Friday, 18 October 2013

Kesi ya Pinda kuunguruma leo


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda PICHA|MAKTABA 
Na James Magai, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Oktoba18  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi

Katika kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013, LHRC na TLS, wanadai kuwa Pinda alivunja katiba kwa kauli aliyoitoa Bungeni kuhusu polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri.

Dar es Salaam. Kesi ya Kikatiba inayomkabili Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), inaanza kuunguruma leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.
Kesi hiyo ilifunguliwa kwa ushirikiano wa Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).
Katika kesi hiyo namba 24 ya mwaka 2013, LHRC na TLS, wanadai kuwa Pinda alivunja katiba kwa kauli aliyoitoa Bungeni kuhusu polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri.
Walalamikaji hao wanadai kuwa kauli hiyo ni amri kwa vyombo vya dola kutekeleza sheria ya kuwapiga wananchi, wakati wa vurugu.
Hata hivyo Pinda na AG katika majibu yao, wamewasilisha pingamizi la awaliambalo pamoja na mambo mengine wanadai kuwa walalamikaji na watu waliorodheshwa katika kesi hiyo, hawana mamlaka kisheria kufungua kesi hiyo.
Pingamizi hilo limepangwa kusikilizwa leo na jopo la majaji linaloongozwa na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu.

SOURCE: MWANANCHI