Na Sharon Sauwa na Habel Chidawali, Mwananchi
Posted Oktoba26 2013 saa 9:48 AM
Posted Oktoba26 2013 saa 9:48 AM
Kwa ufupi
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Kikwete amewataka watendaji kuacha tabia ya rushwa.
Dodoma. Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya
Kikwete amesema kama rushwa haitakomeshwa ndani ya chama hicho, katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015 kitaanguka vibaya na iwapo
kitanusurika hakitapita kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amempa jukumu
la kushughulikia viongozi wa CCM wanaokula rushwa, Makamu Mwenyekiti wa
CCM, Philipo Mangula.
Rais Kikwete, alitoa onyo hilo juzi usiku,
alipokuwa akifunga mafunzo maalumu ya siku nne kwa makatibu wa mikoa,
makatibu na wenyeviti wa wilaya wa chama hicho nchini.
“Kama hatutabadilika katika suala la rushwa mwaka
2015 tutakuwa na wakati mgumu sana na kama mwaka huo tutafanikiwa
kuishika Serikali, basi mwaka 2020 hatutarudi tena madarakani.
“Najua rushwa ipo na mnaendelea kupokea shilingi
laki mbili za airtime (muda wa mawasiliano), ndugu zangu hatutafika ama
wengine watavuka na wengine kukwama,” alisema Mwenyekiti wa CCM, Rais
Kikwete.
Hii ni kauli ya kwanza nzito ya Rais Kikwete ya
hivi karibuni ya kukionya chama hicho kuhusu uimara wake wa kuendelea
kushika dola.
Aliendelea kusema kuwa tatizo la rushwa kwa
viongozi wa chama hicho linazidi kuwa kubwa kila siku, hali ambayo
inawapotezea imani wananchi ambao ndio wapiga kura wao.
“Viongozi wa chama ndio mmekuwa mawakala wa
kusambaza rushwa bila hata aibu. Nawaombeni tubadilike, kama tutaendelea
hivi hali yetu itakuwa ngumu sana katika chaguzi mbalimbali,
nawaambieni,” alisema Rais Kikwete ambaye alitumia muda wa saa mbili
kufunga mafunzo hayo.
Aliwaambia kuwa siku hizi watu wana mbadala wa vyama vingine na siyo CCM peke yao.
Aidha, Rais Kikwete alisema viongozi ambao
wanajihusisha na vitendo vya rushwa waondolewe mara moja katika nafasi
zao, ili kuwaweka watu watakaokisaidia chama kupata mafanikio.
“Tuna vijana wengi kutoka katika vyuo mbalimbali
ambao wanaweza kufanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu, hivyo hatuna
budi kuachana na hawa wala rushwa ambao watatupotezea sifa yetu kwa
wananchi.
“Tukipoteza urais ndiyo tumekwisha na chama kinaweza kufa.”
SOURCE: MWANANCHI
Aidha, aliwaonya viongozi ambao wanajihusisha na uuzaji wa mali
za chama kama vile viwanja na baadhi yao kuingia mikataba yenye utata.
“Kuna watu wanapoingia mikataba sijui wanakuwa
wamelewa...kwanza unashindwa hata kuelewa...kwa mfano utakuta mtu
alipangishwa jengo la CCM kwa miaka 264 sasa unawaza huu mkataba wa aina
gani kwa sisi tuliopo hapa, miaka 50 ijayo hakuna atakayekuwapo
duniani, sasa mmiliki wa lile jengo atakuwa nani?” alisema.
Hata hivyo, aliwataka makatibu hao na wenyeviti wa
wilaya na mikoa kuhakikisha wanawatembelea wanachama wao na kutafuta
wanachama wapya kwa ajili ya kujiimarisha kwa chaguzi mbalimbali zijazo.
“Viongozi wengi hatuna tabia ya kuwatembelea
wanachama wetu na kuwatatulia kero zao, hali ambayo inatugharimu wakati
wa uchaguzi kupata kura kidogo tofauti na idadi ya wanachama tulionao,”
alisema na kuongeza:
“Wenzenu wakiendelea kutembelea wanachama na
kuitisha mikutano, nyie mnabakia kuimba wembe ni uleule ushindi, shauri
yenu mtakatwa,” alisema.
Alisema wapinzani wana rekodi ya kufanya vizuri kwa kufanya mikutano kuliko viongozi wa CCM.
Aidha, alisema iwapo hawatafanya kazi vizuri chama
hakitaweza kufanikiwa na kuwataka kutumia maarifa waliyopata katika
mafunzo hayo kuhakikisha chama kinakuwa imara na chenye uwezo wa
kuongoza. “Lazima muendelee kuongeza wanachama siyo kupanda majukwaani
na kuimba iyena iyena...Utendaji mpya wa kuongeza wanachama ni
kuwatambua na kuwapa majukumu,” alisema.
Alisema chama hicho kina udhaifu wa kuwashawishi watu kujiandikisha katika daftari la kudumu na kwenda kupiga kura.
“Kama ni udhaifu katika chama chetu ni huu kwani
tuna wanachama, lakini wakati wa kwenda kupiga kura hatuwafuatilii ni
vyema suala hili nyie viongozi muanze nalo sasa.”
Peter Kisumu
Hivi karibuni mwanasiasa na kada mkongwe wa CCM,
Peter Kisumo naye alionya kuwa chama hicho kinaweza kuondolewa
madarakani kutokana na kunyamazia vitendo vya ufisadi na matumizi mabaya
ya rasilimali za umma vinavyotokea nchini.
Mzee Kisumo alitoa onyo hilo wiki iliyopita katika mazungumzo
maalumu aliyofanya na gazeti hili nyumbani kwake Dar es Salaam kuhusu
kumbukumbu ya Miaka 14 ya Kifo cha Mwalimu Julius Nyerere.
Alisema tatizo kubwa la chama hicho ni kwamba
kimeendelea kuwa chama dola kikikaa mbali na wananchi, huku kikishindwa
kuidhibiti rushwa na kuwawajibisha wahusika wa vitendo hivyo.
“Chama kimebaki kuwa cha walalamikaji, kila mtu
amekuwa mlalamikaji. Hata Waziri Mkuu amegeuka mlalamikaji. Sijaona watu
wanaowajibishwa kwa ufisadi,” alisema Kisumo na kuongeza:
“CCM haiwezi kujivunia ufisadi unaoonekana nchini.
Siwezi kusema imeukumbatia, lakini nasema imekuwa CCM bubu, hata
kuukemea ufisadi haiwezi. Utamaduni huu enzi za Mwalimu Nyerere
haukuwapo.”
Alisema kutokana na udhaifu huo wa CCM, kuna
uwezekano mkubwa wa chama cha upinzani, na hasa Chadema kutumia mwanya
huo kuwashawishi wananchi na kushinda uchaguzi.
Kisumo ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya
Wadhamini wa CCM, alisema ingawa Chadema haijaonyesha wazi mambo
kinayoyapigania, kinaweza kutumia agenda ya ufisadi na matumizi mabaya
ya rasilimali za umma kuwavutia wananchi na kuchaguliwa.
SOURCE: MWANANCHI