Wednesday 16 October 2013

Upelelezi kesi ya aliyewahi kumfadhili Odinga bado


Na Tausi Ally, Mwananchi

Posted  Jumatano,Oktoba16  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni ile inayohusu kutakatisha fedha haramu takriban Sh6 bilioni kati ya mwaka 2009/10.


Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya kutakatisha fedha haramu zaidi ya Sh6 bilioni, inayomkabili aliyekuwa mfadhili wa mgombea urais wa Kenya, Raila Odinga, Donbosco Gichana (34) bado haujakamilika.

Hayo yalielezwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumaini Kweka alipokuwa akiiomba mahakama iridhie mshtakiwa huyo achukuliwe kwenda kuhojiwa polisi kwa muda wa siku saba.
Kweka alimweleza Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Ilvin Mugeta kuwa, anaiomba mahakama iruhusu mshtakiwa Gichana kupelekwa polisi kwa ajili ya mahojiano kuhusiana na shtaka hilo linalomkabili.
Baada ya kutolewa kwa ombi hilo, Hakimu Mugeta aliridhia mshtakiwa huyo kuchukuliwa kwa muda wa siku saba kwa ajili ya mahojiano.
Gichana alipanda kizimbani kwa mara ya kwanza mwanzoni mwa mwaka huu na kusomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi, Emilius Mchauru.
Mshtakiwa huyo alifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani hapo, mwanzoni mwa mwaka huu na kusomewa mashtaka mawili ya kutakatisha fedha haramu.
Katika shtaka la kwanza, Gichana anadaiwa kukutwa akiwa na washtakiwa wengine ambao hawajulikani kati ya Novemba 2009 na Agosti 2010 jijini Nairobi, Kenya, Arusha na Dar es Salaam wakila njama ya kutakatisha fedha haramu.
Wakili wa mshtakiwa huyo, Semu Anney alidai mteja wake alikuwa mfadhili mkuu wa Raila Odinga katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007, Kenya na ndiye aliyempa gari aina ya Hammer kwa ajili ya kufanyia kampeni wakati huo.
Inadaiwa mshtakiwa alifanya kosa hilo kinyume cha kifungu namba 12 cha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha haramu namba 12 ya mwaka 2006.
Katika shtaka la pili, Gichana anashtakiwa kuwa kati ya Novemba 2009 na Agosti 2010 kwa kupotosha ukweli wa chanzo cha fedha alizokuwa nazo, alihamisha Dola za Marekani 4.9 milioni na kuziweka katika akaunti namba 02J1036325000 inayomilikiwa na Moyale Precious Germs Enterprises.
Inadaiwa kuwa mshtakiwa alihamisha tena kwa kutumia hundi kutoka tawi la Benki ya CRDB Tawi la Meru mkoani Arusha kwenda Makao Makuu ya benki hiyo Dar es Salaam kwa nia ya kufanya utaratibu wa kuzitoa huku akijua hundi hiyo ni ya kughushi.
Mshtakiwa huyo hakuruhusiwa kuongea chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo.

SOURCE: MWANANCHI