Kwa ufupi
Akikaririwa na gazeti la Nyasa Times, Mutharika alisema Tanzania haina cha kuambulia kwa Ziwa Malawi.
Mashirika. Mgombea Urais wa Democratic
Progressive Party (DPP) nchini Malawi, Peter Mutharika, amesema hakuna
sababu za kufanya majadiliano kuhusu Ziwa Malawi ambalo Tanzania
wanaliita Ziwa Nyasa.
Mutharika, ambaye ni mwanasheria, aliyasema hayo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika juzi Mkoa wa Kati.
Akikaririwa na gazeti la Nyasa Times, Mutharika alisema Tanzania haina cha kuambulia kwa Ziwa Malawi.
Kiongozi huyo ambaye hakuwapo katika mkutano wa
Rais Joyce Banda na wapinzani kuzungumzia mustakabali wa ziwa,
aliwahakikishia Wamalawi kuwa wasiwe na wasiwasi wa mvutano huo.
Mutharika ziwa lote ni mali ya Malawi na akisisitiza kuwa, Tanzania haina hata punje ya eneo.
“Hakuhitajiki majadiliano, Ziwa Malawi ni mali ya
Malawi, litakuwa la Malawi,” alisema Mutharika ambaye alichukua masomo
ya Sheria Tanzania.
“Tanzania inatumia nafasi ya udhaifu wa uongozi
wetu, lakini ukweli, hawana hata tone la eneo... Tutakapoitwa kwenye
uchaguzi ujao mwakani, tutamaliza haya yote. Nitaleta meli nyingi kwa
ajili ya maendeleo ya uchumi, kutengeneza ajira za kutosha kwa vijana,”
alisema Mutharika huku akishangiliwa na wafuasi wake.
Tanzania inataka kugawana ziwa, lakini Malawi
imegomea mpango huo na suala hilo liko katika majadiliano ambayo Banda
alisema kama mwafaka haukupatikana ifikapo Septemba 30, Malawi itapeleka
suala hilo Mahakama ya Kimataifa (ICJ).
source: Mwananchi news paper
source: Mwananchi news paper