Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 24:0 AM
Posted Jumanne,Oktoba22 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Dar es Salaam. Ripoti ya Tume ya Kuchunguza
Matokeo ya Kidato cha Nne iliyoundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda
mapema mwaka huu, iliibua madudu mengi ambayo hayajawekwa hadharani.
Wajumbe waliounda kamati hiyo kwa nyakati tofauti
waliliambia gazeti hili hivi karibuni kuwa waligundua mambo mengi
yanayodhihirisha udhaifu mkubwa katika uendeshaji wa sekta ya elimu
nchini.
Sehemu kubwa ya matokeo ya uchunguzi huo
inasemekana yamejikita zaidi katika kuzitupia lawama taasisi za Baraza
la Mitihani la Taifa (Necta) na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Udhaifu wa kiutendaji kati ya taasisi hizo mbili
unadaiwa umechangia kwa wanafunzi wengi kufanya vibaya kwenye mitihani
ya Kidato cha Nne mwaka jana kiasi cha kuilazimisha Serikali kuunda tume
kuchunguza tatizo kutokana na kilio kikubwa cha wadau wa elimu na
wananchi.
Viongozi watatu waandamizi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hawakupatikana kuzungumzia uchunguzi huo jana.
Simu ya Waziri wa wizara hiyo, Dk Shukuru Kawambwa haikupatikana kabisa pale ilipopigwa.
Naye Naibu wake, Philipo Mulugo alijitetea kwamba
alikuwa na shughuli nyingi na hivyo hakuwa na muda wa kuzungumzia suala
hilo wakati Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome hakupokea
kabisa simu yake.
Matokeo hayo ya mtihani wa Kidato cha Nne
uliofanyika mwaka jana yanaonyesha kuwa watahiniwa 240,903 sawa na
asilimia 60.6 walipata sifuri, huku wanafunzi 23,520 tu ambao ni sawa na
asilimia 5.16 ndiyo waliofaulu na wengine 103,327 sawa na asilimia
26.02 wakiwa wamepata daraja la nne. Katika mtihani huo, watahiniwa
397,136 walikuwa wa shule na 68,806 wa kujitegemea.
Kutokana na hali hiyo, Waziri Mkuu Pinda aliamua kuunda tume iliyoanza kufanya kazi kuanzia Machi hadi Juni mwaka huu.
Tume hiyo iliyokuwa inaongozwa na Profesa Mchome ilimkabidhi Waziri Mkuu ripoti Juni 15, mwaka huu.
Hata hivyo, ripoti hiyo haijawahi kutolewa hadharani baada ya tume kumaliza kazi yake.
Badala yake imeshuhudiwa Profesa Mchome, ambaye
alikuwa Katibu Mtendaji wa Taasisi ya Vyuo Vikuu Tanzania akipandishwa
kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Huku kwa upande mwingine, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani
(Necta), Dk Joyce Ndalichako akichukua likizo ya muda mrefu ya
mapumziko.
Madudu yaliyogunduliwa na tume
Wajumbe wa tume hiyo walisema kuwa matokeo ya
uchunguzi wao yalibaini kuwa, maswali na mitihani iliyotungwa ilikuwa ni
ile yenye kuzingatia maudhui badala ya kuzingatia kujenga maarifa na
ujuzi.
“Tulitegemea kwa vile tangu mwaka 2006, mihutasari
ya elimu ya Tanzania ilibadilika kutoka ile inayozingatia maudhui,
kwenda kwenye ile inayozingatia kujenga maarifa na ujuzi basi na mtihani
ungekuwa na mwelekeo huo,” alisema mmoja wa wajumbe wa tume ile.
Pia uchambuzi wa kamati ile uligundua kuwa
hakukuwapo mawasiliano kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Baraza
la Mitihani la Taifa (Necta).
TET, ambao ndio wasimamizi wa mitalaa ya elimu
walitakiwa kuhakiki mitihani ile baada ya kutungwa na Necta, lakini hilo
halikufanyika.
Chanzo kingine kililiambia gazeti hili kuwa tume
hiyo ilibaini katika uchunguzi wake kuwa Necta ilitumia wataalamu wasio
na juzi wa kutosha kutunga na kuhakiki mitihani.
Uchunguzi huo ulibaini baadhi ya mitihani kama ya
masomo ya Hisabati, Kemia na Fizikia ilikuwa na maswali yaliyohitaji
muda mwingi wa kuyajibu kuliko uliopangwa.
“Hii ilifanya wanafunzi kushindwa kukamilisha
kujibu maswali yote yaliyotakiwa kujibiwa kwenye mitihani hiyo. Pia
tulibaini kwamba baadhi ya maswali katika mitihani ya masomo ya Fizikia
na Kemia yalikuwa nje ya mihutasari iliyotumika kuwaandaa wanafunzi,”
aliongeza mjumbe mwingine.
Mjumbe mmoja aliongeza pia kuwa mitihani ilikuwa na misamiati migumu na hata kuwasumbua walimu walioisahihisha.
Hali hii inaweza kuwa imechangia, kwa kiasi
kikubwa, kuongeza ugumu wa mitihani hiyo na hili linaweza kuchangia
wanafunzi kushindwa kuelewa vizuri maswali wanayoulizwa kwenye mitihani.
Wajumbe wa tume hiyo walieleza hali hiyo imefanya imani kujengeka kuwa mitihani ya Tanzania ni migumu kuliko ya nchi nyingine.
Katika kuthibitisha suala la ugumu wa mitihani, Tume
ilijiridhisha kwa kuwafanyisha mitihani walimu waliochaguliwa kutoka
Tanzania Bara na Zanzibar.
“Baada ya kuwafanyisha mitihani matokeo yake
yalikuwa, asilimia 41.2 ya walimu waliotahiniwa walipata alama chini ya
asilimia 50,” kilieleza chanzo chetu.
Pia Tume ya Pinda ililaumu hali ya kukosekana kwa
utaratibu wa mrejesho kutoka shuleni kuhusu mada zilizofundishwa, uwezo
wa wanafunzi na walimu, changamoto katika ufundishaji na kujifunza,
pamoja na mambo mengine ambayo yanaweza yakafanya mtihani unaotungwa
kuwa wa haki.
Taasisi zilizotupiwa lawama ni TET, wakaguzi wa shule (Wizara) na Necta.
Tatizo lingine lililogunduliwa na tume ile ni
kukosekana kwa majadiliano kati ya Necta na wasahihishaji wa mitihani
ile kuhusiana na majibu ya mitihani ili pande hizo ziweze kuangalia
dosari zozote.
“Matatizo tuligundua kwenye masomo ya Kiswahili na
Hisabati. Wasahihishaji walitoa alama zilizostahili na hakukuwa na
utaratibu makini wa kubaini upungufu wa aina hii katika usahihishaji,”
alieleza mjumbe mmoja.
Tume hiyo inasemekana ilibaini katika somo la
hisabati kwa mfano kuna mtahiniwa aliyejibu swali ambalo halikuwepo
kwenye mtihani na kupewa alama 12.
Wajumbe wa Tume ya Pinda
Tume iliundwa na wajumbe 15, chini ya Profesa
Mchome na Makamu wake alikuwa Bernadetha Mushashu (Mbunge wa Viti
Maalumu – Kagera).
Wajumbe wengine walikuwa James Mbatia (Mbunge wa
Kuteuliwa), Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti), Profesa Mwajabu Possi
(Chuo Kikuu – UDSM), Honoratha Chitanda (CWT) na Daina Matemu (TAHOSSA)
na Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).
Wengine ni Rakhesh Rajani (Twaweza), Peter Maduki
(CSSC), Nurdin Mohamed (Bakwata), Suleiman Hemed Khamis (Baraza la
Wawakilishi), Abdalla Hemed Mohamed (Chuo Kikuu – Suza), Mabrouk Jabu
Makame (Baraza la Elimu Z’bar na Kizito Lawa (Taasisi ya Kukuza
Mitaala).
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI