Saturday 2 November 2013

Migogoro ya wafugaji, Operesheni Tokomeza Ujangili kuwang'oa Mawaziri

Mizengo Pinda Kushindwa kuzuia mauaji kwa wananchi wakati wa utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Ujangili Kauli aliyoitoa bungeni kuwa wahalifu wapigwe tu, inatumiwa vibaya na askari wanaoendesha Operesheni Tokomeza Ujangili. Picha na Maktaba 
Na Habel Chidawali, Mwananchi

Posted  Novemba2  2013  saa 1:12 AM
Kwa ufupi
Pinda pamoja na mawaziri hao wanatakiwa kuachia ngazi kama hatua ya kuwajibika kutokana na matukio ya vifo na baadhi ya watu kujeruhiwa, katika matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili kwa upande mwingine.

Dodoma. Waziri Mkuu Mizengo Pinda pamoja na mawaziri wake wawili; Khamisi Kagasheki (Maliasili na Utalii) na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo, Dk Mathayo David wameingia matatani kutokana na shinikizo linalowataka wang’oke katika nafasi zao.
Pinda pamoja na mawaziri hao wanatakiwa kuachia ngazi kama hatua ya kuwajibika kutokana na matukio ya vifo na baadhi ya watu kujeruhiwa, katika matukio ya migogoro ya wakulima na wafugaji kwa upande mmoja na utekelezaji wa Operesheni Tokomeza Majangili kwa upande mwingine.
Jana wabunge walicharuka na kuwataka mawaziri waliohusika katika Operesheni Tokomeza Ujangili wawajibishwe wakieleza kutoridhishwa na maelezo waliyoyatoa mapema jana, baada ya kipindi cha maswali na majibu.
Kelele za wabunge zilizuka baada ya wabunge kuanza kuchangia maelezo ya Serikali kuhusu migogoro ya wafugaji na wakulima, hifadhi za wawekezaji na maelezo ya Serikali kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili.
Aliyekuwa wa kwanza kuchangia mjadala huo ni Mbunge wa Kilolo, Profesa Peter Msola (CCM) ambaye katika hitimisho lake alitoa hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kuchunguza kile ambacho alikiita kuwa ni unyanyasaji wa wafugaji na uporaji wa mifugo yao.
Profesa Msola alielekeza shutuma zake kwa Serikali kuwa ilifanya operesheni zake kwa pupa bila kufanya maandalizi hivyo kuwaathiri wananchi wasiokuwa na hatia.
Spika wa Bunge, Anne Makinda kabla ya kuahirisha kikao cha Bunge jana mchana aliridhia kuundwa kwa Kamati Teule ya Bunge kwa ajili ya kuchunguza migogoro baina ya wakulima na wafugaji, wakati ‘madudu’ ya Operesheni Tokomeza Majangili yatachunguzwa kupitia Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira.
Chimbuko la hoja
Jana asubuhi kabla ya Bunge kuanza kikao chake, Spika Makinda alitoa taarifa kwamba Kikao cha Kamati ya Uongozi kingekutana wakati kipindi cha maswali na majibu kikiendelea, kwa lengo la kutoa mwelekeo wa mjadala wa hoja za dharura.
Hoja hizo ni zile zilizotolewa na wabunge wawili kwa nyakati tofauti; Alphaxard Kangi Lugora wa Mwibara (CCM) kuhusu Operesheni Tokomeza Majangili na Saidi Nkumba wa Sikonge (CCM), kuhusu vita baina ya wakulima na wafugaji.
Kamati hiyo ilikutana baada ya kipindi cha maswali na majibu na Spika Makinda alitoa taarifa za kusitisha shughuli nyingine, ili wabunge waweze kujadili masuala hayo ambako kabla ya kuanza mjadala aliwaita mawaziri kutoa taarifa zao.'
Alianza Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Kagasheki ambaye katika maelezo yake alihitimisha kwa kutangaza kusitisha Operesheni Tokomeza ili kupitia mpango huo na kufanya maboresho ili kuondoa upungufu uliopo.

Licha ya kueleza sababu nyingi zilizofanya Serikali kuendesha operesheni hiyo, alisema ina manufaa makubwa katika kuokoa wanyama aina ya tembo, lakini waziri alihitimisha kwa kusema itakuwa ni busara kuifanyia tathmini wakati ikiendelea, hivyo kutangaza kuisitisha mara moja.
Kwa upande wake Dk Mathayo alitoa maneno ya kuomba radhi na kuwapa pole watu waliopatwa na usumbufu ikiwa ni pamoja na kupoteza mali zao na mifugo.
Mathayo aliwaeleza wabunge kuwa Serikali imepanga kujenga malambo katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wafugaji kupata maji ili kupunguza safari za kuhamahama kutoka eneo moja kwenda jingine.
Shinikizo kwa Pinda
Baada ya kumaliza hotuba zao, wabunge kadhaa walipata nafasi ya kuchangia maelezo hayo huku wengi wakielekeza shutuma zao kwa mawaziri hao na wenzao wa Mambo ya Ndani ya Nchi na yule wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Wabunge wawili wa Chadema, Paulina Gekul (Viti Maalumu) na John Shibuda (Maswa Mashariki) walitaka Waziri Mkuu Pinda ajiuzulu kutokana kushindwa kwake kudhibiti mauaji na mateso kwa wananchi.
Gekul alisema kinachotokea sasa ni utekelezaji wa kauli ya Pinda aliyoitoa bungeni akisema wahalifu wapigwe tu pamoja na ile ya Kagasheki aliyoitoa mjini Arusha akisema majangili watakaokamatwa wamalizwe hukohuko kwenye hifadhi.
Mbunge huyo alieleza operesheni hiyo kwamba imesababisha mauaji ya watu wasio na hatia ikiwemo mama Emiliana ambaye alifuatwa akiuza nyanya, lakini akateswa hadi kufa na hadi sasa mwili wake bado uko katika Hospitali ya Babati baada ya wananchi kugoma kuuzika.
Shibuda kwa upande wake alisema Pinda anapaswa kufungua milango kwa mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu haraka, kutokana na kulea uzembe ambao umesababisha madhara makubwa kwa wafugaji.
Shibuda alisema kuwa Wizara ya Mifugo imekuwa na mtazamo hasi lakini akasisitiza kuwa uzembe wa viongozi wa ngazi za mikoa, wilaya hadi vijiji unatokana na ukimya wa Pinda ambaye anashindwa kuchukua hatua yoyote dhidi yao.
Wabunge wengine
Kwa upande wake Nkumba aliunga mkono kuundwa kwa kamati teule, lakini akasisitiza kuwa mawaziri hao wanne wana hoja za kujibu ndani ya chama tawala CCM na kwa Rais, vinginevyo Serikali haipaswi kuendeshwa na viongozi wazembe wa aina hiyo.

“Mawaziri mnaosimamia jambo hilo mnayo hoja ya kujibu kwa chama chenu tena bahati nzuri wote mnatoka CCM, ambao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ninyi wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Maliasili na Utalii, nasema hatuko pamoja na watu wazembe hata siku moja,” alisema Nkumba.
Mbunge huyo alionya kuwa umefika wakati ambao Serikali inatakiwa iache tabia ya kuwadanganya wabunge kuwa itapeleka taarifa bungeni, lakini mambo yakishapoa basi inakaa kimya na akataka maelezo ya kina majangili wakubwa wako wapi, na kwa nini wasikamatwe na badala yake kinachofanyika ni kuendelea kuwatesa wasiokuwa na hatia, kisha akashawishi wabunge wote wazikatae taarifa za mawaziri hao.
Naye Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola alizikataa taarifa za mawaziri wote wawili kwa madai ya kupikwa na kujaa giliba za kuwahadaa wananchi.
“Mawaziri hawa wataponea wapi katika mkono huu, watu wamekufa, wameteswa, mifugo imeporwa na mingine kupigwa risasi wao wapo tu, nasema wataponea wapi ikiwa ushahidi wote uko hapa,” alisema Lugola na kuongeza:
“Mawaziri hawa wataponea wapi kama damu ya Dasu Lutaligula (Kilombero), Madirisha Luchagula (Mulele), Baya Tambi (Ulanga) wafugaji watano waliokufa huko (Mtimbira- Ulanga ), vilema vya kudumu Luhende, Ofisa Tarafa (Mpimwe) Diwani wa Maji Moto, wafugaji watano wa Mtimbira waliopata vilema kutokana na waliyotendewa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, hivi wataponea wapi kwa damu za hao?”
Alisema zaidi ya ng’ombe 500 walipigwa risasi katika mpango wa mradi wa watu wachache wa kutaka kujinufaisha wenyewe ama kwa kushirikiana na viongozi wa juu.
Aliwatuhumu askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), polisi na askari wa wanyamapori, kuwa wamekuwa wakiua watu ovyo na wengine kubakwa, lakini Serikali inawakingia kifua hali inayoonyesha kuwa kuna udhaifu ndani ya Serikali.
Katika michango yao, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Bulaya (CCM) alisema maelezo yaliyowasilishwa na mawaziri ni mzaha, huku akiwaonya mawaziri kuacha tabia ya kupuuza hoja za wabunge, kwani wanapozungumza huwa tayari wamefanya utafiti.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Magdalena Sakaya (CUF) na Mbunge wa Kuteuliwa James Mbatia (NCCR-Mageuzi), walisema yote yametokea kutokana na uzembe wa viongozi ikiwemo mawaziri kushindwa kutimiza wajibu wao.
Hadidu za rejea
Jana jioni Spika wa Bunge, Anne Makinda alimpa nafasi Profesa Msola, ili aelezee malengo ya kamati teule itakayoundwa ambapo alisema itakuwa na jukumu la kuchunguza na kuchambua sera mbalimbali zinazohusu ardhi, kilimo, mifugo, maji, wanyamapori na uwekezaji ili kubaini kasoro za ardhi, hatimaye kuleta mapendekezo bungeni yatakayoondoa migogoro ya ardhi inayoendelea kati ya wakulima, wafugaji, hifadhi, uwekezaji na watumiaji wengine wa ardhi.
Alizitaja hadidu za rejea za kamati teule kuwa ni kuchambua sera mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi kubainisha kasoro zilizopo katika sera hizo, kuchunguza mikakati iliyowekwa na Serikali, kuchambua mikakati yote ya Serikali ya kusuluhisha migogoro ya wakulima na wafugaji.
Nyingine ni kuchambua mikakati ya kulinda vyanzo vya maji, uharibifu wa mazingira na kutoa mapendekezo yatakayoondoa migogoro yote kudumisha uhusiano mzuri na utengamano na mambo mengine ambayo kamati itaona yanafaa.
Akiboresha hadidu za rejea Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), alisema ni vyema kamati teule hiyo ikapitia ripoti mbalimbali tume na kamati zilizoundwa kuchunguza suala ya matumizi ya ardhi ikiwemo ya Profesa Shivji.
Alisema kuwa kumekuwa na kawaida ya kuunda tume ambazo zimekuwa ni siri na utekelezaji wake hakuna.
Mnyika alisema kuwa ni vyema katika kuongeza hadidu za rejea ya kushughulikia uwajibikaji pale ambapo kuna kasoro za utendaji.
Mbunge wa Tunduru Abdallah Mtutura (CCM), alisema wapo watu ambao wameuawa kwa kisingizio kuwa ni majangili huku wengine wakijificha maporini kuogopa operesheni hiyo.
Aliunga mkono kuongezwa kwa hadidu ya kuchunguza mauaji na watu walioteswa katika operesheni hiyo.
Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama (CCM), alitaka kuwepo kwa muda maalumu wa kamati teule kufanya kazi kwa kuwa jambo hilo ni zito.
Alisema kumekuwa na tume nyingi ambazo hazijaonyesha matokeo yake na kutaka kamati hiyo itakayoundwa iwe ya mwisho katika utekelezaji.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali (NCCR- Mageuzi), alisema operesheni hiyo imefanya zaidi ya ugaidi na unyama na kuomba waliohusika na mauaji na utesaji wa watu kupimwa akili.
Kwa upande wake Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohamed Mnyaa, (CUF), alitaka kuwepo kwa fidia kwa watu walioathirika na operesheni hiyo.
Akihitimisha hoja hiyo, Profesa Msola alisema mapendekezo yote yataingizwa katika hadidu za rejea ili yasaidie katika utendaji wa kamati hiyo teule.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema majina ya wabunge watakaounda kamati hiyo, yatatajwa Jumatatu ijayo.
 
SOURCE: MWANANCHI