba kulipa madeni yao mara moja na kuonya kwamba ikiwa
watashindwa kulipa, watanyang’anywa nyumba hizo na watakopeshwa watu
wengine.
Dk Magufuli ameibuka na hoja hiyo mpya, zikiwa ni
siku chache tangu alipopigwa ‘stop’ na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
kutekeleza sheria ya kuondoa msamaha wa asilimia tano kwa mizigo
inayozidi kwenye malori, hali ambayo ilizusha mvutano mkubwa baina ya
Serikali na wasafirishaji wa mizigo nchini.
Akizungumza wakati wa kuweka jiwe la msingi
kuzindua ujenzi wa nyumba 851 za watumishi wa Serikali eneo la
Mabwepande jijini Dar es Salaam, Dk Magufuli alisema watumishi 2500
hawajalipa mikopo ya nyumba walizonunua.
Dk Magufuli alionya kuwa atafuatilia suala hilo na
kuhakikisha madeni hayo yanalipwa mara moja, huku akimwomba Makamu wa
Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kumuunga mkono kwenye jambo hilo, ambalo
ni utekelezaji wa sheria za nchi.
“Naomba ifahamike kwamba tunapojenga nyumba kwa
ajili ya kuwakopesha watumishi wa umma tunataka kuboresha makazi yao.
Pia fedha tunazokusanya zinasaidia kujenga nyumba zaidi,” alisema Dk
Magufuli. Hata hivyo alisema hadi sasa watumishi wa Serikali 4,900 ambao
walikopa nyumba hizo tayari wamelipa madeni.
“Mimi nafanya kazi kwa kufuata sheria na kila
mtumishi wa Serikali anafahamu jambo hilo, hivyo watu ambao wanajua
tunawadai wakae kwa tahadhari, kwani ndani ya mwezi mmoja kama
hawatalipa tutawachukulia hatua bila kupuuzia,” alionya Magufuli.
Hii siyo mara ya kwanza kwa Dk Magufuli kutangaza
kunyang’anya nyumba hizo, kwani alifanya hivyo mwishoni mwa Machi mwaka
jana pale alipouagiza uongozi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA),
kuwapa siku saba watu wote walionunua nyumba hizo kulipa madeni yao.
Dk Magufuli aliwataka TBA kutoa ilani ya maandishi
inayowataka wahusika walipe fedha hizo ndani ya wiki moja vinginevyo
wangenyang’anywa kwa maelezo kwamba wanachelewesha malengo ya TBA
kujenga nyumba zaidi. Hata hivyo, hakuna taarifa zozote zilizowahi
kutolewa kuhusu kutekelezwa kwa amri hiyo iliyotolewa zaidi ya miezi 18
iliyopita.
Jana, Makamu wa Rais, Dk Bilal alimuunga mkono
Magufuli akisema: “Naunga mkono tamko la Waziri wa Ujenzi kwamba ni
lazima watumishi wa Serikali ambao wanakopeshwa nyumba walipe haraka ili
fedha hizo zisaidie kujenga nyumba nyingine.”
Dk Bilal alikuwa mgeni rasmi katika shughuli ya
kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa nyumba 851, kwenye eneo la Bunju ‘B’
Kinondoni, Dar es Salaam. Ofisa Mtendaji Mkuu wa TBA, Elius Mwakalinga,
alisema ujenzi huo unafanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza
iligharimu Sh2 bilioni na awamu ya pili Sh1 bilioni.
“Nyumba 851 zinazojengwa Bunju B ni sehemu ya
ujenzi wa nyumba 4,400 katika Mkoa wa Dar es Salaam na nyumba 10,000 kwa
nchi nzima,” alisema Mwakalinga.
Hafla hiyo ilisimama takriban kwa dakika 10 wakati
Dk Bilal akitaka kuhutubia baada ya jenereta kushindwa kufanya kazi,
hivyo kumlazimu kurudi kuketi kwenye kiti hadi umeme uliporejea. Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Jordan Rugimbana alilazimika kwenda kufuatilia
suala hilo na mafundi waliokuwapo walifanikiwa kuunganisha mashine za
kipaza sauti na umeme wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), hivyo
Makamu wa Rais aliendelea kuhutubia.
SOURCE: MWANANCHI
Uuzaji wa nyumba
Nyumba nyingi za Serikali zilijengwa kipindi cha
utawala wa ukoloni wa Wajerumani uliodumu kati ya 1885 na 1919 na ule wa
Waingereza ulioanza 1919 hadi 1961.
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa nyumba za
Serikali zilizouzwa nchi nzima tangu mwaka 2002 wakati wa uongozi wa
awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa ni zaidi ya 6,000. Malengo ya
kuuza nyumba ni kwamba, fedha zilizopatikana zingetumika kujenga nyumba
nyingine kwa ajili ya watumishi wa Serikali katika maeneo mbalimbali
nchini yakiwamo Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza.
Hata hivyo, uuzaji huo ulikuwa na utata hali
iliyosababisha kupingwa vikali na watu wa kada mbalimbali wakiwamo
wanasiasa na wanaharakati, kwa maelezo kwamba uliwanufaisha vigogo.
Malalamiko pia yalijengwa kwenye hoja kwamba
nyumba hizo ziliuzwa kwa bei ndogo ambayo haikuzingatia thamani ya ardhi
husika, huku wengine wakisema hakukuwa na umakini kwani viongozi wengi
walikosa makazi na hasa wale walioteuliwa baada ya Rais Jakaya Kikwete
kuingia madarakani.
Miongoni mwa walionunua nyumba hizo ni mawaziri
wengi, kama si wote, wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu, hasa katika
mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma, kwa kuwa walikuwa wakiishi katika
nyumba hizo.
Hali hiyo ilisababisha viongozi mbalimbali
wakiwamo mawaziri, majaji, wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi
wa ngazi mbalimbali na viongozi wengine kukaa hotelini na kuisababishia
Serikali gharama kubwa.
Tatizo lingine lililoibuka ni kuwa baadhi ya
nyumba zilizouzwa zilikuwa ndani ya maeneo ya jeshi na hasa Polisi,
hivyo kuilazimisha Serikali ya awamu ya nne ilipoingia madarakani
kulazimisha kurejesha baadhi ya nyumba hizo.
Hata hivyo, kulikuwa na ugumu katika urejeshaji
kwani baadhi ya waliouziwa tayari walikuwa wamezibomoa na kuanza upya
ujenzi wake na wengine walikuwa tayari wamezipangisha kwa mabalozi,
kampuni binafsi, mashirika yasiyokuwa ya kiserikali (NGOs) na nyingine
kujengewa maduka ya biashara.
SOURCE: MWANANCHI