Wednesday 16 October 2013

Dk Ndalichako kufanya utafiti wa uendeshaji mitihani

Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (Necta),Dk Joyce Ndalichako PICHA|MAKTABA 
Na Fredy Azzahi, Mwananchi

Posted  Jumatano,Oktoba16  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Dk Msonde alisema kuwa, likizo ya Dk Ndalichako ilianza Oktoba Mosi mwaka huu na itamalizika Septemba mwakani.


Dar es Salaam. Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Nchini (Necta),Dk Joyce Ndalichako, ameanza likizo ya mwaka mmoja kwa kile kilichoelezwa kuwa anafanya utafiti juu ya uendeshaji wa mitihani nchini.
Akizungumza na Mwananchi jana, Dk Charles Msonde ambaye ndiye anayekaimu nafasi ya Katibu Mtendaji wa Necta, alisema Dk Ndalichako amechukua likizo ya mwaka mmoja kwa ajili ya kufanya utafiti huo.
Dk Msonde alisema kuwa, likizo ya Dk Ndalichako ilianza Oktoba Mosi mwaka huu na itamalizika Septemba mwakani.
“Amechukua sabbatical leave, kwa wanataaluma ama watu walio kwenye ngazi kama zetu wanaweza kuchukua likizo kama hii. Yeye atakuwa anafanya utafiti unaohusu uendeshaji wa mitihani hapa nchini na pia ataangalia mambo ya matumizi ya alama za maendeleo za mwanafunzi (continuous assessment – CA),” alisema Dk Msonde:
“Utafiti huo utakuwa na manufaa kwa shirika na kwa kuwa yeye ni Rais wa Mabaraza ya Mitihani Afrika atapata nafasi ya kuangalia wenzetu wanafanya nini, kwa hiyo utafiti wake ataufanya ndani na nje ya nchi. Utafiti huu utakuwa na manufaa kwa baraza na nchi nzima.”
Agosti mwaka huu Mwananchi ilifanya mahojiano Maalumu na Dk Ndalichano ambapo alizungumzia vitu mbalimbali ikiwamo kile alichosema ni tishio kwa Necta.
Alisema kuwa,kitu ambacho anaona ni tishio kwa baraza hilo ni mitizamo ya watu ambao kwa kiasi kikubwa wanakataa ukweli.
“Suala la ukweli unataka lisiwe kweli, mimi naona hiyo ni hatari mbaya zaidi, huwezi kutibu tatizo bila kujua ukweli, ili tuweze kuboresha elimu lazima tukubali ukweli na kujirekebisha,” alisema Dk Ndalichako.
Alizungumzia pia ubora wa mitihani na kusema, mitihani inayotungwa na Necta ubora wake upo juu pamoja na usahihishaji wake.
Alisema mfumo wa kila mwalimu anasahihisha swali lake ni wa kipekee na Tanzania ni moja kati ya nchi za mwanzo kutumia mfumo huo.
“Kuna nchi mtu anapewa burugutu la mitihani ya watoto anaenda nayo nyumbani kusahihisha akishamaliza analeta majibu kisha watoto wanatangaziwa. Sisi mfumo wetu ni bora na sijui kwa nini watu wanakuwa na mtizamo hasi na Necta, sifa kubwa ya baraza lolote lile la mitihani ni kutoa majibu yanayofanana na hali halisi ya elimu ilivyo” alisema.
“Kwetu sisi tunachotaka siku zote kuona mtu anapewa kile anachostahili, watu wengine wanasema mitihani inayotungwa na kupewa watoto wote siyo sawa kwa sababu kuna baadhi ya shule walikuwa hawana walimu au vitabu, sasa swali la kujiuliza nani alitakiwa kutoa hivyo vitabu?” alisema Dk
 Ndalichako.

SOURCE: MWANANCHI