Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Posted Ijumaa,Oktoba4 2013 saa 18:42 PM
Posted Ijumaa,Oktoba4 2013 saa 18:42 PM
Kwa ufupi
- Mnyika: "Katika sheria ya magazeti kifungu cha 25 hawajakigusa kabisa, badala yake wamegusa kifungu cha 36 na 37 tena kwa kuongeza faini."
- Mbali na kufungiwa sasa yapendekezwa vilipe faini ya Sh 5milioni badala ya Sh 150,000.
Dar es Salaam. Siku sita baada
ya Serikali kuyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania kwa madai ya
kuandika habari za uchochezi, Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kimeibuka na kueleza jinsi Serikali ilivyowasilisha bungeni
Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa 2013, ikiwemo sheria ya
magazeti ya mwaka 1976 na kuongeza faini kutoka Sh150,000 hadi Sh5
milioni.
Kimesema muswada huo mbali na kulenga kuviminya
zaidi vyombo vya habari, pia unalenga kuwabana wananchi katika haki yao
ya kutoa maoni, kwamba hata katika kifungu cha kanuni za adhabu
imependekezwa faini ya Sh5 milioni kwa watakaoandika maneno ya chuki na
uchochezi.
Kutokana na hali hiyo, chama hicho kimeitaka
Serikali kuwasilisha jedwali la mabadiliko ya muswada huo kabla ya
kuanza kwa vikao vya kamati za Bunge Octoba 16 mwaka huu, kutishia
kuwasilisha hati ya dharura marekebisho ya sheria hiyo bungeni kama
mabadiliko hayatafanyika.
Kimeeleza kuwa uamuzi huo wa Serikali unalenga
kuvifunga mdomo vyombo vya habari, katika kipindi hiki cha mchakato wa
kuandika Katiba Mpya na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Mkurugenzi
wa habari na uenezi wa Chadema, John Mnyika alisema katika muswada huo,
hakuna sehemu iliyopendekeza kufanyiwa marekebisho kifungu cha 25 cha
sheria hiyo ya magazeti, ambacho kinaipa mamlaka Serikali kuyafungia
magazeti, bila kuhitaji utetezi wowote, huku yenyewe ikiwa ndio mshtaki
na mtoa adhabu.
Mnyika alisema muswada huo ulisomwa kwa mara ya
kwanza katika mkutano wa bunge uliopita na utajadiliwa katika mkutano
ujao wa bunge, utakaoanza mwishoni mwa mwezi huu.
“Katika sheria ya magazeti kifungu cha 25
hawajakigusa kabisa, badala yake wamegusa kifungu cha 36 na 37 tena kwa
kuongeza faini” alisema na kuongeza;
“Vifungu hivi vinasema kuwa ukiandikwa uchochezi
au uongo faini ni Sh150,000, lakini katika mapendekezo wanataka faini
iwe Sh 5milioni, wakati huo huo kifungu cha adhabu ya kuyafungia
magazeti hakijaguswa kabisa wakati ndio kinachopigiwa kelele na wadau wa
habari kuwa hakifai.”
Mnyika alisema kinachofanywa na serikali ni
kujaribu kuvibana vyombo vya habari na wananchi kutojadili au kutoa
maoni ya jambo fulani, “Vyombo vya habari vinajiendesha katika mazingira
magumu, hizi faini zinaongezwa ili iweje.”
Alisema tayari muswada huo umeshachapishwa katika
gazeti la serikali tangu Agosti 23 mwaka huu, huku akiwataka wadau wa
habari kupaza sauti na kupinga mapendekezo hayo, kushinikiza yachukuliwe
mapendekezo ambayo waliwahi kuyatoa miaka ya nyuma juu ya kubadilishwa
kwa sheria hiyo.
“Hata katika kanuni za adhabu kifungu cha 55,63 na
63(b), wamependekeza kuongezwa adhabu kwa watu watakaozungumza jambo
lolote litakalotafsiriwa kuwa ni uchochezi na chuki, ingawa wamelenga
katika masuala ya dini, ukabila na mengineyo, lakini lengo lao kuwabana
wasema kweli” alisema Mnyika.
Alisema mapendekezo hayo yanalenga kuwanyima
wananchi haki ya kutoa maoni, kwamba kifungu hicho kitawanyima uhuru na
haki hata wale watakaokuwa wakitoa hotuba mbalimbali.
“Wanafanya hivi ili watu wasihoji kuhusu Katiba, wasihoji kuhusu uchaguzi mkuu, wasipofanya mabadiliko katika muswada huu tutajua wazi kuwa suala hilo linahitaji hati ya dharura ili kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi bungeni” alisema.
SOURCE: MWANANCHI
“Wanafanya hivi ili watu wasihoji kuhusu Katiba, wasihoji kuhusu uchaguzi mkuu, wasipofanya mabadiliko katika muswada huu tutajua wazi kuwa suala hilo linahitaji hati ya dharura ili kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi bungeni” alisema.
SOURCE: MWANANCHI