Wednesday 16 October 2013

Zitto asimamisha ruzuku za mwezi kwa vyama vya siasa

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac),Zitto Kabwe PICHA |MAKTABA 
Na Raymond Kaminyoge, Mwananchi

Posted  Jumatano,Oktoba16  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi

Alisema baada ya siku mbili za kazi atakuwa na majibu ya kuridhisha kuhusiana na suala hilo.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (Pac),Zitto Kabwe amevilipua vyama vya siasa kwa uvunjaji wa sheria na kusimamisha ruzuku ya kila mwezi hadi vitakapowasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha za umma tangu mwaka 2009 kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Pia kamati hiyo itawaweka kitimoto makatibu wakuu wa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku ili wajieleze ni kwa nini hawajawasilisha taarifa hiyo hadi sasa.
Alisema hayo jana wakati kamati hiyo ilipokutana na Msajili wa Vyama vya Siasa katika Ofisi ndogo za Bunge.
Zitto alisema tangu mwaka 2009 vyama tisa vya siasa vinavyopewa ruzuku na Serikali vilipata jumla ya Sh67.7 bilioni lakini havijawahi kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa ruzuku kwa msajili kama vinavyopaswa kufanya hivyo kisheria.
“Ninaagiza msajili kuanzia sasa ruzuku isitolewe kwa chama chochote cha siasa hadi hapo kitakapowasilisha ripoti ya ukaguzi wa hesabu tangu mwaka 2009 hadi sasa na makatibu wataitwa ili wajieleze kwa nini hawajafanya hivyo,” alisema.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nauye alipoulizwa jana alisema: “Ninahitaji muda kuangalia kama kweli taarifa hiyo haijawasilishwa na sheria inasemaje kuhusu suala hilo,” alisema.
Alisema baada ya siku mbili za kazi atakuwa na majibu ya kuridhisha kuhusiana na suala hilo.
Viongozi wengine wa vyama vya siasa vinavyopata ruzuku, hawakupatikana kuelezea hali hiyo. Zitto aliongeza,“ Hivi ni vyama vya siasa ambavyo wakati ukifika vinaweza kuja kuongoza Serikali, lakini inashangaza ni kwa nini vinatumia fedha za walipakodi bila kukaguliwa, huu ni uvunjaji wa sheria.”
Kwa mujibu wa Zitto, vyama hivyo na fedha za ruzuku walizopata kwenye mabano tangu mwaka 2009 ni CCM (Sh50.9 bilioni), Chadema (Sh9.2 bilioni) na CUF (Sh 6 bilioni).
Vingine ni NCCR-Mageuzi(Sh677 milioni),UDP (Sh333 milioni), TLP (Sh217 milioni), APPT-Maendeleo (Sh217 milioni), DP (Sh3.3 milioni) na Chausta (Sh2.2 milioni).
Zitto alisema ingawa jukumu la ukaguzi wa fedha za umma ni la ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali lakini hakufanya hivyo kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.
Alisema vyama vya siasa viliagizwa kufanya ukaguzi kwa kutumia kampuni binafsi kama vilivyokuwa vikifanya zamani hadi hapo ofisi ya CAG itakapopata fedha.

Mwenyekiti huyo alitoa wito kwa msajili kuviagiza vyama vya siasa kutenga sehemu ya fedha za ruzuku kwa ajili ya ukaguzi.
Alisema viongozi hao waone kwamba suala la ukaguzi wa fedha za ruzuku ni muhimu ili kuleta uwazi katika matumizi ya fedha za umma.
“Sasa kamati imeshindwa kuendelea na kazi kwa sababu hakuna hesabu zilizokaguliwa, nendeni tutawaita siku nyingine,” alisema.
Kwa upande wake, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema vyama hivyo vimekuwa vikidai kwamba havina ruzuku ya kufanya ukaguzi kwa kutumia kampuni binafsi.
“Kwa hiyo siwezi kuchukua fedha nikavipa vyama vya siasa kwaajili ya ukaguzi wakati hazijatengwa katika bajeti,” alisema.
Hata hivyo,Zitto alimwelekeza Mutungi kwamba fedha za ukaguzi ziko kwenye ruzuku wanazopewa na kwamba hiyo siyo sababu ya kuhalalishwa kutokaguliwa kwa hesabu zao.

SOURCE: MWANANCHI